Huko Yanga ishu si jina, CV ndo mpango mzima

Muktasari:

  • Alisema timu hiyo pia inahitaji kuwa na kipa mzoefu mwenye kiwango ambaye akisimama golini, mashabiki wanashusha presha, lakini pia kuwa washambuliaji watatu.

WAKATI wagombea walioenguliwa kwenye usaili katika uchaguzi wa Yanga kesho Jumatano wakianza kuwasilisha rufani zao dhidi ya Kamati ya Uchaguzi kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, mshambuliaji nyota wa zamani wa Yanga na mwanachama wa klabu hiyo, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ ametoa rai kwa wapiga kura katika uchaguzi huo.

Kesho Jumatano hadi Ijumaa itakuwa ni siku ya kukata rufani dhidi ya Kamati ya Uchaguzikisha rufani hizo kuanza kusikilizwa kabla ya orodha ya mwisho ya wagombea kutangazwa Jumatatu ijayo ili kupisha mchakato wa kampeni siku inayofuata tayari kwa uchaguzi huo wa Mei 5.

Wakati mchakato huo ukiendelea, Homa ya Jiji ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo ametoa rai kwa wapiga kura wa Yanga akiwasisitiza kutochagua viongozi kwa umaarufu wa majina ya wagombea, bali wazingatie wasifu wa mgombea.

“Yanga kwa ilipo sasa inahitaji kiongozi ambaye atakuwa na mlengo wa maendeleo na si kiongozi jina,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani na kusisitiza:

“Klabu inahitaji kiongozi mwenye maono, uwezo binafsi katika utendaji na ili tufike hatua ambayo ndiyo ndoto ya kila Mwanayanga. Tupige kura bila kuangalia jina la mgombea, bali uwezo wake kama unaendana na klabu ya Yanga,” alisema.

Alisema Yanga ina matatizo makubwa kuanzia katika timu kwani kikosi kilichopo kinapaswa kufumuliwa na Yanga kufanya usajili wenye tija utakaokuwa na faida ndani ya klabu na hilo ni jukumu la kiongozi ajae kuwa na mikakati madhubuti.

“Timu inahitaji maboresho makubwa, kuanzia kwa kipa, viungo na hata beki iongezewe nguvu, kwani Yondani (Kelvin) pamoja na kuwa anafanya vizuri, huwezi kumtegemea pekee kwani ndiyo anaelekea ukingoni katika soka,” alisema.

Alisema timu hiyo pia inahitaji kuwa na kipa mzoefu mwenye kiwango ambaye akisimama golini, mashabiki wanashusha presha, lakini pia kuwa washambuliaji watatu.

“Tukiwa na wachezaji aina ya Makambo au zaidi pale mbele watatu, kina Tshishimbi wawili, Fei Toto wawili, Yanga itaimarika, lakini sasa ukiachana na hao niliowataja na Kamusoko ambaye pia anaelekea ukingoni, bado timu ina changamoto,” alisema.

Alisema mbali na usajili, pia uongozi utakaoingia madarakani unapaswa kuweka utaratibu mzuri kwa wanachama kuchangia klabu, lakini pia usione ugumu kufuata nyayo za watani zao Simba katika mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.