Huyu jamaa akitua tu Simba mtakoma

Muktasari:

Mwanaspoti lilipata taarifa, mabosi wa Simba wana mawasiliano ya karibu na kocha wao wa zamani, Patrick Phiri katika kuwapa taarifa za Mugalu ambaye alipitishwa na kocha huyo kwa kuwaeleza kama wataweza kumnasa.

KATIKA kuhakikisha safu ya ushambuliaji ya kikosi cha Simba inakuwa tishio, mabingwa hai watetezi wa Ligi Kuu wamepanga kumleta straika matata kutoka Congo ambaye anakipiga Zambia na walikuwa wakimsaka kabla ya dirisha la usajili wa ndani na ule wa Shirikisho la soka Afrika (CAF) kufungwa ili waweze kumtumia katika mashindano ya kimataifa.

Mpaka sasa kikosi cha Simba kina wachezaji tisa wa kigeni huku nafasi moja ikibaki wazi ili kutimiza idadi ya nyota 10 wa kigeni ambao wanatakiwa katika kikosi hicho kama msimu uliopita.

Mwanaspoti kama kawaida yake huwa halishindwi kukupa habari za ndani zenye uhakika, lilifahamu Simba ilitaka kuziba nafasi hiyo kwa kumshusha straika matata kutoka Power Dynamos ya Ligi Kuu ya Zambia, Chris Mugalu.

Usajili huo ulishindwa kukamilika kutokana na tarehe za usajili la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilikuwa ikiwatupa mkono huku Simba ikitaka kumtumia katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo inacheza na mwishoni mwa wiki ilicheza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya UD Songo.

Mwanaspoti lilipata taarifa, mabosi wa Simba wana mawasiliano ya karibu na kocha wao wa zamani, Patrick Phiri katika kuwapa taarifa za Mugalu ambaye alipitishwa na kocha huyo kwa kuwaeleza kama wataweza kumnasa.

Kigogo mmoja wa Simba aliliambia Mwanaspoti, “tuliongea na Mugalu na tulianza kumfuatilia huku tukiwasiliana na Phiri ambaye alikuwa kocha wetu lakini hata kiungo wetu, Clatous Chama ni miongoni mwa watu waliompitisha kuwa anaweza na anafaa kucheza katika timu yetu.

“Mambo mawili ambayo yalitufanya kushindwa kumsajili Mugalu katika kipindi cha usajili wa awali, kwanza alikuwa bado na mkataba na timu yake na hata tulipokuwa tukiongea na uongozi wake ulitaka pesa nyingi kwasababu Zesco United ya nchini humo nayo ilikuwa ikimfukuzia.

“Sababu ya pili kama tungetumia nguvu nyingi kukamilisha usajili wake tusingeweza kuwahi usajili wa CAF, kwa maana hiyo angeshindwa kucheza mashindano haya kutokana na kukosa leseni kama ilivyokuwa kwa Haruna Shamte jambo ambalo kama uongozi tusingekubali kuliona linatokea kwa upande wetu,” alisema kiongozi huyo (jina lake tunalo).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema waliogopa kusajili mchezaji mwingine kutokana kipindi walichokubalina kuongeza nyota mpya wa 10 wa kigeni wasingeweza kuwahi dirisha la usajili la CAF, ambalo muda wake ulikuwa umeikifia mwisho.

Magori alisema katika nafasi hiyo moja ya mchezaji wa kigeni walipanga kumleta straika wa maana mwenye uwezo wa kufunga zaidi ya waliokuwepo katika kikosi cha hivi sasa na walitaka kufanya hivyo ili kuongeza makali ya timu hasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kufikia mafanikio zaidi ya msimu uliopita.

“Siwezi kumtaja jina lake kutokana bado hatujakamilisha usajili wake huyo mshambuliaji lakini kama mambo yatakwenda vizuri kama ambavyo tumepanga na mwenyewe ataendeleza kasi yake ya kufunga tutamsajili katika dirisha dogo kama ambavyo viongozi tumekubaliana,” alisema Magori.

OFISA MTENDAJI BADO

Katika hatua nyingine Magori pamoja na viongozi wengine wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kumpata Ofisa Mtendaji mkuu mpya wa klabu huku kuna waliomba kutoka nchi mbalimbali Ulaya, Afrika ikiwemo na wa hapa Tanzania.

“Kuna majina matatu ambayo yatakwenda katika bodi na kati ya hao kuna mmoja, ambaye atapitishwa na kuwa katika nafasi ya Mtendaji Mkuu. Muda si mrefu nitatangaza kuondoka kama nilivyoeleza awali.

“Muda si mfupi tutatangaza kwani mchakato upo katika hatua za mwisho za kukamilisha na wote tayari wameshafanya mahojiano na kamati yetu na wanasubiri ni majibu ambayo siku si nyingi tutaweka wazi,” alisema Magori.

Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa katika majina hayo yumo Senzo Masingisa raia wa Afrika Kusini, ambaye ana nafasi kubwa ya kumrithi Magori.

Hivi karibuni Senzo amejiuluzu nafasi yake kama Mtendaji wa Plutnamz Stars ya Afrika Kusini aliyojiunga nayo mwaka 2013 akitokea Orlando Pirates.