IGENI: Staili za mastaa zilizobamba kitaa

Muktasari:

Msimu wa 2018/19 umekuja kivingine kwa mastaa wa ligi kuu Bara, kuwa na staili mbalimbali za kushangilia na zimepata umarufu mkubwa nchini.

ZIMEIBUKA staili mbalimbali za ushangiliaji wa wachezaji wa Ligi Kuu Bara, lakini zinazoonekana kubamba zaidi kitaa na kwenye mitandao ya kijamii ni zile za mastaa wa Simba na Yanga.
Upinzani wa Simba na Yanga haujaanza leo umekuwepo miaka nenda rudi,  mashabiki kutambiana huku kila mmoja akivutia kamba kwake, wachezaji nao wameanza kutafuta staili za ushangiliaji ambazo zinafanya ziwe maarufu.
Mwanaspoti linakuletea orodha ya staili za wachezaji ambazo zimebamba msimu huu na kuwa  gumzo zaidi ni zile zilizoibuliwa na wachezaji wa Simba na Yanga zinazotumika mitaani na mitandaoni kwa mashabiki wa klabu hizo.

Meddie Kagere-Simba
Tangu Kagere ajiunge Simba alitikisa na mambo matatu makuu, staili ya kushangilia kwa kufumba jicho moja iliopata umarufu mkubwa nchini, akaja na staili ya kutembea kama babu aliyeshika fimbo, lakini pia uwezo wake uwanjani.
Simba kumsajili Kagere ilionekana wamechemka kumchukua babu na kama si kujitambua kwa staa huyo kuwajibika ipasavyo kwenye nafasi yake ya kushambulia ambapo mpaka sasa anamiliki mabao saba,  basi mambo kwake yangekuwa magumu hasa kutaniwa na watani zao Yanga.
Kama haitoshi Kagere ameibuka na staili mpya ya kufumba macho yote mawili iliyozua gumzo kwa mara nyingi kwa wadau wa soka nchini, baada ya kufunga bao mojawapo kati ya 4-1 Simba ikiibuka shujaa Uwanja wa Taifa dhidi ya Mbabane Swallows. 

Heritier Makambo-Yanga
Tangu ajiunge Yanga msimu huu, amechangia mabao saba timu hiyo kukaa kileleni kwa ikiwa na pointi 35, kila anapofunga Makambo ana staili yake ya kushangilia iliopa umaarufu mkubwa.
Yanga ikicheza na ukisikia makofi yanapigwa basi ujue Makambo kafanya mambo kwani akizitikisa nyavu za wapinzani anasogea sehemu walipo mashabiki wa timu hiyo anaanza kuonyesha ishara ya kutaka kupongezwa kwa kupigiwa makofi.
Lakini pia akimaliza kupiga makofi anaweka vidole vyake katika masikio yote mawili, akitaka kusikilizia zaidi mashabiki kama watampigia makofi ya nguvu kuonyesha saluti.

Mrisho Ngassa-Yanga
Amekuwa akionyesha staili mbalimbali, tangu msimu huu uanze Ngassa ameigilizia staili ya mwanamuziki wa Nigeria King Monada ya nyimbo yake ya Malwedhe Idibala ambayo inachezwa kwa staili ya kuanguka chini.
Mbali na staili yake ya kuanguka pia amekuwa akishangilia kwa kuonyesha ishara ya kumshukuru Mungu, wakati mwingine anabusu mkono wake.

Emmanuel Okwi-Simba
Okwi ambaye anamiliki mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara, mara nyingi akifunga amekuwa akishangilia kama sikupiga magoti ama kusimama ananyosha vidole juu kwa ishara ya kumshukuru Mungu.

Ibrahim Ajib -Yanga
Ajibu ana aina mbili za ushangiliaji, kuna wakati anavua jezi ya juu na kukimbilia kwa mashabiki huku akiipeperusha juu, lakini wakati mwingine amekuwa akipiga magoti na kusujudu ishara ya kumshukuru Mungu.

Jafary Kibaya-Mtibwa Sugar
Alipofunga Hat trick dhidi ya Northern Dynamo ya Shelisheli, mchezaji huyo alikuwa anashangilia kwa ishara ya kufanya mazoezi kama anaruka kamba.