Huko Yanga, mambo yameiva

Muktasari:

UONGOZI mpya wa Yanga chini ya Dk Mshindo Msolla na Makamu Mwenyekiti wake, Fredirck Mwakalebela uliingia madarakani Mei 5, mwaka jana katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam.

MABINGWA wa kihistoria wa Tanzania, Yanga umeamua kufuata mfumo wa uongozi wa kisasa wa klabu maarufu ya Hispania, Sevilla FC na kesho saa 1 usiku watasaini mkataba la Kampuni ya La Liga.

Hatua hiyo imefikia baada ya uongozi wa klabu hiyo kwa kushirikiana na wadhamini, GSM kuvutiwa na mfumo huo ambao umeifanya klabu ya Sevilla kuwa na maendeleo mazuri nchini Hispania.

Yanga itasaini mkataba na kampuni ya La Liga inayoendesha Ligi Kuu ya Hispania katika hafla iliyopangwa kufanyika kwenye hoteli moja ya kitalii ya nyota tano iliyopo jijini Dar es Salaam.

Habari kutoka ndani ya Yanga zimesema kutokana na mazingira tofauti ya mifumo ya mpira, uongozi wa Yanga hautabadili umiliki wa klabu ambao utabaki kwa wanachama.

Hali hiyo itaendelea kuwapa wanachama fursa ya kushiriki katika mambo mbali mbali ya klabu tofauti na fikra za watu wengine.

“Wananchama wataendelea kuwa na nafasi katika klabu ya Yanga, sera ya nchi inawapa umiliki wa asilimia 51, hivyo bado watakuwa na fursa ya kuchangia mambo ya maendeleo, ila mfumo wa uongozi utakuwa wa kisasa zaidi,” alisema chanzo chetu.

Alisema mfumo halisi wa uongozi wa klabu utatangazwa kwenye uzinduzi huo ambapo kampuni ya GSM itagharimia gharama za hatua za awali za malipo kwa kampuni ya La Liga.

Chanzo chetu kiliongeza, Yanga pia inatarajiwa kupata faida kutoka timu ya Sevilla kwani baadhi ya wachezaji wake wa timu za vijana watapata nafasi ya kwenda kujifunza na kufanya majaribio huko.

“Sevilla ni timu kubwa ambayo  ina kituo maarufu ya vijana hivyo tunatarajia kupeleka wachezaji wetu huku kufanya majaribio na vile vile kujifunza kutoka kwao,” alisema .

Naye Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, alisema; "Tunakwenda kutia sahihi, uanzishwaji  kamili wa mchakato sahihi wa kwenda na wakati husika. Ni mkataba baina ya Yanga na La Liga. Ukisimamiwa na ukifadhiliwa na GSM. Sio GSM ambaye ndiye anafanya mabadiliko. Mabadiliko yatafanywa na Yanga."

Nugaz alisema uamuzi wa kuwashirikisha La Liga umetokana na uzoefu walionao kutokana na uendeshaji na mafanikio ya soka la Hispania.