Huyu ndiye kiboko ya Okwi

Monday February 18 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Licha Yanga kufungwa na Simba juzi, lakini mshambuliaji nyota wa timu hiyo Emmanuel Okwi alikiona cha moto kutoka kwa beki chipukizi Paul Godfrey ‘Boxer’.
Meddie Kagere alifunga bao pakee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Okwi alishindwa kufurukuta mbele ya beki huyo wa kulia aliyemdhibiti vyema nyota huyo wa kimataifa wa Uganda.
Wengi walizoea kumuona Okwi akipiga chenga za maudhi, mashuti na kufunga mabao huku akiwahadaa atakavyo mabeki wa timu pinzani, lakini juzi alikwaa kisiki mbele ya Godfrey.
Kinda huyo mwenye miaka 20, alicheza kwa kiwango bora na kwangu alikuwa nyota wa mchezo kutokana na uhodari wa kuhimili vishindo vya washambuliaji watatu Kagere, Okwi na John Bocco.
Okwi hakung’ara mbele ya mchezaji huyo ambaye amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Mwinyi Zahera.
Godfrey amempoka namba aliyekuwa beki hodari wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Juma Abdul ambaye kwasasa anasubiri kwa kinda huyo.
Zahera amewahi kukiri Godfrey ni beki hodari anayechipukia katika soka ya Tanzania kutokana na kasi na uhodari wake wa kuthibiti mashambulizi ya pembeni.
Nafasi ya beki wa pembeni anayocheza Godfrey aliyepandishwa kutoka kikosi cha vijana mwaka jana, ni moja ya nafasi ngumu katika soka kutokana na majukumu yake kimchezo.
Daima makocha huhitaji mtu alioyekomaa ambaye ana umakini wa kutosha na uzoefu ili aweze kuwa msaada mzuri katika kulinda, kuanzisha na kupandisha mashambulizi ya pembeni.
Kinda huyo, tangu alipoanza kuaminiwa na Zahera kwa kuanza kupata nafasi hasa baada ya kupata majeraha Abdul alionyesha uwezo mkubwa ambao ulimfanya aingie moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.
Jina la Godfrey limeteka hisia za wadau baada ya kuwazuia nyota hao, ukiangalia aina ya mashambulizi ambayo Simba ilikuwa ikitengeneza ilikuwa ikitumia mara nyingi upande wa kushoto ambako alikuwa akicheza Gadiel Michael.
Kwa kuthibitisha hilo, bao la Kagere alilofunga kwa kichwa lilitokea upande wa kushoto ambapo beki wa Simba, Zana Coulibaly alimpigia pasi nahodha Bocco ambaye alimpa pasi nyota huyo kwa kumpasia pasi ya juu.
Godfrey taratibu anaonekana kama ataendelea kuonyesha kiwango alichonacho anaweza kuingia anga za wakina Shomary Kapombe wa Simba ambaye kwa sasa ni majeruhi na Hassan Kessy wa Nkana ya Zambia ambao wamekuwa wakitegemewa Taifa Stars.
Kiwango cha Godfrey anachoendelea kukionyesha kumeifanya Yanga kutokuwa na mipango ya kuongeza mlinzi mwingine wa kulia ambaye walikuwa wakimlenga ili aleteushindani kwa Juma Abdul.
Awali hesabu za Yanga zilikuwa ni kuongeza beki wa kulia baada ya kuondoka kwa Hassan Kessy ambaye alitimkia zake Zambia.
Silaha kubwa ya kwanza ya Godfrey ni kujiamini na uhakika wa vitendo, nguvu na uwezo mzuri wa kupanda na kushuka kwa wakati.
Godfrey   anakumbukumbu ya kuonyeshwa kadi  nyekundu, Oktoba 30 mwaka jana   ambapo ilikuwa kwenye mchezo wa Ligi  dhidi ya Lipuli uliochezwa  Uwanja wa taifa na waliibuka na ushindi wa bao 1-0, baada ya kumchezea rafu Miraji Adam dakika ya 84 aliyekuwa anaambaa na mpira kuelekea maeneo ya Beno Kakolanya.
Ili Godfrey aweze kufika mbali zaidi kisoka anatakiwa kuendelea kufuata miiko na nidhamu sahihi za soka ndani ya uwanja na nje ya Uwanja. atakujakuwa msaada mkubwa kwa Taifa kwa siku chache za usoni.

Advertisement