Huyu mpinzani wa Mwakinyo! kazi ipo J'pili

Muktasari:

Mwakinyo alipata umaarufu kwenye ndondi baada ya kumchapa Sam Egginton aliyekuwa bondia namba nane kwa ubora, pambano lililompandisha hadi ‘top 20’ ya dunia kwenye uzani wa super welter.

Dar es Salaam. Kazi ipo! kuelekea katika pambano la Hassan Mwakinyo na Joseph Sinkala litakalopigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, mjini Tanga.

Sinkala atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Mwakinyo aliyetoka kumchapa Sam Eggington wa Uingereza kwa Technical Knock Out (TKO) kabla ya hivi karibuni kumchapa kwa Knock Out (KO), Said Yazidu.

Sinkala yeye tangu Novemba 10 mwaka jana alipochapwa na Balazs Bacskai nchini Hungary, hajacheza pambano lolote hadi Jumapili atakapozichapa na Mwakinyo.

Bondia huyo aliyepata umaarufu baada ya kumchapa Eggington aliyekuwa bondia namba nane kwa ubora duniani anapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri ingawa, pambano hilo limetajwa kutompa rekodi yeyote Mwakinyo.

Bondia mkongwe nchini, Habibu Kinyogoli alisema, Mwakinyo kucheza mapambano ya kitaifa ni sahihi, lakini aangalie anapigana na bondia mwenye ubora kiasi gani.

"Asijifu kuwa ameshinda KO, lakini je ni bondia wa aina gani anapigana naye?," alihoji Kinyogoli na kufafanua kwamba ni wakati wa Mwakinyo kuimarisha jina lake kwenye masumbwi kwa kucheza mapambano ya viwango.