Huyu Messi sio mtu wa kawaida aisee

Muktasari:

Kwenye mchezo huo, Messi alifunga hat-trick katika kipindi cha kwanza na kumfanya awe amefikisha hat-trick 36 kwenye La Liga, mbili zaidi ya alizofunga mpinzani wake, Cristiano Ronaldo. Alifunga bao lake la nne kwenye kipindi cha pili na kuipa ushindi mtamu Barca

BARCELONA, HISPANIA . SUPASTAA, Lionel Messi amekuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya mchezo wa soka kuhusika kwenye mabao 100 baada ya kutupia nyavuni mara nne, chama lake la Barcelona liliposhusha kipigo cha mabao 5-0 kwa Eibar kwenye La Liga wikiendi iliyopita.

Messi alikuwa kwenye ukame mkubwa wa kufunga mabao, lakini aliumaliza kwa staili ya kipekee baada ya kufunga mara nne kwenye mechi moja, huku bao jingine akimpiga tobo beki na kisha kuubetua mpira kumpita kipa wa upinzani.

Kwenye mchezo huo, Messi alifunga hat-trick katika kipindi cha kwanza na kumfanya awe amefikisha hat-trick 36 kwenye La Liga, mbili zaidi ya alizofunga mpinzani wake, Cristiano Ronaldo. Alifunga bao lake la nne kwenye kipindi cha pili na kuipa ushindi mtamu Barca.

Licha ya kwamba Messi alikuwa hafungi, lakini rekodi zake kwenye kuchangia mabao hazikuwa mbaya na alihusika kwenye asisti nane katika mechi tisa za mwisho kwenye La Liga kabla ya kipute hicho cha Eibar.

Jambo hilo limemfanya Messi kuwa mchezaji wa kwanza kuhusika kwenye mabao 1,000, iwe kwa kufunga au kuasisti moja kwa moja. Staa huyo anayevaa jezi namba 10, amefunga mabao 696 na kuasisti 306 katika nyakati zake zote alizochezea Barcelona na timu yake ya taifa ya Argentika katika kipindi cha miaka 16 aliyodumu kwenye mchezo huo wa soka.

Staa Messi ameshinda Ballon d’Or mara sita na sasa ameirudisha Barcelona kwenye kilele cha La Liga baada ya Real Madrid kuchapwa kwenye mchezo wao uliopita. Kitu pekee ambacho Messi anabakiza kufanya ni kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia au Copa America akiwa na timu yake ya taifa.