Huu ndio mkwanja wa Inter kumbeba Messi

Muktasari:

Lionel Messi amecheza mechi 761 katika vikosi vyote vya Barcelona tangu mwaka 2003, akitupia jumla ya mabao 644.

MILAN, ITALIA. MZAHA mzaha, mara paap – Lionel Messi ndani ya uzi wa Inter Milan.

Lisemwalo ni kwamba, miamba hiyo ya Italia ipo tayari kutoa mkwanja wa Pauni 235 milioni kunasa huduma ya supastaa Messi ili akakipige kwenye Serie A.

Siku za karibuni, Messi amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya San Siro - kwenda kuifanya Serie A kuwa na mvuto mkubwa baada ya mpinzani wake wa miaka yote, Cristiano Ronaldo kukipiga huko Juventus.

Kwa miaka kibao, Ronaldo na Messi walikuwa wakichuana jino kwa jino huko kwenye La Liga kabla ya mmoja, staa wa Kireno kutimkia zake Juventus – alikotumika kwa msimu wa pili sasa.

Staa Messi, bado hajakubaliana na Barcelona kuhusu mkataba mpya, wakati huu uliopo kwa sasa utafika tamati mwishoni mwa msimu ujao na hapo atakuwa huru kwenda kujiunga na timu yoyote anayohitaji.

Messi akiondoka Barcelona hakuna ubishi jambo hilo litaibua mshtuko mkubwa kwa mashabiki wa soka duniani.

Karibu msimu wote huu, Messi amekuwa akiripotiwa kutofurahia maisha yake ya Nou Camp kutokana na timu hiyo kufanya vibaya na kushindwa kubeba mataji, likiwamo taji la La Liga lililonyakuliwa na wapinzani wao Real Madrid msimu huu.

Barca imemaliza ligi katika nafasi ya pili - pointi tano nyuma ya vinara Real Madrid, wakati kabla ya mlipuko wa janga la virusi vya corona, Messi na wenzake timu yao ilikuwa kileleni kwenye La Liga kwa tofauti ya pointi mbili.

Ripoti za kutoka Catalan zinadai kwamba kocha Quique Setien atafutwa kazi kama atashindwa kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Messi amekuwa akilalamikia kiwango cha timu na kutoa tahadhali kwamba kama hawatabadilika basi hawatawashinda Napoli kwenye mchezo wao wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mechi ya kwanza timu hizo zilipokutana Italia, ilimalizika kwa sare ya 1-1.

Kwa mujibu wa La Gazzetta Dello Sport, Inter Milan ipo tayari kumlipa Messi Pauni 60 milioni ili kwenda kujiunga kwenye kikosi chao, ambapo wamemwaandalia mkataba wa miaka minne.

Likitokea hilo, basi vita ya Messi na Ronaldo itahamia kwenye Serie A. Sambamba na hilo, Messi pia atakwenda kumpiku Ronaldo kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye Serie A.

Ronaldo anavuna zaidi ya Pauni 27.3 milioni kwa mwaka kupitia mishahara yake huko Juventus, kabla ya janga la corona ambapo baadaye ilielezwa kwamba kuna jambo la kupunguza mishahara ya wachezaji.

Siku chache zilizopita, wamiliki wa Inter Milan walizua mshtuko mkubwa baada ya kuitumia picha ya Messi kwenye tangazo la mchezo wa Serie A huko China. Jambo hilo liliwafanya watu kuanza kujadili kwamba huenda staa huyo akasajiliwa ndani ya dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Siku kadhaa zilizopita, Messi aliripotiwa kuwaambia mabosi wa Barcelona kwamba ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Nou Camp kama tu Xavi atarudishwa kuja kuwa kocha.

Sambamba na hilo, kitendo cha Messi kuchelewesha kukubaliana juu ya mpango wa kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kubaki Barcelona unazua utata zaidi, kwamba huenda akaamua kuachana na timu hiyo mkataba wake utakapomalizika mwakani.

Lakini, kwa upande wa Barcelona katika kuzuia uwezekano wa kumpoteza bure supastaa wao huyo endapo kama atagoma kusaini mkataba mpya, basi wanafikiria kumpiga bei kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi na kujiandaa kwa hilo mapema, Inter imeshatenga mkwanja wa Pauni 235 milioni kumaliza mambo.