Huu ndio wasifu wa Yono Kevela

Muktasari:

  • Kevela anachuana katika nafasi hiyo na Fredrick Mwakalebela, Titus Eliakim Osoro, Salum Chota na Mbunge wa Ileje, Janeth Mbena.

KATIKA muendelezo wa wasifu wa wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi wa Uchaguzi Mkuu wa Yanga, leo tunamuangalia Yono Stanley Kevekla anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

Kigogo huyo aliyewahi kuwa Mbunge wa Njombe Magharibi, alipitishwa kuwania nafasi hiyo kupitia mchakato wa awali kabla ya Uchaguzi wa kuziba nafasi za uongozi Jangwani kusitishwa Januari mwaka huu.

Kevela anachuana katika nafasi hiyo na Fredrick Mwakalebela, Titus Eliakim Osoro, Salum Chota na Mbunge wa Ileje, Janeth Mbena.

WASIFU WAKE

Mgombea huyo ana umri wa miaka 55 akiwa na uzoefu katika masuala ya uongozi kwani mbali na kuwa Mbunge wa Njombe Magharibi kati ya mwaka 2005-2010, pia amewahi kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwamo Kampuni ya Sigara kama Mhasibu Msaidizi, Afisa Mikopo wa Benki ya CRBD.

Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Yono Auction Mart pia ni mdau wa michezo akiwa ni Mwenyekiti wa Chama Soka Mkoa wa Njombe (Njorefa) na katika uchaguzi mkuu wa TFF uliopita aliwania Ujumbe kupitia Kanda ya Njombe na Rukwa na kuangushwa.

ELIMU YAKE

Kevela anashahada ya pili ya Biashara (MBA), kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa sasa anasomea udaktari wa Biashara na Utawala (PHD) katika Chuo Kikuu Huria, amehudhuria kozi mbalimbali za masuala ya biashara katika China, Korea Kusini, Italia, India, Hispania na Afrika Kusini.

Elimu yake ya Sekondari kwa Kidato cha Nne ameipata Malangali Iringa, huku ile ya Kidato cha Sita akiipata katika Shule ya Tosamaganga pia ya mkoani Iringa, kabla ya kujiendeleza katika masuala ya biashara na kuanza kupata ajira sehemu mbalimbali.