Huyu Kagere ni balaa

MASHABIKI wa Simba kwa sasa wanaliimba jina la Chris Mugalu kutokana na mshambuliaji huyo mpya kutua Msimbazi na moto wake akifunga kila anapoingia uwanjani, lakini jamaa ni lazima ajipange kwelikweli kwani kinara wa mabao wa klabu hiyo kwa sasa, Meddie Kagere ni balaa zito.

Kama hujui ni mguu wa kulia ni silaha hatari ya Kagere pindi awapo uwanjani.

Rekodi zinaonyesha hadi sasa wakati Ligi Kuu ikiwa raundi ya tano, Kagere ameshafunga mabao manne, akiwa nafasi ya pili kwenye orodha ya ufungaji nyuma, Prince Dube wa Azam FC, lakini mabao hayo yamemfanya afikishe jumla ya mabao 49 katika misimu yake mitatu Msimbazi.

Tathmini ya mabao 49 yaliyofungwa na Kagere katika Ligi Kuu tangu alipojiunga na Simba 2018, inaonyesha amekuwa akipachika idadi kubwa ya mabao kwa mguu wake wa kulia.

Kagere ameshafunga jumla ya mabao 27 kwa mguu wa kulia, mabao 14 kwa kichwa na mabao nane kwa mguu wa kushoto.

Msimu uliopita, mguu wa kulia ndio ulikuwa hatari zaidi kwani alifunga mabao 15, manne akifunga kwa kichwa na matatu kwa mguu wa kushoto wakati katika msimu wake wa kwanza, alifunga mabao 11 kwa mguu wa kulia, mabao manne ya mguu wa kushoto huku mabao ya kichwa yakiwa nane.

Msimu huu amefunga mawili kwa kichwa huku mojamoja akifunga kwa mguu wake wa kushoto na kulia.

Ukiondoa hilo, Kagere pia amedhihirisha hatari zaidi katika kufumania nyavu katika dakika za mapema zaidi za mchezo, ingawa amekuwa akifunga katika muda mwingine.

Takwimu zinaonyesha, amekuwa tishio katika dakika 15 za mwanzo za mchezo ambapo ndani ya muda huo amefunga jumla ya mabao 12, japo amekuwa akifunga katika dakika za mwanzoni mwa kipindi cha pili ambazo kwa mujibu wa takwimu, mshambuliaji huyo amefunga mabao 11 katika dakika 15 za mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kiujumla Kagere ni tishio zaidi kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo kwani kati ya mabao hayo 25 amefunga kipindi cha kwanza na 24 dakika 45 za pili.

Kiujumla Kagere kazifunga jumla ya timu 18 ikiwamo Singida United, Biashara United, Yanga, Mbeya City, Prisons, Ruvu Shooting, Gwambina, JKT Tanzania, Lipuli, Mwadui, Azam na Coastal Union, Alliance, Mbao, Ndanda, Namungo, Kagera Sugar na Mtibwa.

WAKONGWE WAMCHAMBUA

Nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika Simba, Majimaji Songea na Taifa Stars, Abdallah Kibadeni ‘King’ alichambua kinachombeba Kagere ni malengo.

“Wachezaji wa kigeni wanapokuja nchini kwanza wanataka sifa na wanakuwa na malengo, hicho ndicho anachokifanya Kagere japo kufunga ni kazi yake kwenye timu,” alisema Kibadeni.

Naye, Abeid Mziba aliyekuwa kinara wa kupachika mabao ya kichwa enzi zake, alisema Kagere anamkumbusha enzi wao wakicheza.

“Tulicheza kwa malengo, wakati ule mchezaji ulijipanga kufanya kitu cha kuvutia uwanjani ili mradi tu ujulikane, Kagere anafanya hivyo kwenye soka la sasa, anafanya kitu ili watu wamjue, asisahaulike.”