Hoteli 6 zalamba dili tamu

Friday March 15 2019

 

By CHARLES ABEL

HOTELI sita za kifahari zimethibitishwa rasmi kupokea ugeni wa timu na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) utakaokuja kwenye Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, zitakazofanyika nchini Aprili 14 hadi 28.
Timu hizo ni nane ambazo zitashiriki mashindano hayo ni wenyeji Tanzania 'Serengeti Boys', Uganda, Angola, Morocco, Nigeria, Cameroon, Guinea, na Senegal huku maofisa wakiwa ni waamuzi watakaochezesha mechi hizo, makamishna pamoja na wale wa idara mbalimbali za CAF.
Mtendaji Mkuu wa Kamati ya Ndani ya Maandalizi ya mashindano hayo, Leslie Liunda aliliambia gazeti hili kuwa hoteli hizo sita zimepata fursa hiyo baada ya kukidhi vigezo na sifa zilizowekwa na CAF hasa sauala la malazi, usalama na vyakula.
"Tayari tumeshapanga hoteli ambazo timu na maofisa  wa CAF watakuwepo katika kipindi chote cha mashindano na kila nchi inaruhusiwa kutuma maofisa wake kuja kufanyia ukaguzi hizo hoteli ambazo tumezipangia kukaa katika kipindi chote cha mashindano.
Timu Serengeti Boys pamoja na Morocco zimepangiwa kwenye Hoteli ya Ledger Plaza na Nigeria na Senegal zenyewe zitakuwepo Hoteli ya Seascape. Angola na Cameroon zenyewe zitakuwepo kwenye Hoteli ya Holiday Inn na Uganda na Guinea wenyewe watakuwa Hoteli ya Peacock. Marefa watakuwa kwenye Hoteli ya Tiffany Diamond na Maofisa wa watakuwa kwenye Hoteli ya Sea Cliff," alisema Liunda.
Liunda alisema kuwa kuna kundi kubwa la wageni ambalo linategemewa kufika nchini kwa ajili ya mashindano hayo hivyo ni vyema hoteli zikachangamkia fursa ya kutoa huduma kwao.

Advertisement