Huduma zao ghali kinoma ila hawachezi timu za taifa

Muktasari:

Hawa hapa wachezaji ghali ambao hawajawahi kuzitumikia timu zao za taifa za wakubwa.

LONDON, ENGLAND.KUCHEZEA timu ya taifa ni ndoto ya takriban kila mchezaji, bila ya kujali kwamba atabeba mataji mengi kiasi gani kwenye klabu yake.

Lakini, kuna mastaa hao wana vipaji vikubwa vya soka, kiasi cha kufanya hata saini zao zinaswe kwenye pesa nyingi, hata hivyo hawajawahi kuitwa hata siku moja kwenda kuzichezea timu zao za taifa za wakubwa.

Hawa hapa wachezaji ghali ambao hawajawahi kuzitumikia timu zao za taifa za wakubwa.

5. Alex Teixeira - Pauni 38.5 milioni

Alex Teixeira umri wake ni miaka 29, lakini bado hajaitwa kuichezea timu ya taifa ya Brazil. Alichezea timu za watoto tu, lakini hajawahi kugusa kwenye kikosi cha wakubwa licha ya kipaji alichokuwa nacho.

Klabu ya Jiangsu Suning ya China haikujali hilo wakati ilipoamua kutoa Pauni 38.5 milioni kunasa huduma yake na kumfanya Teixeira kuwa mmoja wa wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi, lakini hawajawahi kuchezea timu za taifa.

4. Vinicius Junior - Pauni 38.7 milioni

Vinicius Junior ndio kwanza umri wake ni miaka 18 tu, lakini kipaji chake ni balaa zito. Jambo hilo limewafanya Real Madrid kutofikiria mara mbili wakati walipotoa Pauni 38.7 milioni kunasa huduma yake bila ya kujali hajawahi kuichezea timu ya taifa ya wakubwa hata mara moja. Kinda huyo amenaswa kwa pesa nyingi, lakini anakuwa mmoja wa wachezaji ambao saini zao zimegharimu pesa nyingi wakiwa hawajawahi kuchezea timu za taifa za wakubwa.

3. Rodrygo - Pauni 40 milioni

Kinda mwingine aliyeigharimu Real Madrid pesa ndefu ni Rodrygo. Wababe hao wa Bernabeu walitoa Pauni 40 milioni kunasa huduma ya Mbrazili huyo. Santos wamekuwa wakiamini katika uwezo wa mchezaji huyo na jambo hilo liliwafanya Real Madrid kutoa pesa ndefu kunasa huduma yake licha ya kwamba mchezaji huyo hajawahi kuitwa kuichezea timu ya wakubwa ya taifa ya Brazil.

2. Aaron Wan-Bissaka - Pauni 50 milioni

Manchester United ilikuwa na matatizo ya beki wa kulia na ndio maana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya wameingia sokoni kunasa huduma ya Aaron Wan-Bissaka kutoka Crystal Palace. Beki huyo alicheza kwa msimu kamili mmoja tu huko Palace na kuzivutia klabu nyinngi kiasi cha kuwafanya Man United kutoa Pauni 50 milioni.

Man United wametoa pesa hiyo nyingi kwenye kusajili mchezaji ambaye bado hajaitwa kuichezea timu ya taifa ya wakubwa.

1. Aymeric Laporte - Pauni 57.2 milioni

Mchezaji mwenye umri wa miaka 25 mwenye uwezo wa kuzichezea timu za taifa za Hispania na Ufaransa, inashangaza kuona beki wa kati wa Manchester City, Aymeric Laporte kwa ubora wote aliokuwa nao, hajaitwa kuichezea timu ya taifa.

Man City wala hawakujali hilo walipotoa ada ya Pauni 57.2 milioni kunasa saini yake ilipomnasa kutoka Athletic Bilbao.