Huyu MO Ibrahim mbona mtampenda

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana alisema MO amejiunga na timu juzi na ameanza mazoezi jana pamoja na wanzake.

KAMA ni mkwara basi huu alioutoa Kocha wa Namungo, Hitimana Thiery juu ya kiungo wake fundi wa mpira, Mohammed ‘MO’ Ibrahim, aliyetua klabuni akitokea Simba ni balaa, kwani amedai moto anaokuja nao jamaa si mchezo na waliombeza watamshangilia.

Wakati Mo Ibrahim akijiandaa kuwasha moto, ishu ya Adam Salamba ikipigwa danadana, lakini kiungo huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar aliyepotea kabisa aliposajiliwa Simba misimu mitatu iliyopita.

Kocha Hitimana amesema kiungo huyo amejiandaa kuthibitisha amezaliwa upya Namungo.

MO amejiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Simba, na ameanza kujifua na timu hiyo huku leo atakuwa ni miongoni mwa nyota wanaotarajia kuivaa Ndanda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana alisema MO amejiunga na timu juzi na ameanza mazoezi jana pamoja na wanzake.

Lakini akitolea ufafanuzi suala la Salamba kuwa atajiunga wakati wowote kwasababu ni mchezaji wao.

“Salamba ni mchezaji wetu kwa mkataba wa mwaka mmoja na tayari makubaliano ya pande mbili yameshafikiwa na ishu iliyopo sasa ni mchezaji huyo atajiunga lini na timu,” alisema.

“Hili siwezi kulizungumzia, zaidi nauachia uongozi kwani ndio ulionihakikishia kuwa ni mchezaji wetu lakini simuoni kambini.

“Awali iliripotiwa atajiunga na timu mara baada ya kutoka Sauzi ambako alienda kufanya majaribio, lakini tangu amerejea kutoka huko hajafanya hivyo, kikubwa kinachotakiwa kufahamika ni kwamba ni mchezaji wetu wakati wowote atajiunga na sisi.”

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Ndanda alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatumia uwanja wao wa nyumbani kupata pointi tatu na kuongeza kuwa wanategemea mchezo wa ushindani kutoka kwa wapinzani wao.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu, lakini kitu kikubwa tunachojivunia ni kwamba tupo nyumbani na maandalizi yetu ya msimu yalikuwa mazuri, wachezaji wetu kwa asilimia kubwa wako vizuri,” alisema kocha huyo anayeifundisha timu hiyo msimu huu.