Huyo Kante kazigomea Inter Milan na Real Madrid Ulaya

KIUNGO wa Chelsea na timu ya Taifa ya Ufaransa, N’Golo Kante, 29, amesisitiza kwamba hana mpango wa kuondoka klabuni hapo katika dirisha lijalo licha ya kuwepo kwa taarifa zinazo mhusisha kujiunga na Real Madrid au Inter Milan.

Kante ambaye amekuwa na kiwango bora kwa zaidi ya misimu minne tangu akiichezea Leicester City amekuwa kwenye rada za Inter Milan na Real Madrid ambapo Real inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuinasa saini yake kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya Kante na kocha wa Real, Zinedine Zidane.

Mkataba wa mchezaji huyo unatarajiwa kumalizika mwaka 2023 na thamani yake katika soko la usajili ni Euro 70 milioni.

Kwa upande wake Inter Milan nayo inataka kumsajili kwa sababu ni moja ya wachezaji ambao kocha Antonio Konte anawahitaji ili kujenga timu, lakini pia ni mchezaji anayemfahamu vizuri kwa kuwa aliwahi kumfundisha wakati anaifundisha Chelsea kabla ya kutimuliwa.