Huyo Ajibu anaisoma namba kimyakimya mjue!

Sunday August 12 2018

 

MSHAMBULIAJI wa Yanga Ibrahim Ajibu bado anaisoma namba aisee, kocha wa timu hiyo wamemuandalia dozi nzito unaambiwa mpaka juzi bado alikuwa akifanya mazoezi makali ya kukimbia peke yake.

Kama unavyojua Ajib alichelewa kujiunga na timu hiyo na sababu ilikuwa ni kuumwa sasa alipofika katikati ya wiki hii alikimbizwa balaa huku akipewa kocha maalum wa kumsimamia Noel Mwandila.

Baada ya mazoezi hayo ya siku ya kwanza kwake shughuli ikaonekana kama kumalizika akarudishwa kucheza na wenzake lakini juzi jioni kibao kikabadilika tena.

Kocha Mkuu Mwinyi Zahera juzi hiyo akamrudisha tena katika mbio hizo ambapo jamaa alikimbizwa kuanzia mazoezi yanaanza mpaka yanamalizika.

Ajibu alionekana akikimbia nje ya uwanja tena huku Mwandila akimfuatilia kwa karibu ambapo hakujumuika na wenzake waliokuwa wakipewa mazoezi ya ufundi uwanjani.

Kocha Zahera aliliambia Mwanaspoti kuwa mchezaji pekee atakayekosa programu yake ni yule aliyeamua kuondoka moja kwa moja katika timu hiyo ambapo mshambuliaji huyo atapata dozi sawa kama waliyopata wenzake.

“Ajibu bado anaendelea na programu yake nataka kila mchezaji awe fiti, ukiwa unaumwa tutakupa pole tutakuombea upone haraka ukishakuwa sawa utafanya mazoezi kama waliyofanya wenzako,” alisisitiza Zahera.

“Ajibu ni mchezaji mzuri lakini ili awe mzuri zaidi anatakiwa awe fiti zaidi sitaki wachezaji wanacheza kidogo halafu wanachoka.”

Advertisement