Huko Bunju kumenoga kinoma

WAKATI familia na wadau mbalimbali wa soka nchini jana Jumamosi wakifurahia kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji ‘Mo’, huko kwenye Uwanja wa Simba uliopo Bunju nako mambo yamenoga kwani mafundi wanaendelea kupambana kufanikisha lengo la mzabuni huyo anayetaka hadi Februari mwakani ukamilike.

MO alitekwa wiki iliyopita ikiwa ni siku 9 kupita amepatikana usiku wa kuamkia jana Jumamosi akiwa ametupwa eneo la Viwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam huku ikielezwa kuwa watekaji walihitaji wapewe pesa.

Mkandarasi wa uwanja huo unaojengwa na Kampuni ya Masasi Constaructions, Eng Danny alisema hawakusimamisha ujenzi huo kwani tayari waliingia mkataba na tajiri huyo ambaye alipita kwenye mchakato wa awali tenda ilipotangazwa akiwa ni mzabuni pekee aliyejitokeza kuomba uwekezaji ndani ya Simba kwa Sh 20 bilioni akimiliki hisa asilimia 49.

Eng Danny alisema hatua iliyofikiwa sasa ni kuweka mabomba ya kunyonya maji ya mvua na kuyatoa nje na baada ya hapo hatua nyingine itafuata wakati uwekaji nyasi za bandia ukiwa wa mwisho kabisa. “Tunaendelea na kazi kama kawaida, tupo hatua ya kuweka mabomba na baadaye tutahamia hatua nyingine, Tunashukuru Mungu MO amepatikana akiwa hai hilo ndiyo jambo kubwa mno. “Kwa vile tuliingia makubaliano ya kimkataba na kila kitu kilinunuliwa hatukuwa na sababu ya kuacha kuendelea na ujenzi wakati vyombo vya dola vikiendelea na kazi yao ya kumtafuta MO,” alisema Eng Danny

Katika ahadi za MO ujenzi wa uwanja wa Bunju ndiyo ilikuwa ahadi yake ya kwanza kuanza kuitekeleza na baadaye kuhamia kwenye mipango mingine.

MO anajenga uwanja huo wa mazoezi ambao unagharimu Sh 600 milioni huku iliwekwa wazi kwamba uwanja huo utaanza kutumika Februari mwakani.