Huko Msimbazi hakuna kulala

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi aliliambia Mwanaspoti baada ya mechi yao ya juzi Jumamosi maandalizi ya mechi ijayo yalianza ikiwamo kuchagua kikosi kitakachosafiri.

PEMBA.KIKOSI cha Simba jioni ya jana Jumapili kilikuwa Uwanja wa Gombani, kisiwani hapa kuvaana na Azam FC katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, lakini mabosi wake hawajalala kwani wameshaanza mipango ya safari ya timu kwenda DR Congo.

Simba itaenda Kinshasa kucheza dhidi ya AS Vita katika mechi ya pili ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika siku chache baada ya kuifumua JS Saoura ya Algeria.

Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi aliliambia Mwanaspoti baada ya mechi yao ya juzi Jumamosi maandalizi ya mechi ijayo yalianza ikiwamo kuchagua kikosi kitakachosafiri.

“Nawapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi nzuri ya jana (juzi) Jumamosi pamoja na mashabiki kwa kutoa sapoti kubwa, sisi hatupumziki kwani tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi ijayo,” alisema Mkwabi.

“Baada ya mechi kocha aliteua kikosi kitakachosafiri kitakachongazwa baadaye na timu itaondoka Alhamisi kwa Shirika la Ndege la KQ. Bado tunaomba sapoti kutoka kwa mashabiki wetu kuelekea mafanikio,” alisema Mkwabi

ISHU YA NDEMLA

Mkwabi alizungumzia ishu ya kiungo wao, Said Ndemla anayeondoka leo Jumatatu kuelekea Sweden kwa kufafanua;

“Kwanza Kocha Patrick Aussems alimteua Ndemla kucheza fainali ya Mapinduzi, lakini alipata taarifa juu ya safari hiyo hivyo akabadilisha na kumteua Mzamiru Yassin aliyepigiwa simu tayari naye alikuwa safarini kuelekea Morogoro kwa shida ya kifamilia, ndio maana naye hajaja.”

“Ndemla anakwenda kwenye timu yake ile ile aliyofanya majaribio mara ya kwanza atakuwa huko kwa wiki mbili, ni muda mrefu umepita hivyo wanataka kujiridisha tena kiwango chake ikiwemo kufanyiwa vipimo vya afya,” alisema Mkwabi.

Awali ilisemwa Ndema alifuzu kuitumikia timu hiyo.