UCHAMBUZI : Huruma za Mungu ndizo zitaziokoa Mbeya City

Friday October 23 2020
mbeya city pic

MBEYA City iko taabani katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu katika msimamo wa raundi saba zilizochezwa hadi sasa.

Inashika mkia ikiwa imekusanya pointi mbili tu katika mechi saba ilizocheza ambazo zimetokana na sare mbili ilizopata dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji FC na mechi nyingine tano imepoteza dhidi ya Yanga, KMC, Namungo, Azam na Mwadui FC.

Bahati mbaya zaidi kwao, katika mechi saba walizocheza, wamefunga bao moja tu huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa ikiwa inashika nafasi ya pili kwa kufungwa idadi kubwa ya mabao nyuma ya JKT Tanzania ambayo imefungwa mabao 10.

Matokeo hayo yasiyoridhisha yameanza kuuweka katika presha uongozi wa timu hiyo na katika kuthibitisha hilo, Jumanne mwanzoni mwa wiki hii waliamua kumtimua kocha wao Amri Said wakiamini anawajibika kwa kufanya kwao vibaya katika mechi hizo.

Kutimuliwa kwa Amri Said ‘Stam’ ni jambo ambalo wengi walilitegemea kutokana na muendelezo wa kufanya vibaya kwa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Jiji la Mbeya tangu ilivyopanda Ligi Kuu msimu wa 2013/2014.

Ni jambo lililozoeleka katika mpira wa miguu kwa makocha kuwajibika pale timu inapofanya vibaya na hilo limeshika kasi hapa nchini na uthibitisho ni klabu nyingine mbili ambazo zimeshaamua kuachana na makocha wao kutokana na kutofanya vyema katika mechi za mwanzoni msimu huu ambazo ni Ihefu ya Mbeya na Mtibwa Sugar.

Advertisement

Hata hivyo kwa uhalisia, uamuzi uliofanywa na uongozi wa Mbeya City kumtimua Amri Said unaweza usiwe na tija na usiiokoe timu hiyo kwa sababu kufanya kwake vibaya kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na sababu nyingi tofauti zaidi hata ya mbinu za kocha huyo.

Kuna mambo mengi ambayo yanaiangusha Mbeya City mbali na Stam na miongoni mwa hayo ni kuwa na kundi kubwa la wachezaji wasio na ubora na wasio na hadhi ya kucheza mechi za ushindani za Ligi Kuu.

Kundi kubwa la wachezaji wao ni vijana wasio na uzoefu na Ligi Kuu lakini pia hawana nyota wanaoweza kuamua matokeo katika mechi ngumu na kuhimili ushindani wa ligi.

Wachezaji hawa ni matunda ya bajeti kiduchu ambayo Mbeya City iliitumia katika kufanya usajili wao kwa ajili ya msimu huu hali iliyopelekea wawakose wachezaji wazuri, bora na wenye uzoefu wa ligi ambao wangekuwa chachu kwa timu hiyo kufanya vyema katika mechi zake.

Unapokuwa na timu yenye kundi kubwa la wachezaji wa namna hiyo, ni vigumu kuweza kufanya vizuri katika ligi na mashindano mengine yanayohusisha timu zenye wachezaji wazuri na walioandaliwa vyema na badala yake timu itahitaji muda mrefu ili wachezaji waweze kuzoeana na kupata uzoefu wa ligi.

Changamoto kubwa ambayo inaonekana kuisumbua Mbeya City katika Ligi Kuu msimu huu ni ubutu katika safu ya ushambuliaji kwani haina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kutumia nafasi chache ambazo timu hizo huzipata pindi inapokuwa inacheza.

Suluhisho la hilo ni uongozi wa Mbeya City kuingia sokoni katika dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka huu kunasa mshambuliaji mwenye sifa hizo lakini kwa bahati, timu hiyo italazimika kucheza michezo kadhaa ya ligi katika kipindi hicho jambo ambalo linaweza kupelekea wapoteze pointi zaidi katika baadhi ya michezo hiyo.

Inawezekana uamuzi wa kumtimua Amri Said wakauona ni sahihi lakini uongozi wa Mbeya City nao unatakiwa kubadilika na kuachana na uendeshaji wa timu kimazoea tofauti na unavyofanya sasa kwani timu inazidi kujiweka katika mazingira magumu ya kubakia katika Ligi Kuu.

Wanapaswa kukumbuka msimu uliopita walikuwa katika hatari ya kushuka daraja na walilazimika kutegemea mechi ya mchujo dhidi ya Geita Gold SC vinginevyo leo hii wangekuwa katika Ligi Daraja la Kwanza.

Ilitegemewa na wengi kuwa baada ya kuponea chupuchupu kukumbana na janga la kushuka daraja, uongozi wa Mbeya City ungefanya usajili wa wachezaji wazuri na bora ambao wangeifanya timu hiyo iwe imara na yenye ushindani msimu huu ili isikutane na kile kilichoisibu msimu uliopita.

Kwa bahati mbaya wameonesha kutojifunza kutokana na makosa na wanaiendesha timu kwa maisha yaleyale ambayo walikuwa nayo msimu uliopita.

Wahenga walisema bahati huwa haiji mara mbili. Wakiendelea hivyo, soka litawapa wanachostahili ambacho ni kushuka daraja. Hawaonekani kama timu inayochukia kufanya vibaya. Ni Mungu tu ambaye anaweza kuwaokoa.

 

Advertisement