Huyu mshkaji humwambii kitu jinsi anavyomkubali Samatta

Muktasari:

  • Kiwango kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Taifa Stars na Klabu ya Genk ya nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta kimemfanya shabiki wa soka, Geofrey Megan 'Jeff' ambaye pia ni raia wa Tanzania asikauke uwanjani kila timu hiyo inapocheza ili tu amshuhudie mchezaji huyo anayetoka Mbagala jijini Dar es Salaam.

UNAJUA kama kuna shabiki namba moja wa Mbwana Samatta, Geoffrey Megan ‘Jeff’ mwenye uraia wa Tanzania ambaye amekuwa akienda kumshangilia kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu Ubelgiji?

Jeff ambaye ni mkazi wa Brussels anadai kuwa shabiki wa Samatta muda mrefu na alisema sababu iliyomfanya kumshangilia ni namna anavyoipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Shabiki huyo alisema anachokifanya pia kitakuwa kwa Mtanzania mwingine ambaye atafanikiwa kupasua anga kwa kufanya vizuri kwenye ligi yoyote kubwa Ulaya.

“Mara zote Samatta amekuwa akinifurahia pindi anionapo maana tumeshafahamiana, napenda kumshangilia kwa kutumia maneno ya Kiswahili, nimekuwa nikiwashangaza mashabiki wenzangu.

“ Wapo waliokuwa wakihisi ni ndugu yangu maana kuna siku nilikuwa karibu na sehemu ya kuchezea, baada ya mechi kumalizika Samatta alinifuata na tukapiga picha ya ukumbusho pamoja,” alisema Jeff.

Shabiki huyo alilitaja jina la Saimon Msuva kama nyota mwingine wa Kitanzania anayefuata kwa ukaribu nyayo za Samatta.

Jeff alisema hata kama Msuva atafanikiwa kujiunga na timu ya Ufaransa au Hispania hatasita kuwa anaenda mara kwa mara kumshangilia kama anavyofanya kwa Samatta.

Mbali na kuwa shabiki mkubwa wa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchi, Jeff pia ni mnazi mkubwa wa Manchester United ambayo wikiendi iliyopita imeifunga Newcastle United kwa mabao 3-2.