Huyu hapa pilato wa kuzihukumu Simba, Yanga

Muktasari:

IKIWA zimebaki saa 24 kuchezwa mechi ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la Azam baina ya Simba na Yanga, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetangaza waamuzi sita watakaochezesha mechi hiyo.

IKIWA zimebaki saa 48 kuchezwa mechi ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la Azam baina ya Simba na Yanga, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetangaza waamuzi sita watakaochezesha mechi hiyo.
Simba na Yanga zitacheza keshokutwaJumapili, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumpata mshindi atakayetinga hatua ya fainali atakayecheza kati ya mshindi baina ya Sahare All Stars na Namungo ambao wanacheza kesho Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Simba wenyewe wamejihakikishia ushiriki wao kimataifa baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambapo wamekata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao huku bingwa wa kombe la shirikisho ataiwakilisha nchi michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, ushiriki ambao Yanga wanaupigania.
Waamuzi katika pambano hilo ni Abubakar Mturo (Mtwara), Abdallah Mwinyimkuu (Singida), Nadeem Aloyce (Dar), Ramadhan Kayoko (Dar), Frank Komba (Dar) na Kassim Mpanga (Dar) huku kamishna wa mchezo atakuwa ni Ally Katolila wa Dar.
Mara kadhaa, TFF imekuwa ikitumia mfumo huo wa waamuzi sita hasa katika mechi kubwa na zenye ushindani zaidi kama ilivyowahi kufanyika siku za nyuma katika mpambano wa timu hizo kongwe za jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, TFF haijaweka wazi ni mwamuzi yupi kati ya hao atakuwa mwamuzi wa kati lakini gazeti la Mwanaspoti lina taarifa kamili juu ya mwamuzi huyo, hivyo fuatilia zaidi gazeti lako pendwa kesho Jumamosi.