Hutaki! Hii ndio Simba buana

Muktasari:

  • Mwanaspoti lilishuhudia Simba ikitetea ubingwa wao ugenini mchezo uliokuwa na ushindani kabla na wakati wa mechi yenyewe.

 SINGIDA. SIMBA wametetea ubingwa wao wakiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Biashara United watakaokaribishwa Uwanja wa Uhuru keshokutwa Jumamosi pamoja na Mtibwa Sugar itakayochezwa wiki ijayo Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Simba ilitetea taji hilo baada ya kuifunga Singida United bao 2-0 kwenye Uwanja wa Namfua, mjini Singida.

Mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na washambuliaji wake, Meddie Kagere dakika ya 10 pamoja na nahodha John Bocco. Kagere alifikisha mabao 23 wakati Bocco ana mabao 16.

Mwanaspoti lilishuhudia Simba ikitetea ubingwa wao ugenini mchezo uliokuwa na ushindani kabla na wakati wa mechi yenyewe.

MASHABIKI SIMBA WALIFUNIKA

Ni wazi mechi yoyote inyaochezwa katikati ya wiki kwa maana siku za kazi, haziwi na mashabiki wengi uwanjani lakini mechi ya Simba na Singida United ilikuwa ni tofauti.

Licha ya uwepo wa taarifa za awali mchezo huo kutajwa kuchezwa saa 8 mchana, bado pia isingekuwa tatizo kwa mashabiki wa Simba ambao walifurika uwanjani hapo kabla ya saa 8 wakisubiria kuiona timu yao ikicheza uwanjani hapo.

Ndani ya uwanja rangi iliyokuwa imefunika ni nyekundu na kwa uchache nyeupe ambazo zote ni rangi za jezi za Simba msimu huu huku jezi za wenyeji Singida United hazikuonekana sana jambo lililoonyesha timu hiyo imepoteza mvuto kwa mashabiki wao.

NJANO YAHARIBU MAMBO

Kabla ya mchezo kuanza, eneo la jukwaa kuu kulikuwa na waangalizi (Stewards) waliokuwa wamevalia nguo zenye rangi ya njano ambao walikuwa na jukumu la kuhakikisha hakuna kasoro yoyote itakayojitokeza eneo hilo lakini haikuwa hivyo badala yake mashabiki wa Simba walianza kuwazonga wakianza na mtazamaji aliyekuwa na mwenzake walipokaa upande waliokaa mashabiki wa Simba na kusababisha kelele.

Mashabiki wa Simba waliwaunganisha wote na kulazimisha watoke eneo hilo na baada ya kuzozana kwa muda mrefu ilibidi Kamishna wa mchezo huo, George Komba kutoka Dodoma kuwaondoa eneo hilo ndipo mambo yakatulia.

UWANJA BADO TATIZO

Mashabiki waliujaza Uwanja wa Namfua kwa sababu tofauti ikiwemo uwanja kutokuwa na majukwaa ya kutosha na hivyo kulazimisha mashabiki wavuke kwenye krosi za mwisho ambazo walizikata na kusogelea senyeng’e za karibu na uwanja jambo ambalo ni tatizo endapo mambo yatakwenda tofauti.

Mbali na hilo, hata eneo la kuchezea pia nalo sio zuri na kama ilivyokuwa kwa Yanga walilalamikia walipocheza na Singida uwanjani hapo, ndivyo ilivyokuwa kwa Simba walicheza kwa tahadhari kubwa ili wasipate majeraha kutokana na uwanja kutokuwa mzuri sana eneo la kuchezea.

SINGIDA ILIKUWA LAZIMA WAPIGWE

Hili la Singida United kufungwa na Simba ndilo lililokuwa linatarajiwa na wengi kabla ya mchezo wenyewe kutokana na jinsi ambavyo timu hiyo imekosa makali msimu huu tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ilipojaza wachezaji wengi nyota chini ya Kocha Hans Pluijm.

Singida iliyo chini ya Kocha Fred Minziro haikutengeneza nafasi nyingi za mabao ukiachilia mbali nafasi chache ambazo walizipata hata hivyo hazikuleta hofu yoyote kwa Simba zaidi ya nafasi hizo kupotezwa na wachezaji wao.

Wachezaji Geoffrey Mwashiuya, Issa Makamba, Boniface Maganga na Habib Kiyombo hawakuwa na madhara yoyote kwa Simba jambo lililowapa nafasi kubwa Simba kutawala mchezo ambao hata hivyo uliathiriwa na ubovu wa eneo la kuchezea.

KAGERE GUMZO

Mshambuliaji Meddie Kagere ndiye alikuwa gumzo zaidi kwenye mchezo huu na kabla hata ya mchezo, mashabiki wa Simba walikuwa wakimsubiria kwa wingi wakimtaja pamoja na kuonyesha ishara ya kuziba jicho lake moja.

Bahati nzuri kwao ilikuja baada ya mchezo kuanza ambapo kama walivyokuwa wakitarajia ndani ya dakika 10 tu Kagere aliwanyanyua mashabiki hao akifunga bao la kuongoza kwa Simba na likiwa la 23 kwake msimu huu akiongoza kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu.

Kagere kwa bao hilo alilofunga ameendelea kuweka hai uwezekano wa kuvunja rekodi ya mabao iliyodumu kwa miaka 20 sasa ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ akiwa na Yanga mwenye mabao 26 ya ligi kuu ambapo ili kuvunja rekodi hiyo Kagere anatakiwa afunge mabao matatu kuifikia au manne ili kuweka rekodi yake binafsi.

BAO LA BOCCO

Kipa wa Singida United, Said Lubawa alifanya kazi yake vema ya kuokoa mpira usiwe kona uwe wa kurushwa badala yake ilisababisha bao hili la John Bocco aliyefunga kwa krosi ya Emmanuel Okwi ambaye aliurusha haraka mpira huo kwa Mzamiri Yassin aliyemrudishia Okwi naye akiupiga kwa Bocco wakati ambao walijua kabisa kipa wa Singida yupo chini nje ya uwanja akiugulia maumivu ya mguu.

Baada ya bao hilo kuingia mashabiki waliokuwepo uwanjani wakiwemo wa Simba hawakushangilia huku baadhi yao wakishangilia wakati huo wakiendelea kujiuliza nini kitatokea huku wengine wakidai ilipaswa mchezo usiendelee.

Mashabiki wengine walidai kuwa mwamuzi Shomary Lawi alikuwa sahihi kuruhusu mchezo uendelee kutokana na kipa kuwa nje ya uwanja na alitakiwa aingie ndani ya uwanja ndipo mwamuzi asimamishe mchezo lakini alichelewa kwani wachezaji wa Simba walitumia kosa hilo kupasiana haraka na kufunga.

SHANGWE KAMA LOTE TU

Filimbi ya kumalizika mchezo iliyopulizwa na Lawi iliamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Simba na zaidi viongozi, wachezaji na benchi la ufundi ambao walionyesha furaha yao huku wakishangilia kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo ikiwemo kocha Patrick Aussems kumwagiwa maji.