Ighalo anogewa Manchester United, kusaini dili jipya kwa 15M

Wednesday March 25 2020

Ighalo anogewa Manchester United, kusaini dili jipya kwa 15M,OLD Trafford ,Manchester United,

 

Manchester, England .OLD Trafford kutamu aisee asikwambie mtu na sasa supastaa wa Nigeria, Odion Ighalo ameamua kuhamia jumla na mabegi yake. Ndio, Ighalo ambaye yuko kwa mkopo Manchester United ameripotiwa kuwa kwenye mchakato wa kukamilisha uhamisho wa jumla kukipiga na wababe hao.

Ighalo aliyenaswa na United dirisha dogo la usajili la Januari akitokea Shanghai Greenland Shenhua ya Ligi Kuu ya China, atasaini dili jipya baada ya kiwango chake kuwavutia mabosi wa United.

Mkataba wa sasa wa mkopo wa Ighalo unafikia tamati mwezi Mei, mwaka huu, wakati huu ligi zote zikiwa zimesimama kutokana na kusambaa kwa virusi vya Corona. Kwa maana hiyo kwa mujibu wa mkataba wa sasa na kama mambo yatabaki kama yalivyo basi, Ighalo hatamaliza msimu akiwa na Man United.

Kutokana na hilo, mabosi wa Man United na Shenhua wameanza majadiliano huku ikielezwa mshambuliaji huyo atagharimu Pauni 15 milioni.

Awali, Ighalo alifichua tangu akiwa mtoto alikuwa na ndoto ya kuichezea United na siku anapigiwa simu na wakala wake kuelezwa kuhusu dili hilo, alitoa jibu moja tu la ndio.

Alisema wakati akipokea simu hiyo alikuwa akitoka bafuni na alimwomba wakala wake kuhakikisha anasimamia uhamisho huo ili kumwezesha kutimiza ndoto yake.

Advertisement

Kutokana na shauku ya kuichezea United, Ighalo aliamua kupunguza kiwango cha mshahara wake alichokuwa analipwa na matajiri hao wa China hadi kufikia Pauni 300,000 kwa wiki.Mshambuliaji huyo wa zamani wa Watford inayoshiriki Ligi Kuu England, alitua Shenhua mwaka 2017 kabla ya Januari, mwaka huu, kurejea tena England.

Mpaka sasa Ighalo ameifungia Manchester United mabao manne kwenye michuano yote na uwezo wake umeongeza ubora kwenye eneo la ushambuliaji akicheza sambamba na Anthony Martial, wakati huu Marcus Rashford akisumbuliwa na majeraha.

Katika hatua nyingine, kiungo mshambuliaji wa Barcelona anayekipiga kwa mkopo Bayern Munich ya Ujerumani, Phillipe Coutinho anajiandaa kurejea kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Habari kutoka kweye korido za Camp Nou, zinaeleza wababe hao wamepanga kumuuza Coutinho jumla kwenda Chelsea.

Coutinho alitua Barcelona kwa dau nene la euro 142 milioni mwaka 2018 akitokea Liverpool na alikuwa kwenye kiwango cha juu.

Hata hivyo, akiwa Barcelona alishindwa kuendeleza makali yake na muda mfupi akasukumiwa Bayern kwa mkopo na mwishoni mwa msimu huu, atauzwa jumla ili pesa yake kutumika kumrejesha Neymar Jr Catalunya.

Hata hivyo, Arsenal, Tottenham na Man Utd nazo zimekuwa zikifuatilia maendeleo ya Mbrazili huyo na huenda zikajitosa kusaka huduma yake.

Advertisement