Hofu ya mechi yampandisha presha kocha Mgambo Shooting

Muktasari:

Mgambo Shooting iliambulia sare mfululizo katika mechi zake ilizocheza za Ligi Daraja la Kwanza kwenye  uwanja wao wa nyumbani,ambapo Oktoba 20 itakuwa ugenini mkoani Mbeya kuwakabili Boma FC.

 WAKATI mashindano mbalimbali nchini yakiwa yamesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Kocha wa Mgambo Shooting, Elias Kija amesema kuwa timu yake haitapumzika kutokana na matokeo waliyonayo badala yake ni matizi mwanzo mwisho.

Timu hiyo ambayo sasa imehamishia maskani yake  mkoani Tabora inashiriki Ligi Daraja la Kwanza katika kundi B ambapo kati ya mechi mbili walizocheza hadi sasa imevuna pointi mbili,huku vinara katika kundi hilo Arusha United wamekusanya alama Nne sawa na Geita Gold.

Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Kija alisema kuwa kutokana na matokeo waliyopata kwenye mechi zao mbili hayajamfurahisha badala yake wataendelea kujifua kwa kipindi hiki cha mapumziko mafupi.

Alisema kuwa licha ya kwamba vijana wake wanacheza vizuri na kumpa nguvu,lakini hajafurahishwa na safu yake ya ushambuliaji ambayo imembidi atenge muda wa ziada kuhakikisha inakaa sawa.

“Sisi hatuna cha kupumzika ukizingatia matokeo yetu si mazuri sana kwa sababu nililenga kila mchezo nipate pointi tatu lakini imekuwa tofauti,kwahiyo lazima tuendelee kujifua ili Ligi ikiendelea tuwe fiti”alisema Kija.

Kocha huyo aliongeza kuwa licha ya Ligi kuwa ngumu pamoja na kundi walilomo kuwa na ushindani lakini anaamini timu hiyo itarudi kwa nguvu na lazima wafikie malengo yao ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Kija alisema kuwa kwa sasa wakati wanaendelea kujinoa akili na mawazo yao yanafikiria mchezo ujao dhidi ya Boma FC utakaopigwa mkoani Mbeya kuhakikisha wanashinda.

“Ligi ni ngumu na kundi letu ni la ushindani lakini tutapambana kuhakikisha tunafikia malengo yetu ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao,kwa sasa tunaiwazia mechi yetu ya ugenini dhidi ya Boma FC”alisema Kocha huyo.