Hofu tupu! Mashabiki Man Utd walia kupangwa kundi la kifo

LONDON, ENGLAND. KUMEKUCHA. Mashabiki wa Manchester United wamefyumu na kudai kwamba droo ya upangaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu “imepangwa” baada ya chama lao kupangwa Kundi la Kifo pamoja na PSG na RB Leipzig.

Mashabiki hao walioshtushwa na makundi hayo, walisema kikosi chao kinachonolewa na Ole Gunnar Solskjaer kimefanyiwa makusudi kwa kupangwa na timu ngumu tofauti na ilivyo kwa wapinzani wao kwenye Ligi Kuu England hasa mahasimu wao, Manchester City.

Kwenye makundi hayo, Man City ya kocha Pep Guardiola imepangwa pamoja na FC Porto, Olympiacos na Marseille, wakati Liverpool imepangwa kwa kundi moja na Ajax, Atalanta na Midtyjlland huku Chelsea wakipewa Sevilla, Krasnodar na Rennes.

Na mashabiki wa Man United waliripuka kwenye mitandao ya kijamii, shabiki mmoja alisema: “Usiniambie kwamba hii haijapangwa! Droo ya hovyo sana.”

Shabiki mwingine aongeza: “Nadhani walitumia mapumziko ya muda wa kutoa zawadi wakati watangazaji wakilandalandaa na kuipangia ratiba nyepesi Man City.”

Kuna shabiki alisema: “Liverpool imepewa Ajax, Man City imepewa Porto na sisi tumepewa PSG, hii droo imefanywa na mafia wawili wa Chelsea!!!??”

Shabiki mwingine aliandika kwenye tweeter: “Mungu wangu tunakabiliana na watu waliofika nusu fainali na fainali msimu uliopita hata bado hatujafika hatua ya 16 bora. Hili Kundi la Kifo.”

Kuna shabiki mmoja alifika mbali zaidi akiitaka klabu hiyo kusajili wachezaji wapya, aliandika kwenye twitter: “PSG, United na Leipzig......tumia pesa Ed au tukumbane na shida Oktoba. Tutacheza na Chelsea na Arsenal katikati ya mechi hizo.”

Mashabiki wa Man United wanawaza watakapowakabili Neymar na Kylian Mbappe, United italazimika kucheza na RB Leipzig huku wakikabiliwa na mabingwa wa Uturuki, Istanbul Basaksehir.