Hongereni Yanga na Simba SC kwa pambano la Kistaarabu

Muktasari:

  • Ukianza na tukio la kuingia uwanjani mashabiki walionekana kuwa na nidhamu kubwa katika kukata tiketi na hata kuingia ndani ya uwanja huku ulinzi ukiwa mzuri usioleta kero kwa mashabiki na kama kulikuwa na dosari hazionekani kuwa kubwa.

MECHI ya Yanga na Simba imemalizika baada ya kuchezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mechi hiyo ni moja kati ya mechi kubwa hapa nchini na hata Afrika Mashariki na inapokuwa inakaribia maandalizi yanakuwa makubwa kwa kuzihusisha mamlaka mbalimbali za Usalama wa nchi.

Umakini wa vyombo vya usalama kushirikiana na Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) sambamba na klabu mbili husika ni katika kuhakikisha mchezo huo unakuwa na maandalizi mazuri na kumalizika salama.

Tofauti na huko nyuma mechi ya iliyopita baina ya timu hizo imethibitisha kwamba mechi hiyo inaweza kumalizika kwa amani na utulivu na kuwafanya mashabiki wa timu zote mbili kurudi majumbani kwao kwa utulivu.

Ukianza na tukio la kuingia uwanjani mashabiki walionekana kuwa na nidhamu kubwa katika kukata tiketi na hata kuingia ndani ya uwanja huku ulinzi ukiwa mzuri usioleta kero kwa mashabiki na kama kulikuwa na dosari hazionekani kuwa kubwa.

Hali kadhalika hata maafisa wa usalama nao hawakuwa na matukio ya kuwakimbiza mashabiki kama ilivyozoleka kwa kuwa wakali na kupiga watu hovyo na kufanya mambo kwenda kwa ustaarabu mkubwa.

Mpaka sasa hakuna matukio makubwa yaliyojitokeza ambayo yangeweza kuleta picha mbaya katika mechi kama hii zaidi ya timu zote mbili kuendelea na majukumu hayo.

Hii inathibitisha sasa kwamba viongozi, wanachama na mashabiki wa timu zote mbili wameanza kukomaa na kuwa na nidhamu ya soka ambayo matokeo ya mwisho yanaheshimiwa na shughuli nyingine za kujenga Taifa zikiendelea.

Tumezoea kuona mechi kama hii inapomalizika hasa timu moja inapopoteza vurugu za kukataa matokeo au kuwa wakali kwa viongozi wao na hata wachezaji huwa kubwa na kulazimu polisi kutawanya watu kwa nguvu lakini katika mechi iliyopita hakukuwa na kitu cha namna hiyo.

Yanga walipoteza mchezo lakini walionekana kuyakubali matokeo na kutoka uwanjani kwa utulivu wakiangalia mechi zinazofuata kwa timu yao.

Hali kadhalika Simba nao ambao walikuwa washindi hawakusababisha vurugu zozote katika kuwakebehi wenzao na kuleta bughudha kila mmoja alitoka na furaha na kurudi alikotoka kuendeleza furaha yake.

Wachezaji wa timu zote mbili nao walionyesha kandanda safi kwa kuonyeshana ufundi uwanjani kutetea klabu zao bila kuwa na matukio ya kukamiana na kuumizana kama ilivyokuwa inatokea katika mechi kama hizi huko nyuma.

Jambo zuri zaidi mchezo ulipomalizika kila mchezaji alimpongeza mwenzake kuashiria mchezo wa kiungwana kama ambavyo Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) linashauri.

Wakati mwingine uharibifu wa utulivu husababishwa na maamuzi ya waamuzi ambao hata hivyo nao licha ya dosari ndogo za kibinadamu walifanikiwa kusimamia sheria za soka kuhakikisha mshindi halali anapatikana.

Soka sio uadui na upinzani wa Yanga na Simba ni kwa mlengo wa kimichezo na hiki ndicho tunachokipongeza kuanzia wasimamizi wa mchezo mpaka timu zenyewe kwa kuwa na mchezo mzuri.

Ukomavu huu unatakiwa kuendelea kuthibitisha ukongwe wa timu hizo katika medani ya soka hapa nchini kuzidi kuzifunza timu zingine kuiga mfano huo.

Rai yetu ni kwamba TFF iendelee na usimamizi kama huu kuhakikisha mechi kama hizi hazileti matukio ya ajabu kuweza kuzivutia klabu husika kupata udhamini zaidi wakati huu ambao dunia inaangalia mechi hizi kwa kuwa zinaonyeshwa mubashara.

Mpambano kama ule unapomalizika salama kunaashiria mambo mengi nyuma yake, kwanza viongozi, wachezaji na mashabiki kukua kisoka na kuhitaji kufurahia kandanda linaloonekana ndani ya uwanja na wala sio mambo yaajabu.

Hakuna anayeona jambo la ajabu kutokea kwa tambo mbalimbali kwa mashabiki kwa sababu nayo ni sehemu ya michezo bali kinachoonesha ushamba ni yale yanayofanyika kwa uvunjifu wa amani na hata mali za uwanjani eti kisa ni ushabiki.

Ni pongezi kwa wote waliokubali yaishe hasa kwa upande wa mashabiki wa Yanga kwani licha ya kufungwa, waliondoka kwa amani uwanjani licha ya kuwa na maumivu ya kupoteza mchezo huo ambao ulikuwa muhimu pande zote mbili.