Ighalo atengwa na wenzake

Muktasari:

Virusi vya Corona vilivyoanzia huko China vimepoteza maisha ya watu zaidi ya 1,100. Straika huyo Mnigeria hakujumuishwa kwenye kikosi cha Man United kilichokwenda kuweka kambi ya mazoezi huko Hispania kwa hofu hiyo ya virusi hivyo.

MANCHESTER,ENGLAND .STRAIKA mpya wa Manchester United, Odion Ighalo amepigwa marufuku kusogelea uwanja wa mazoezi wa timu hiyo huko Carrington kutokana na hofu ya kuogopa maambukiza ya virusi vya corona.

Ighalo, ametua Man United kwa mkopo akitokea Shanghai Shenhua ya China, mahali ambako kuna maambukizi makubwa ya virusi vya Corona. Staa huyo amekuwa akifanya mazoezi na kocha wake binafsi huko kwenye eneo jingine ndani ya Jiji la Manchester.

Virusi vya Corona vilivyoanzia huko China vimepoteza maisha ya watu zaidi ya 1,100. Straika huyo Mnigeria hakujumuishwa kwenye kikosi cha Man United kilichokwenda kuweka kambi ya mazoezi huko Hispania kwa hofu hiyo ya virusi hivyo.

Watu wengi wanaotoka China wamekuwa wakikumbana na zuio la kuingia kwenye nchi mbalimbali kutokana na hofu ya kusambaa kwa virusi hivyo ambavyo vinaangamiza maisha ya watu.

Ighalo atakuwa kwenye zuio hilo kwa muda wa siku 14 kuona kama kuna tatizo lolote.

Ighalo hakutokea kwenye mji wa Wuhan, ambako virusi hivyo vimesambaa kwa kasi, lakini Man United ilichukua tahadhari ya kumweka mbali wakimtaka afanye mazoezi peke yake kabla ya kujumuika na wenzake baadaye.

Wakati wenzake walipokuwa kambini huko Marbella, Hispania, staa Ighalo alibaki England akijifua chini ya kocha binafsi.