IOC yaibeba Tanzania Olimpiki Argentina

Muktasari:

Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC),imewabeba wanariadha wa Tanzania walioshiriki michezo ya  Olimpiki ya vijana inayofanyika Argentina.

Mfumo mpya unaotumiwa na IOC umewaingiza wanariadha wa Tanzania kwenye orodha ya 10 bora.

 

Dar es Salaam.Mfumo mpya unaotumiwa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) katika michezo ya Olimpiki ya vijana inayoendelea Argentina, umewabeba wanariadha wa Tanzania ambao wameingia kwenye orodha ya 10 bora.

Tanzania imepenya baada ya mwanariadha Regina Mpigachai kumaliza mbio za marudio za mita 800  baada ya kushika nafasi ya kwanza na Francis Damiano alimaliza wa nne katika mbio nyingine za kilomita nne juzi na jana.

Awali, Damiano alikimbia mbio za mita 3,000 na kumaliza kwenye nafasi ya 12 na Regina akimaliza katika nafasi ya saba katika mbio za mchujo za mita 800 ingawa mfumo mpya wa IOC umewapa nafasi nyingine ya kufanya vizuri wawakilishi hao wa Tanzania.

IOC imeweka utaratibu wa kukimbia mbio za marudiano kwa wanariadha wanaoshiriki michezo hiyo na washindi wanapatikana kwa kujumumlisha muda katika mbio zote mbili wakipewa pointi.

"Huu ni utaratibu mpya wa IOC ambao timu yetu imekutana nao, kama kwenye soka unavyocheza mechi ya nyumbani na ugenini, ndivyo ambavyo IOC imefanya kwenye Olimpiki ya vijana," alisema Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.

Alisema Regina aliyemaliza wa kwanza katika mbio za mita 800 kwenye kundi lake, jana aliingia kwenye  10 bora kama ambavyo imetokea kwa Fabiano aliyekuwa wa saba katika matokeo ya jumla.

"Inachofanya IOC wanajumlisha muda aliokuwa amekimbia katika mchujo wa kwanza wanajumlisha na ule wa mbio za pili na kutoa pointi kwa washindi, hivyo hata Regina baada ya mgawanyo huo atakuwa amepanda," alisema Bayi.

Alisema utaratibu huo umewajengea uwezo wanariadha hao na kusisitiza kuwa, matokeo ya awali yanaonyesha yalichangiwa na uoga wa mashindano lakini baada ya kuzoea mazingira wote wawili wamefanya vizuri kwenye mbio za marudio.

Tanzania iliwakilishwa na wanariadha wawili na waogeleaji, Sonia Tumiotto na Denis Mhini ambao wameondoshwa katika hatua ya awali kwenye mashindano hayo yatakayofungwa kesho Alhamisi.