Iheanacho arudishwa kikosini Nigeria upyaa

Muktasari:

Iheanacho aliondoshwa kwenye kikosi cha Nigeria Machi, wakati Kocha Gernot Rohr alipohoji umuhimu wake kwenye timu kwa sababu alikuwa hapati nafasi ya kucheza huko King Power.

LEICESTER, ENGLAND. STRAIKA wa Leicester City, Kelechi Iheanacho amerudishwa kwenye kikosi cha Nigeria baada ya kuwekwa kando kwenye kile kikosi kilichoshiriki mikikimikiki ya Afcon 2019 huko Misri.

Iheanacho aliwekwa kando kwenye kikosi hicho cha Super Eagles kilichomaliza nafasi ya tatu huko Misri, lakini sasa amerudi kwenye timu hiyo ya Taifa ya Nigeria kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Ukraine.

Staa mwingine wa Leicester City, Wilfred Ndidi, aliyekuwa nyota wa Nigeria kwenye Afcon, naye amejumuishwa kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa huko Dnipro, Septemba 10.

Iheanacho aliondoshwa kwenye kikosi cha Nigeria Machi, wakati Kocha Gernot Rohr alipohoji umuhimu wake kwenye timu kwa sababu alikuwa hapati nafasi ya kucheza huko King Power. Baadaye akawekwa kwenye kikosi cha awali cha Super Eagles kabla ya kuondolewa kwenye orodha ya kikosi cha mwisho kabisa kilichokwenda kwenye Afcon 2019.

Kipindi hicho fowadi huyo alikuwa anakaribia mwaka bila ya kufunga bao, huku mara yake ya mwisho kufunga ilikuwa kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Huddersfield Town, Septemba 22, 2018.

Hata hivyo, Iheanacho amefunga mara tatu kwenye mechi za kujianda na msimu huu, akipiga kwa kichwa dhidi ya Cambridge kabla ya kufunga mara mbili kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Rotherham.