INEOS 1:59 Challenge: Eliud Kipchoge aushinda mkono wa muda!

Saturday October 12 2019

 

By Fadhili Athumani

KWA macho ya kawaida ya binadamu wa kawaida, mbio za IEOS 1:59 Challenge, si mbio ya kawaida kama ilivyo mbio nyingine. Asikudanganye mtu! Kukimbia kilomita 42 ndani ya muda huo,sio rahisi hata kidogo!
Bingwa wa Dunia wa Marathon na mshikilizi wa rekodi, Eliud Kipchoge, ambaye ni mzaliwa wa Kapsisiywa, kaunti ya Nandi, eneo la Bonde la ufa, nchini Kenya, aliuonesha ulimwengu mzima ukomo wa uwezo wa Mwana wa Adamu.
Achana na kampeni iliyofanyika dunia nzima kuhamasisha mbio hizo zisizotambulika na Shirikisho la Riadha Duniani. Sahau kabisa kuhusu pesa zilizomwagwa kudhamini mbio hizi. Sahau pia kuhusu furaha iliyoko kwenye mioyo ya Wakenya na Waafrika.


Tangu kuumbwa kwa Dunia, tulishuhudia mwanadamu akipambana na mkono wa sekundu wa saa. Jiji zima la Vienna ilisimama. Dunia nayo ikakataa kuzunguka kwa muda. ‘INEOS 1:59 Challenge’ na Kipchoge kwa kweli wametuonesha ‘No Human is Limited’
Akiongozwa na wakimbiaji ‘Pace Makers’ 41, kutoka mataifa zaidi ya 20 tofauti, bingwa huyu wa Olimpiki, alianza kukata mawimbi ya ardhi, akisaidiwa na kiatu cha kipekee kilichotenengezwa maalum (Nike ZoomX Vaporfly NEXT%), kwa ajili ya mbio hizo na Kampuni ya Nike, akikimbia nyuma ya gari maalum.
Akishindana na rekodi yake, Kipchonge alianza kampeni hiyo, taratibu kuanzia saa 3:15 asubuhi, kwa saa za Afrika Mashariki (saa moja na dakika 15 kwa saa za Austria). Kwa kasi ile ile, kilomita 20 zilimalizika ndani ya dakika 57. Dunia inashangaa?
Hadi kufikia saa 4:44 asubuhi, tayari Kipchoge alikuwa amekamilisha kilomita 31, ambapo kwa mujibu wa mkono wa muda, zilimchukua saa 1:28:03 kumaliza kilomita na kubakisha kilomita 11 tu kuweka rekodi itakayotikisa Dunia. Alihitaji dakika 28 kujishangaa!
Saa tano kamili asubuhi, zilimkuta Kipchoge akimaliza kilomita 34, akiwa ametumia saa 1:40:34 na kubakisha kilomita sita, ambazo ni sawa na dakika 19, kuweka rekodi mpya. Kufika saa 5:10 tayari alikuwa amemaliza kilomita 39, akitumia muda wa 1:52:04 ambapo zilibaki kilomita 2.6 kukamilisha mbio.

Advertisement