Huku Morisson, kule Eymael poleni sana Yanga

Tuesday July 28 2020

 

By EDDO KUMWEMBE

JINSI maisha yanavyokwenda kasi Jangwani, majuzi Makamu Mwenyekiti alitishia kuondoka kama akiendelea kushutumiwa. Kesho yake staa wa timu akaonekana anacheza mechi za mchangani pale Msasani. Keshokutwa yake kocha wa timu akamwaga matusi kwa mashabiki na kuwafananisha na nyani na mbwa.

Mambo lazima yawe magumu kwa watoa uamuzi. Kama mtoa uamuzi mwenyewe, mtu kama Makamu Mwenyekiti, Fredric Mwakalebela anatishia kujitoa, nani atamchukulia hatua mchezaji kama Bernard Morisson?

Kwa haraka haraka jibu linaweza lisiwe Mwakalebela. Kwa sasa majukumu mengi ya Yanga yamebebwa na GSM. Hawa ndio ambao walimleta kocha, Luc Aymael ambaye juzi aliwaita mashabiki nyani na mbwa.

GSM chini ya Injinia Hersi Said wana kazi ngumu. Wana mwanzo wa wiki ngumu. Kazi ya kwanza ambayo wameifanya nadhani wameifanya kwa usahihi. Kumtimua kocha. Mzungu Luc alikuwa amevunja madaraja ya uhusiano na kila mtu nchini.

Amevunja uhusiano na viongozi wake, wachezaji wake, TFF, Simba, lakini zaidi na mashabiki na wanachama wa Yanga ambao ni roho ya klabu. Ilikuwa ni kazi rahisi kuhitimisha hili kwa sababu kabla hata hajatukana Yanga walishaamua kuachana naye. Nadhani alitukana kwa sababu alijua kwamba anaondoka.

Na sasa Yanga wana kazi ya kutafuta kocha mwingine. Kocha ajaye anatakiwa kuwa yule ambaye atasimamia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na pia kuifanya timu icheze kitimu. Tangu wakati wa Mwinyi Zahera, kisha huyu mzungu, sijawahi kuvutika na kandanda la Yanga.

Advertisement

Na wachezaji wengi pale Yanga viwango vyao vimedumaa na wamekosa mwelekeo. Hawa kina Abdulaziz Makame tuliambiwa ni wachezaji wazuri lakini kila siku naona viwango vyao vimedumaa. Kocha ajaye aamshe viwango vyao.

Lakini wakati huu GSM wakiwa wamepania kufanya kufuru, mastaa watakaoletwa Yanga inabidi wawe chini ya kocha anayeeleweka ili ijulikane nini ni tatizo hasa la Yanga. Wachezaji, uongozi au benchi la ufundi?

Msimu huu ulioisha Yanga waliweka rekodi ya kusajili wachezaji 22 tofauti. Bado hawakuwa na msimu mzuri na haijulikani tatizo lilikuwa wapi. Mchezaji kama Juma Balinya alichukuliwa baada ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda, lakini akaachwa katikati ya msimu.

Tuachane na hili la kocha. Yanga wameshalitibu kwa haraka. Tugeukie kwa Morrison. Yanga wanamalizaje tatizo la mtukutu huyu? Ninazo taarifa za uhakika kwamba Morrison alisaini mkataba wa miaka miwili Yanga Machi mwaka huu.

Hata hivyo, kwa hatua aliyofikia, Morrison amevunja madaraja yote ya uhusiano na mashabiki wa timu hiyo na hawezi kubakia klabuni. Mwenyewe anatamani kwenda Simba. Yanga kama wana uhakika na karata yao ni bora waachane naye kifaida. Wamuingize mnadani na kurudisha kiasi fulani cha pesa.

Hakuna mchezaji mkubwa kuliko klabu. Mambo ambayo Morrison ameyafanya Yanga hayajawahi kufanywa na mastaa wengi wakubwa waliopita klabuni hapo na kuitumikia timu kwa muda mrefu. Kina Sunday Manara na Edibily Lunyamila hawakuwahi kufanya haya.

Kuikomesha tabia hii ya Morrison ili asitokee Morrison mwingine klabuni, Yanga inabidi itengeneze kikosi chenye mastaa wengi. Wamemruhusu Morrison kujiona mkubwa zaidi klabuni kwa sababu hakuna mastaa wengi katika timu.

Miaka ya karibuni Yanga waliunda kikosi kilichokuwa na kina Simon Msuva, Donald Ngoma, Amis Tambwe, Obrey Chirwa, Juma Abdul, Thaban Kamusoko na wengineo. Morrison asingeweza kuwa mkubwa katika timu hii. Angekuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa kikosini.

Itazame Simba ya leo. Morisson anawezaje kupenya na kuwa mchezaji mkubwa klabuni? Kuna Francis Kahata, Clatous Chama, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, John Bocco, Mohamed Hussein, Luis Miquissone na wengineo. Morrison angepenyaje kuwa mkubwa kiasi cha kusumbua klabuni?

Kitu kingine kinachotia wasiwasi kwa Morrison ni utimamu wake wa akili. Nadhani hata mabosi wa Simba ambao walikuwa wanamtamani kwa nguvu kwa sasa watakuwa hawana furaha na akili yake. Sidhani kama kichwani yuko sawa.

Ni kweli kwamba unaweza kumtaka mwanamke fulani aachane na bwana wake ili uwe naye, lakini kuna wakati anamfanyia bwana wake visa mpaka vinakupa wasiwasi. Vituko anavyofanya Morrison hata wachezaji wetu wa ndani ambao tunasema hawajitambui hawawezi kufanya.

Tukiachana na suala la kocha na Morrison tunamgeukia Mwakalebela. Kutibu suala la Mwakalebela ni kwa klabu kwenda katika mabadiliko. Nguvu ya kiuchumi ya Yanga itatokana na mabadiliko ambao watayafanya. Na wakiwa na nguvu nzuri ya kiuchumi basi watatengeneza timu nzuri.

Wakiwa na timu nzuri hawawezi kuanza kuwa na hofu na timu kama ya Lipuli. Yanga walimshutumu Mwakalebela kwamba alitangulia kwenda Iringa kwa ajili ya kuwahujumu wafungwe na timu ya mkoa wake, Lipuli ili wasishuke daraja.

Hofu kama hizi zinakuja unapokuwa na mshambuliaji kama Yikpe. Ukiwa na washambuliaji kama Kagere na Bocco hauwezi kuwa na hofu na kikosi cha Lipuli. Kila mechi imekuwa ngumu kwa Yanga siku hizi ndio maana neno hujuma au uonevu limebakia kwao zaidi kuliko kwa wapinzani wao.

Simba wametulia na inaonekana kama vile viongozi wote makini. Hapana. Ni kwa sababu wana timu nzuri tu uwanjani. Wamekaa katika nafasi nzuri dhidi ya shutuma. Hata wanapofanya vibaya kwa kiwango chao lawama huwa zinakwenda kwa wachezaji wao.

Kwa Yanga hii ni rahisi kwa lawama kwenda kwa viongozi. Ni mara ngapi kina Kelvin Yondani waligoma kucheza kwa sababu ya kutolipwa mishahara? Hakuna kiongozi ambaye ataonekana mzuri Jangwani mpaka pale wachezaji watakapoanza kuishi maisha ya raha na yanayowastahili.

Advertisement