Huku Kisiga, kule Boban patamu hapo!

Muktasari:

  • Wachezaji hao wamewahi kucheza kwa mafanikio wakiwa na kikosi cha Simba na kutikisa soka la Tanzania kutokana na uwezo wao.


PIGA picha tu, huku kuna Shaaban Kisiga na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ halafu kule yupo Haruna Moshi ‘Boban’ na Jabir Aziz ‘Stima’, hapo utamu unakuwaje? Sasa chama la mafundi hao wa soka nchini lipo pale African Lyon baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu Bara kuwakusanya pamoja kupitia dirisha dogo linaloendelea.

Redondo, Kisiga na Stima wanaungana na Boban katika timu hiyo wakisajiliwa Lyon kutoka klabu nyingine tofauti na nyota hao wakongwe waliwahi kucheza pamoja wakiwa na kikosi cha Simba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nyota hao walisema wamefurahia kukutanishwa pamoja na kwamba kilichobaki ni kufanya mambo ya maana tu pale Lyon.

Kisiga alisema mbali na ushirikiano wa timu nzima, uwepo wa Boban, Redondo na Stima kikosini, anaamini watafanya maajabu kwani kombinesheni sio ya mchezo kabisa.

“Boban ana vitu vya peke yake, kuna wakati anaweza akatoa pasi wewe unayepokea unaona kipaji cha hali ya juu kwenye mguu wake, nimekuwa nikisema bila kificho kuwa sijaona kiungo wa staili yake,” alisema Kisiga.

“Stima na Chombo ni wachezaji wanaojua wanachokifanya, yapo mengi yanayoweza kumfanya mchezaji akakaa pembeni hata kama anajua kiasi gani, bila shaka tutafanya kitu cha tofauti, “alisema.

Stima aliyesajiliwa akitokea Friends Rangers ya pale Magomeni, alisema ni furaha kucheza na wachezaji anaoamini wana uwezo mkubwa kama Kisiga, Redondo na Boban “Asikuambie mtu wachezaji tunajuana uwezo wetu, tutafanya kazi hilo ndilo la msingi,” alisema.

“Napenda miguu yangu ifanye kazi yake, hakuna mwenyewe katika ligi nafasi ipo wazi,” alisema Boban.