Huko Jangwani kicheko kitupu

Muktasari:

Inaelezwa mzigo ulioingizwa Jangwani ni karibu Sh 300 milioni zilizotokana na mgao wa awamu ya pili, huku ikielezwa fedha hizo zimepunguza matatizo ya wachezaji na mabosi wa benchi la ufundi.

KIKOSI cha Yanga jana Alhamisi kiliendelea kujifua kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini kujiweka tayari kwa ngwe ya pili ya Ligi Kuu Bara, lakini taarifa tamu kwa mashabiki ni kwamba ule mshiko wao kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) umetua mwanangu.

Ni hivi. Yanga ilikuwa kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na Gor Mahia ya Kenya, USM Alger ya Algeria na Rayon Sport ya Rwanda. Sasa unaambiwa mgao wa awamu ya pili kwa timu hizo umeshatua kwa timu zote zilizokuwa Kundi D.

Inaelezwa mzigo ulioingizwa Jangwani ni karibu Sh 300 milioni zilizotokana na mgao wa awamu ya pili, huku ikielezwa fedha hizo zimepunguza matatizo ya wachezaji na mabosi wa benchi la ufundi.

“Angalau sasa tunapumua kwani mzigo kutoka CAF umeingia,” kilisema chanzo kutoka Yanga.

Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alipoulizwa juu ya jambo hilo, alikanusha kupokea mgao huo huku akionekana kuwa mkali baada ya kuulizwa zaidi kuwa, mbona klabu walizokuwa nao kundi moja zimeshapewa mgawo wao na CAF.