Huyu ndo mbadala wa Hazard Madrid

Muktasari:

Kwa kuwa Mjapani Kubo hana kibali cha kucheza nchini Hispania, Zidane hana budi kumgeukia mmoja kati ya nyota hawa watano kuvaa viatu vya Hazard. Je, nani atavaa viatu hivyo?

BUNDI mweusi aliyetua Santiago Bernabeu amekataa kuondoka. Kila kukicha ni majanga tu pale Real Madrid. Kama si majeruhi ni vipigo tu. Habari mbaya kwa sasa ni kuumia kwa Eden Hazard.

Ni kwamba, Mbelgiji huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Chelsea hataingia uwanjani kwa kati ya majuma matatu au manne, hii inamaanisha Kocha Zinedine Zidane hana budi kumtafuta mbadala wake.

Kwa kuwa Mjapani Kubo hana kibali cha kucheza nchini Hispania, Zidane hana budi kumgeukia mmoja kati ya nyota hawa watano kuvaa viatu vya Hazard. Je, nani atavaa viatu hivyo?

5. RODRYGO

Mbrazil huyu, alitua nchini Hispania, na kuingia katika kikosi cha vijana cha Real Madrid ‘Castilla’, lakini uwezo aliouonyesha katika mechi za kujiandaa na msimu, ulimkuna Zidane ambaye hakusita kumjumuisha katika kikosi cha wakubwa.

Bila kupepesa, kinda huyu anaweza kuwa hazina kubwa kwa Los Blancos, kwani ni fundi wa kukokota mipira, ana kasi na pia anajua kufunga mabao. Kuumia kwa Hazard, kunaweza kukamfungulia milango ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Los Blancos.

4. BRAHIM DIAZ

Kinda huyu, alirejea uwanjani baada ya kupona jeraha lake, na kutokana na michezo kadhaa alizocheza, amethibitisha tayari kukinukisha msimu huu. Brahim Diaz, alikuwa katika kikosi akiba cha Madrid, walipoitandika Celta Vigo 3-1, ugenini.

Mhispania huyu, ndiye mchezaji pekee katika kikosi cha sasa cha Los Blancos, anayefanana na Eden Hazard kiuchezaji. staili yake ya kupiga chenga, kufunga mabao, kukokota mpira haina tofauti na uchezaji wa ‘Belgian little magician’.

Tatizo pekee linaloweza kumzuia Diaz, kuvaa viatu vya Hazard mbele ya wanaume kama Bale na Rodriguez, ni kukosa uzoefu wa kucheza kwenye La Liga. hili ni tatizo kwa sababu, Zizou anawaamini sana wazoefu. Lakini sifa zingine zote anazo kinda huyu.

3. VINICIUS JUNIOR

Msimu uliopita, aliuwa mmoja wa wachezaji wapya waliotikisa kwenye ulimwengu wa soka, hususan ligi kuu ya Hispania. changamoto pekee aliyokuwa nayo na ambayo anapaswa kufanyia kazi ni shabaha.

Vinicius alikuwa vizuri tu, isipokuwa mashuti yake, hayakulenga lango. Kwa kuwa Hazard hatokuwepo, Zizou hana budi, kurejesha imani yake kwa mchawi huyu wa kibrazil, huku pia akijaribu kumsaidia, katika ulengaji wa shabaha, akilifanyia kazi hilo, mbona mabaya yatakuja tu.

Alikuwa kwenye kikosi kilichoivaa Celta Vigo, jambo ambalo linazidi kumuongezea matumaini, kwa sababu Zizou mwenyewe, alinukuliwa akisema yuko tayari kumpatia nafasi nyingi msimu huu. Kuumia kwa Hazard ni fursa kubwa kwake kutesa.

2. GARETH BALE

Ilibidi kuwe na tatizo, ilie Zidane abadili mawazo yake kuhusu hatma ya Bale pale Santiago Bernabeu. Tatizo lenyewe likawa ni kuumia kwa Eden Hazard. haraka sana, baada ya kuangalia kulia na kushoto, aliamua kusalimu amri. Hakuwa na namna zaidi ya kumkumbatia hasimu wake huyu.

Zidane kishingo upande, alikubali kumwongezea nahodha huyu wa Wales, mkataba wa mwaka mmoja. huo ulikuwa uamuzi mzuri sana, kwani katika kikosi kizima, wachezaji wazoefu ni wachache sana, Bale akiwa ni mmoja wao.

Sio kwamba, Bale hana uwezo, hapana winga huyu bado analipa. Hofu kubwa aliyonayo Zizou, juu yake ni kawaida ya kupata majeraha. Zidane anachukizwa sana majeraha ya mara kwa mara ya staa huyu.

Pia, ukweli ambao hawezi kuupinga ni kwamba, anapokuwa vizuri kiafya, Bale ni bonge la mashine na mchezaji pekee, anayeweza kuvaa viatu vya Hazard kwa sasa, katika winga ya kushoto.

1. JAMES James Rodriguez

Mkolombia huyu, ni mmoja wa wachezaji ambao, hawakuwahi kumvutia Zidane. hajawahi kumpenda hata kidogo, lakini tangu msimu huu uanze, baada ya kurejea kutoka Bayern Munich, alikokuwa kwa mkopo, ni kama ameweza kuuteka moyo wa mfaransa huyo.

Haikuwa rahisi kwa James Rodriguez kumshawishi Zizou. Imani yake kwa nyota huyu, ilikuja baada ya kushindwa kulainisha moyo wa mashetani wekundu, kuhusu saini ya Paul Pogba. baada ya kukataliwa, hakuwa na jinsi, ilibidi ampigie James magoti.

Baada ya kuumia kwa Eden Hazard, Los Blancos walijikuta wakiwa hawana budi kumtumia Rodriguez sambamba na Bale. walianza kwenye mchezo wao wa kwanza wa La Liga, dhidi ya Celta Vigo.