Huyu Zahera hatari,Yanga yamwaga ofa

Muktasari:

Yanga kesho Jumapili watavaana na AFC Leopads katika mechi nyingine ya kirafiki kwa ajili ya kunoa makali kabla ya kuwafuata Township Rollers kwa mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa nchini Botswana wiki ijayo, huku akisaka ushindi.

ACHANA na matokeo ya mechi yao jana Ijumaa mjini Moshi, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera mipango yake sio ya kitoto kwani unaambiwa usiku wa jana fasta aliamua kuwakimbiza vijana wake, jijini Arusha huku mabosi wake wakimwaga ofa kwa mashabiki.

Tuanze na ishu ya Zahera. Kocha huyo jioni ya jana na vijana wake walikuwa wakivaana na Polisi Tanzania katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Ushirika, Moshi, lakini mara baada ya mchezo huo fasta alitaka kikosi hicho kusafiri hadi Arusha kuwawahi Wakenya.

Yanga kesho Jumapili watavaana na AFC Leopads katika mechi nyingine ya kirafiki kwa ajili ya kunoa makali kabla ya kuwafuata Township Rollers kwa mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa nchini Botswana wiki ijayo, huku akisaka ushindi.

Katika mchezo wa kwanza Yanga ililazimishwa sare ya 1-1, tena ikilazimika kuchomoa bao jioni kwa mkwaju wa penalti, hivyo akili za Zahera ni kutaka kuona wanaenda kupindua meza kwa wenyeji wao waliowang’oa kwenye michuano hiyo mwaka jana nchini humo.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Zahera amepitia upya video ya mchezo wao na Township na kubaini kuna mambo machache yaliyowaangusha ndio maana akataka mechi mbili kabla ya kuondoka nchini ili kuweka mambo sawa na kuwasapraizi wenyeji wao.

Inaelezwa, jana alipanga mara baada ya mchezo wao na Polisi Tanzania iliyorejea Ligi Kuu, angeenda Arusha usiku usiku kuisubiri AFC Leopards na baada ya mchezo huo atakaa na vijana wake kujadiliana mambo kadhaa kabla ya Jumatatu kurejea tena Moshi kukwea pipa kwenda Afrika Kusini ikiwa ndio mwanzo wa safari ya kuifuata Township.

Yanga imepanga kuweka kambi ya muda mfupi Sauzi ndipo iwafuate wapinzani wao kwao mjini Gaborone na mipango ya Zahera ni kuona vijana wake wanaivusha Yanga raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano, Rodger Gumbo alilithibitishia Mwanaspoti kuwa, Kocha Zahera amepania kuhakikisha Yanga inavuka kwenye mchezo wa marudiano na kwamba amepanga kukaa na wachezaji na kuzungumza nao mara baada ya mechi ya AFC. “Mara baada ya mchezo wetu na AFC Leopards, Kocha na viongozi watakuwa na kikao na wachezaji na mipango ya safari itapangwa tayari kuwafuata Rollers,” alisema Gumbo.

WAMWAGA OFA

Katika kuhakikisha wanaenda kupata sapoti ya kutosha ugenini, Yanga imepanga kumwaga ofa kwa mashabiki wa klabu yao ilui kufuata na timu kwenye mchezo wao wa Township.

Mabosi wa klabu hiyo wameamua kupunguza gharama ya usafiri kwa mashabiki ambapo kwenda na kurudi watatoa kiasi cha Sh 350,000 tu.

Gumbo alisema mashabiki watakaokuwa tayari kuungana nao kwenye mapambano ya kuwang’oa Township watatoa Dola 500 tu, kwa wale wataosafiri kwa ndege hadi Afrika Kusini na kutafutiwa usafiri wa basi kwenda Botswana.

Alifafanua kuwa yapo mabasi matatu ya kuwapeleka kwenda kushuhudia majembe yao yakifanya kazi ya kuonyesha uwezo wa kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.