Huyu Samatta si wa nchi hii nakwambia

Muktasari:

  • Katika mahojiano yake, Sonck ambaye anaamini msimu huu Genk inaweza kutwaa ubingwa wa Jupiler Pro, alisema hatoshangazwa na Samatta kama pia atashinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka.

GWIJI wa zamani wa KRC Genk, Wesley Sonck amemvulia kofia nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwa kusema anaweza kutwaa Kiatu cha Dhahabu msimu huu wa 2018/19 kutokana na kasi aliyonayo kwenye upachikaji mabao.

Sonck ambaye alistaafu soka Aprili 2014 enzi zake alifanya makubwa KRC Genk ambako hadi sasa anashikilia nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote akiwa na mabao 80 kwenye klabu hiyo nyuma ya Jelle Vossen (105).

Mkali huyo, alisema kwa sasa Genk wapo kwenye kiwango bora kinachochangiwa kwa kiasi kikikubwa na ubora wa Samatta ambaye anaongoza orodha ya wafungaji Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ akiwa na mabao 22.

“Samatta ni mshindi na amelionyesha hilo msimu huu, muda mrefu nimekuwa nikimfuatilia na nilijisemea kuwa ipo siku anaweza kuwa mchezaji muhimu. Alichokuwa anakipigania ni kufika kwa wakati wake ambao ni sasa.

“Huu ni msimu wake hakuna cha kushangaza, anafunga katika mazingira tofauti. Natambua vile ambavyo kujiamini kwa mshambuliaji huwa kunaongezeka kadri anavyofunga,” alisema Sonck.

Katika mahojiano yake, Sonck ambaye anaamini msimu huu Genk inaweza kutwaa ubingwa wa Jupiler Pro, alisema hatoshangazwa na Samatta kama pia atashinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka.

“Sasa kama ataiwezesha pia Genk kushinda ubingwa wa Ligi inawezekanaje mtu wa namna hiyo kutokuwa mchezaji bora? Binafsi naamini atakuwa na sifa za kuwa mchezaji bora,” alisema.

Msimu wa 2001/02, Sonck akiwa na KRC Genk aliibuka kuwa Mfungaji Bora wa Jupiler Pro ambapo alipewa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu pia alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka.

Baada ya kufanya vizuri kwa Sonck ndani ya msimu huo, Genk ilimuuza kwa Ajax ya Uholanzi ambayo aliichezea kwa miaka miwili, kisha akatimkia zake Ujerumani ambako aliichezea Borussia Monchengladbach kabla ya kurejea kwao Ubelgiji.