Ibra Class afunguka ishu za misosi yake kwa Trump

Monday May 13 2019

 

By IMANI MAKONGORO

KIBONGOBONGO bondia kunywa kahawa kwa kashata, kisha akaenda kupanda ulingoni sio ishu, lakini Ibrahim Class anakuambia kule Marekani bondia anafanya kila kitu kwa maelekezo na hasa masuala la misosi na kadhalika, jambo lililompanua akili zake.

Bondia huyo maarufu kama King Class Mawe, si unafahamu alikuwa Marekani kwa miezi saba alikokuwa akijifua kwa mkataba maalumu. Jamaa anakwambia hakuwahi kufikiria kukutana na maisha kama aliyokutana nayo Marekani, hasa kwa bondia.

“Wenzetu acha tu watambe kwenye ngumi, jamaa wako makini sana,” anasimulia Class ambaye yuko nchini kwa mapumziko mafupi.

Alisema amekutana na maisha tofauti ya mabondia wa Marekani japo mwanzo ilikuwa ngumu kuyazoea kutokana na mazingira ya Tanzania.

“Kuna tofauti kubwa sana kati yao na sisi kuanzia mazoezi yao na vyakula vya mabondia anapojiandaa na pambano na anapokuwa akijifua tu kujiweka fiti.”

Aliongeza katika mazoezi ya kule kuna kocha wa mazoezi, kocha wa mazoezi ya nguvu, kocha wa padi na mtu maalumu wa maelekezo, vyakula na vitu vingine.

“Unapokaribia kucheza pambano kuna vyakula maalumu, ambapo bondia atakula samaki, mboga za majani na matunda, lakini Kibongo Bongo hayo wala hatuna, huwa tunachukulia poa tu hata kahawa anaweza kunywa ukaenda kupigana kitu ambacho si sawa,” alisema.

Bingwa huyo wa zamani wa GBC anakwambia alichojifunza mabondia wa Bongo hawajengi wanaharibu.

Alisema kingine ambacho amejifunza kule, bondia anapokuwa na mechi muda wote anakuwa anakula.

“Sio kula kula, lakini unakula kwa utaratibu vyakula vyepesi siyo vya kushiba, unaweza kukaa baada ya saa mbili unakula hiki, baada ya muda tena unakula, yaani kifupi unakuwa unakula mara kwa mara si kwa kushiba, lakini Bongo ilikuwa umekula mihogo yako asubuhi, basi ndiyo mpaka jioni tena.”

Akizungumzia mazingira ya mazoezi kule, Class anasema kwa miezi saba aliyoishi Marekani amejifua kwenye majimbo manne tofauti. Majimbo hayo ni Washngton, Calfonia, Texas na Witches.

“Tulikuwa tunazunguka kwa ajili ya kufanya mazoezi ya Sparing (hana kwa hana), katika mazoezi hayo nimebahatika kukutana hana kwa hana na Kocha wa Manny Pacquiao ambaye alikuja katika gym niliyokuwa najifua,” alisema.

Class yuko nchini ambapo licha ya mapumziko kabla ya kurejea Marekani anatarajiwa kucheza pambano la kimataifa nchini.

Advertisement