Huyu ndiye Mo Dewji

Muktasari:

  • Mo alitekwa jana asubuhi akiwa anaelekea kwenye mazoezi katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Tukio la kutekwa kwa Mfanyabiasha maarufu nchini Mohammed Dewji 'MO Dewji' ambaye ni mshindi wa zabuni ya kuwekeza kwenye klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa 49%, ndio habari iliyotikisa vyombo vya habari nje na ndani ya nchi kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa za mashuhuda wa tukio hilo, Dewji alitekwa majira ya saa 11 Alfajili katika hoteli ya kifahari ya Colosseum ambayo alikwenda kwa lengo kufanya mazoezi ya viungo.

Wakati vyombo vya usalama vikiendelea na harakati za kuhakikisha Mfanyabiara huyo anapatikana sambamba na kuwanasa wahalifu, gazeti hili linakuletea dondoo muhimu kuhusiana na Dewji ambaye ni mmoja wa wanachama na mashabiki wa kutupwa wa klabu ya Simba.

Familia

Dewji mwenye umri wa miaka 43, alizaliwa Mei 8, 1975 katika Kata ya Ipembe iliyopo katika Jimbo la Singida Mjini ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu ya Mwaka 2000, ina jumla ya wakazi zaidi ya 2,853.

Amezaliwa akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya watoto sita ya Mzee Gulamabbas Dewji na Bi. Zubeda Dewji.

Mfanyabiashara huyo kijana ni mwenza wa Bi. Saira Dewji ambaye alianza naye uhusiano mwaka 2001 huku wakifanikiwa kupata watoto watatu kwenye familia yao.

Elimu

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Arusha kabla ya kuendelea na elimu ya Sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Dar es Salaam kabla ya baadaye mwaka 1992 kuhamishwa katika shule ya Arnold Palmer Golf Academy iliyopo Florida, Marekani kwa ajili ya kuandaliwa kwa elimu ya juu.

Baada ya kusoma hapo kwa miaka kadhaa, Mohammed Dewji, baba yake alimhamishia kwenye Shule ya Saddle Brooke alikohitimu elimu ya juu na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Georgetown kilichopo Washington, D.C ambako mwaka 1998 alihitimu Shahada ya Kwanza ya Kimataifa ya masuala ya Biashara, Fedha na Theolojia.

 

Biashara

Muda mfupi baada ya kuhitimu Shahada ya Chuo Kikuu, Dewji alianza rasmi kujishughulisha na biashara hasa katika usimamizi wa kampuni tanzu za Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL) akihudumu kama Ofisa Mkuu wa masuala ya fedha.

Kampuni ya METL imekuwa ikimiliki kampuni zinazojihusisha na masuala ya Kilimo, Masoko, simu za mkononi. Bima, udalali, usafirishaji, ugavi pamoja na uzalishaji wa vyakula na vinywaji.

Chini ya usimamizi wa Dewji, Kampuni tanzu za METL zimefanikiwa kuongeza kipato na faida kutoka kiasi cha Dola 30 milioni (zaidi ya Shilingi 68 bilioni) hadi kiasi cha Dola 1.5 bilioni (zaidi ya Sh 3.4 trilioni).

Kampuni Tanzu za METL zimekuwa zikihudumia takribani nchi 11, zikiwa zimeajiri wafanyakazi wapatao 28,000 na kwa makadirio ya haraka, huenda zikawa zimetoa ajira kwa watu 100,000 ifikapo mwaka 2021.

Nchini Tanzania, METL inayoongozwa na Mohammed Dewji inakadiriwa kuchangia 3.5% ya pato la Taifa kutokana na malipo ya kodi na tozo mbalimbali.

Utajiri alionao

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Mohammed Dewji anakadiriwa kuwa na utajiri unakaribia Dola 1.54 bilioni (zaidi ya Sh 3.5 trilioni) ambao unamfanya awe nafasi ya 17 katika orodha ya watu Matajiri Barani Afrika huku akishika nafasi ya kwanza nchini.

Siasa

Mbali na biashara, Dewji pia amekuwa akijihusisha na masuala ya kisiasa ambapo amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho bado ameendelea kuwa mwanachama wake.

Uwekezaji Simba

Mohammed Dewji ni miongoni mwa wadau na wanachama wenye mapenzi mazito na klabu ya Simba tangu enzi za utoto wake hadi sasa ambapo amekuwa akitoa msaada wa mara kwa mara wa fedha katika kuhakikisha inafanya vizuri.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, chini ya ushawishi wa Dewji, Kampuni zake za METL ziliingia mkataba wa kuidhamini timu hiyo ambao ulichangia klabu hiyo ipate mafanikio makubwa katika mashindano mbalimbali ya soka ndani na nje ya nchi.

Ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2002, ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu, ilitwaa Kombe la Tusker mara tatu huku pia ikifanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2003.

Baada ya hapo, Dewji aliachana nayo kutokana na kutofurahishwa na mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo na aligeukia kwenye klabu ya African Lyon ya jijini ambayo aliinunua kwa ajili ya kuimiliki lakini hakukaa nayo kwa muda mrefu na kuchukua uamuzi wa kuiuza.

Baada ya kukaa kwa kipindi kirefu bila kujishughulisha na masuala ya soka, Julai 2016 alitangaza nia ya kutaka kuwekeza kwenye klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa cha 50% alizotangaza atazinunua kwa kiasi cha Shilingi 20 bilioni.

“Shabaha yangu ni kuitoa klabu kwenye Bajeti ya Bilioni 1.2 hadi Bilioni 5.5. Mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka. Lazima tusajili vizuri na tuajiri makocha mzuri. Ukitenga Bilioni 4 kwa mwaka, tayari umewazidi wapinzani Azam na Yanga," alinukuliwa Mfanyabiashara huyo.

Suala hilo la Dewji liliibua vuguvugu ndani ya klabu hiyo ambalo lilikuja kupelekea kubadilishwa kwa katiba yake na kupatikana kwa mpya ambayo inabariki mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na kuifanya Simba iwe Kampuni huku mfanyabiashara huyo akishinda zabuni ya kuwa mwekezaji kwa 49% wa hisa za klabu hiyo.

Katika kipindi chote cha mchakato wa mabadiliko hayo, Dewji amekuwa akitoa fedha za kusaidia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Simba ikiwemo usajili, kambi, mishahara na posho jambo lililoisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2017/2018 ukiwa ni wa kwanza tangu ilipotwaa mara ya mwisho msimu wa 2011/2012.

Maisha binafsi

Dewji licha ya utajiri alionao, amejinasibisha kama mtu ambaye amekuwa karibu na jamii inayomzunguka akishirikiana nayo katika masuala mbalimbali ya shida na raha.

Mara kwa mara amekuwa akishiriki na kuchangia fedha katika kusaidia huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji safi na salama sambamba na kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji maalum.

Mwaka 2014 alianzisha Taasisi ya Mo Dewji Foundation kwa lengo la kusaidia kuwakwamua Watanzania kwenye umasikini, pia kusaidia kuboresha huduma mbalimbali muhimu za kijamii.

Pia, ni mwanachama wa Taasisi ya Giving Pledge inayojishughulisha na utoaji wa misaada kwa jamii zenye uhitaji duniani. Taasisi hiyo inaundwa na Mabilionea 150 kutoka nchi mbalimbali duniani na miongoni mwao ni Bill Gates, Warren Buffett, Mark Zuckerberg, Strive Masiyiwa na Patrice Motsepe.

Mtu wa mazoezi

Utajiri alionao haumfanyi Mohammed Dewji akose nafasi ya kuweka sawa mwili wake kwa mazoezi na badala yake amekuwa ni mtu anayehusudu programu mbalimbali za kumfanya awe fiti.

Amejijengea utaratibu wa kwenda kwenye vituo vya mazoezi mara kwa mara asubuhi na jioni na hata tukio la utekwaji wake limetokea akiwa anajiandaa kuingia kwenye progaramu ya mazoezi ya asubuhi katika Hoteli hiyo ya Colosseum iliyopo Osterbay jijini.

Tuzo

Mfanyabiashara huyo amefanikiwa kushinda tuzo mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia kuongeza na kukuza umaarufu wake.

Mwaka 2012 alitangazwa na Jukwaa la Uchumi duniani kama Kiongozi Bora Kijana na miaka miwili baadaye alitajwa na Jarida la Forbes kuwa miongoni mwa watu 10 wenye nguvu Afrika.

Mwaka 2014 alishinda tuzo mbili nyingine ambazo ni mtu mwenye Utu barani Afrika inayotolewa na Jarida la African Leadership na pia alitangazwa kama mmoja wa viongozi bora wa kiuchumi duniani.

2015 alishinda tuzo ya Utu kwa Afrika Mashariki, tuzo ya Kiongozi Bora wa Kibiashara ya Jarida la African Business na pia akatajwa na Jarida la Forbes kama Mwafrika Bora wa mwaka wakati mwaka 2016 alitajwa kuwa miongoni mwa Waafrika 100 watakaokuwa vinara wa kesho kiuchumi.