Huku Shiboub, kule Mo Banka kitanuka

Muktasari:

Hapa Mwanaspoti linakuletea mastaa wanaotarajiwa kutisha msimu huu kwa vipaji walivyonavyo na hata vikosi vya timu wanazozichea.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Bara utafunguliwa rasmi kesho Jumamosi, kwa baadhi ya timu kucheza mechi za raundi ya kwanza, huku zile nne zinazowakilisha nchi, Simba, Yanga, KMC na Azam zikipangwa kuanza kukinukisha kuanzia mwanzoni mwa wiki ijayo.

Pazia la msimu huu lilifunguliwa kwa mchezo wa Ngao ya Jamii uliozikutanisha Simba na Azam na kumalizika kwa Wekundu kunyakua kwa mara ya pili mfululizo ikiitamba Azam kwa mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Taifa.

Hapa Mwanaspoti linakuletea mastaa wanaotarajiwa kutisha msimu huu kwa vipaji walivyonavyo na hata vikosi vya timu wanazozichea.

MO BANKA

Fundi huyu wa mpira, Mohammed Issa ‘Mo Banka’, anatabiriwa kung’ara katika kikosi cha Yanga kutokana na ubora aliouonyesha kwenye mechi chache za kirafiki akiwa ametoka kutumikia kifungo kilichomweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Kiungo huyo aliyemweka benchi Feisal Salum kwa sasa aliyetamba na Yanga msimu uliopita anajua soka buana asikuambie mtu, ule ufundi wake ulioonekana kwenye mechi dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi ni salamu tosha.

Banka ni mzuri pindi timu inaposhambulia na amekuwa mahiri kuanzisha mashambulizi zaidi ya msimu uliopita, lakini pia ni mzuri kwa kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na amekuwa akicheza kwa maelewano na mafundi wenzake Mapinduzi Balama na Papy Kabamba Tshishimbi.

PATRICK SIBOMANA

Winga mpya wa Yanga anatarajiwa kung’ara msimu ujao kutokana na kasi aliyoanza nayo akiwa mwepesi wa kupasia nyavuni katika mechi alizocheza tangu atue Jangwani akitokea Mukura Viktori ya Rwanda.

Ndiye aliyeifungia Yanga bao la kusawazisha dhidi ya Kariobang Sharks na kurudia tena katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga ilipoumana na Township Rollers ya Botswana. Ni mkali wa kupiga mipira iliyokufa na hata mabao yake ya mwisho katika mechi hizo za kimataifa zilitokana na mikwaju ya penalti.

Anajua kujiseti langoni mwa adui na ana kasi, chenga na pia anaonekana kuwa na uchu wa mafanikio kitu ambacho kama ataenda na moto huo, lazima afunike msimu huu.

SHIBOUB SHARAFELDIN

Kiungo huyu mpya kutoka Sudan ni balaa, kwani katika mechi tatu zilizopita za Simba dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, UD Songo ya Msumbiji na Azam kwenye Ngao ya Jamii ameonekana sio mtu wa mchezomchezo kabisa.

Shiboub anakaba, anatoa pasi na kufunga vilevile, kitu ambacho kinamfanya awe gumzo kwa mashabiki wa Simba kwa namna anavyojua kutimiza majukumu yake uwanjani.

Kama atakwenda na moto huohuo ndani ya Simba, hakuna kitakachomzuia kiungo huyo kufunika na kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi ambao, wamekuwa na misimu miwili mizuri iliyopita.

SHAABAN CHILUNDA

Kurejea kwake Azam FC kumezua maswali, lakini ukweli ni kwamba mshambuliaji huyo chipukizi ni fundi wa mpira na anajua kucheka na nyavu.

Aliondoka kwenda Hispania akiwa kinara wa mabao wa Azam na amerejea kuendeleza moto wake kama kawaida na walioliona pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, watakubali kuwa fundi amerudi na wapinzani wa Azam wajipange kwelikweli.

Chilunda amejaliwa kasi, chenga na mashuti kwani mara kadhaa amekuwa akifunga mabao ya mashuti ya mbali, achana na ile tikitaka yake dhidi ya Yanga misimu miwili iliyopita na kumfanya jamaa awashe taa ya kijani mapema kwamba, huu unaweza kuwa msimu wake.

JUMA BALINYA

Straika huyu mpya wa Yanga waliyesajiliwa kutokea Polisi Uganda kama mfungaji bora na kuingia rada za Simba kabla ya kuchomoa na kutua Jangwani ni mtu wa mipango.

Bado haijaizoea soka la Bongo, lakini kwa umahiri aliouonyesha katika mechi kadhaa alizopewa nafasi ya makocha wa Yanga ni wazi atakuwa moto mkali ligi itakapoanza.

Anatazamwa kama moja kati ya nyota watakaong’ara Yanga kama ataweza kufanya kama ambavyo ilikuwa akifanya nchi Uganda katika kutupia nyavuni.

MEDDIE KAGERE

Kama kuna mtu anadhani, Meddie Kagere aliotea tu msimu uliopita alipoibeba Simba kwa mabao yake 23 na kunyakua kiatu cha dhahabu, basi pole yake. Jamaa huyu nyota inaendelea kumng’aria na msimu huu anaweza kutisha zaidi ya ilivyokuwa msimu uliopita.

Kasi yake uwanjani, ujanja wa kuwachomoka mabeki na umahiri wa kuwaaibisha makipa ni vitu vinavyombeba Mnyarwanda huyu mwenye asili ya Uganda.

Kama mabeki wataendelea kuzembea mbele yake, basi mashabiki watarajie jina la MK14 likiendelea kutisha hata msimu huu, kwani jamaa anachezea sifa pale Msimbazi na hata mabeki wenyewe wanajua.

RICHARD DJODY

Benchi la ufundi la Azam, chini ya Kocha Etienne Ndayiragije mbali ya kuwa na mastraika wakali kama Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Emmanuel Mvuyekure na Shaaban Chilunda ameongeza kwa kumleta mkali mwingine kutoka Ivory Coast, Richard Djod.

Huyu jamaa kwa namna anavyoonekana uwanjani kwa kasi yake na namna alivyo na uchu wa kutupia, kuna kila dalili anaweza kuja kuwa Kipre Tchetche mwingine pale Azam FC.

GADIEL MICHAEL

Amesajiliwa na Simba akitokea Yanga na kuingia kikosi cha kwanza licha ya kwamba, amekutana na changamoto za kushindania nafasi ya kucheza na nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Gadiel ana kila dalili za kuendelea kung’ara msimu huu kama alivyong’ara akiwa Azam kabla ya kutua Jangwani na kuichezea Yanga kwa misimu miwili hasa kwa ile kasi yake ya kupanda na kushuka akitengeneza nafasi kwa washambuliaji wake.

FRANCIS KAHATA

Winga mpya wa Simba aliyosajiliwa akitokea Gor Mahia ya Kenya, tayari ameanza makeke yake ikiwamo kufunga moja kati ya mabao ya timu yake wakati wakiiangamiza Azam katikia Ngao ya Jamii.

Kahata ni miongoni mwa nyota wazuri ambao wapo Afrika Mashariki kwa sasa kutokana na umahiri wake wa kutumia mguu wa kushoto kwani, amekuwa akifanya hivyo katika Gor Mahia na kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars.

Umahiri wake huo uliomfanya agombewe na klabu kubwa nchini ni dalili za wazi kwamba msimu huu wanaweza kutisha Bara.

WENGINE

Licha ya orodha hiyo, lakini kuna wapo wachezaji wengine kibao wanaopewa nafasi kubwa ya kufunika msimu huu akiwamo Deo Kanda (Simba), Salim Aiyee(KMC), Farouk Shikhalo (Yanga) na Awadh Juma (Mtibwa Sugar).

Wengine ni Vitalis Mayanga (KMC), Beno Kakolanya (Simba) na Sadney Urikhob (Yanga).