Kipa Azam asaka namba

BAADA ya kuzikosa mechi mbili mfululizo Kipa wa Azam FC, Benedict Haule amesema hajakata tamaa na anaamini muda ukifika atapangwa na atafanya vizuri kutokana na uwezo alionao.

Haule ambaye alisajiliwa Azam msimu wa 2017/18 akitokea Mbao FC ya jijini hapa ambapo hata msimu uliopita alianza msimu akiwa benchi kabla ya raundi ya pili mambo kumnyookea na kuwa chaguo la kwanza mbele ya aliyekuwa mpinzani wake, Razack Abarola.

Msimu huu ni kama historia inajirudia, kwani katika mechi mbili walizocheza na kushinda, Kocha wa kikosi hicho, Aristica Cioaba ameonekana kukubali kazi ya David Kisu.

Haule alisema anaendelea kujituma mazoezini ili kumshawishi kocha kumpa namba. Alisema hana wasiwasi na kiwango chake na kama muda wake utafika wa kuaminiwa na benchi la ufundi anaamini atafanya vizuri na kuisaidia timu kufikia malengo.

“Njia ya kumshawishi kocha ni kupambana kwenye mazoezi ili siku nikipangwa nifanye vizuri na kudumu na namba kikosini, sina wasiwasi na uwezo wangu na ninaweza kufanya vizuri” alisema Haule.