Huyu hapa Mandawa wa Botswana

Muktasari:

Mandawa ni miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na nyota huyo anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake wa Taifa Stars kujiandaa na mchezo wa kuwania nafasi ya Afcon, Oktoba 12 dhidi ya Cape Verde, ugenini.

INAWEZEKANA nyota wa Kitanzania, Rashid Mandawa (24) alikaribishwa kwa Kitswana ‘o amogelesegile’ na raia wa kawaida waliokuwa wakipishana naye pindi alipokuwa akiingia kwenye kota ya kambi ya Kijeshi ya BDF.

Mandawa aliishia kutabasamu na kupishana nao huku akishindwa kuwajibu chochote kutokana na kutoelewa nini wanamaanisha Wabotswana hao, anasema mshambuliaji huyo kwenye mazungumzo maalumu na gazeti hili.

Haya ni mahojiano maalumu na Mandawa namna ilivyotua Botswana, maisha yake yalivyo ya soka, mahusiano yake ya kimapenzi na mikasa mengine kibao ya kimaisha aliyokumbana nayo nchini humo.

Mandawa ni miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na nyota huyo anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake wa Taifa Stars kujiandaa na mchezo wa kuwania nafasi ya Afcon, Oktoba 12 dhidi ya Cape Verde, ugenini.

o’ amogelesegile ni maneno ya kilugha cha Watswana ambao wamekuwa wakipenda kuyatumia kumkaribisha mgeni pindi anapoingia kwenye himaya yao.

ALICHOSHWA NA SOKA LA BONGO

Mandawa ambaye alizaliwa Mei 5, 1994 akiwa na zaidi ya miaka mitano ya kucheza Ligi Kuu Bara, mshambuliaji huyo, anasema aliamua kuanza mchakato wa kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.

“Niliichezea Coastal Union ya Tanga msimu wa 2012/13, lakini msimu wa 2014/15 nikajiunga na Kagera Sugar ambayo ilinipatia umaarufu mkubwa nchini ila kama unavyojua maisha ya mpira ulifika muda wa kuondoka na nikajiunga na Mwadui.

“Mwadui nilikaa kwa kipindi kifupi nikasajiliwa na Mtibwa Sugar ambayo baada na yenyewe kuichezea tangu 2016 hadi 2017, nikiwa Mtibwa nilikuwa nikipata nafasi kibao za kufanya majaribio na kichokuwa kinanisaidia ni uhusiano wangu mzuri na benchi la ufundi,” anasema.

WABABE WA YANGA WALIMWONA GALASA

Mandawa anasema wababe wa Yanga, Township Rollers ambao iliwaondoa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1, walimpiga chini baada ya kufanya majaribio.

“Township Rollers ni klabu kubwa sana kwa huku na lengo langu la kuja Botswana lilikuwa ni kujiunga nao ila kibaya mipango sio matumizi ndio maana sikupata nafasi ya kujiunga nao,” anasema mshambuliaji huyo.

WAJEDA WALIVYOMCHUKUA

Baada ya kupigwa chini na Township Rollers , Mandawa anasema akapata nafasi ya kujiunga moja kwa moja na timu ya maafande wa Botswana, BDF XI F.C. bila ya hata kufanyiwa majaribio.

“Jamaa walikuwa wakinikubali na walikuwa wanaujua uwezo wangu wakaona hakuna sababu ya kufanya majaribio, walinichukua muda huo ambao nilikuwa na mawazo ya kurejea nyumbani na kunipeleka kambini kwao.

“Tulifanya mazunguzo ya mkataba pamoja na vipengele vingine ambavyo nilikubaliana navyo na kuingia mkataba nao,” anasema.

ALIVYOLIPA

KISASI KIBABE

Mandawa hakuwaacha salama Township Rollers pindi alipokutana nao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Botswana, Februari 26, 2018 aliwafunga mabao matatu ‘hat trick’ kwenye ushindi walioupata wa mabao 3-1.

“Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kufanya vile nchini humo, ujue kwenda sehemu na kutokukubalika huwa kuna sababu maalumu kwa hiyo kwangu sikuchukulia mabao yale kama nimelipiza kisasi,” anasema.

KIDOGO AWE

MFUNGAJI BORA

Mandawa ambaye msimu huu amefunga mabao mawili na kutengeneza matatu, anasema msimu uliopita alikuwa kwenye nafasi ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Botswana lakini akajikuta anapoteza nafasi hiyo mwishoni mwa msimu.

“Aliyekuwa anaongoza alinipita mabao machache ila kasi yangu yangu ya kufunga ilipungua mwishoni mwa msimu baada ya kutokuwa kwenye nafasi ya kuchukua ubingwa.

“Bingwa mara nyingi akishafahamika hata ule upambanaji wa timu unapungua ndio kilichotokea kwenye timu,” anasema.

Kiatu cha mfungaji bora wa BWPL kilienda kwa Thatayaone Kgamanyane aliyemaliza msimu huo wa 2017/18 akiwa na mabao 18, Mandawa aliyepachika mabao 11 kwenye msimu wake huo wa kwanza Botswana.

ANAVYOISHI

NA WAJEDA

“Jamaa wananikubali kwa sababu ya staili yangu ya uchezaji na siku zote nimekuwa nikiishi nao vizuri, najivunia kuwasoma ndio maana nimekuwa nikiishi nao bila matatizo ya aina yoyote,” anasema.

KUHUSU MAHUSIANO

Licha ya uwepo wa mademu wakali nchini Botswana kama ilivyo Afrika Kusini, Rwanda na mataifa mengine ambayo yanasifika kuwa na warembo, Mandawa anasema ametulizana na mke wake.

JAMAA ANAMISI MLENDA

Hakuna chakula ambacho Mandawa anakimisi kule Botswana kama ugali kwa mlenda, dagaa mchele na kachumbari ambavyo anadai havipikwi kwa kiwango alichoezoea hapa nyumbani.

“Wabotswana wana namna yao ya mapishi ambayo ni tofauti kidogo na nyumbani, utofauti nadhani utakuwa kwenye viungo, wao wanaweka vitu vingi ambavyo asilimia kubwa ni vigeni kwangu,” anasema Mandawa.

ANAKOTULIZA AKILI

Mandawa anasema mara kadhaa anapojihisi kutokuwa sawa amekuwa akienda kutalii kwenye mbuga ya wanyama ya BDF iliyopo ndani ya eneo la maafande hao.

“Akili kuna muda inachoka kwa hiyo huwa napendelea kwenda kwenye hifadhi hiyo ili kujichangamsha,” anasema.