Hizi ndizo sifa za mikutano Simba

Thursday September 13 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

JUZI Jumanne katika mfululizo wa uchambuzi wa Katiba Mpya ya Simba, tuliona haki ya wanachama ilivyo na mambo mengine ambayo wanachama wa klabu hiyo kongwe wanapaswa kuwa nayo ama kuepukana nayo.

Leo tunaendelea nayo tukiangazia sifa za mikutano ndani ya klabu hiyo na mambo gani ambayo ni muhimu zaidi katika kuifanya Simba iendeshwe kwa mafanikio.

Endelea nayo...!

IBARA YA 22:

Ajenda ya Mkutano Mkuu wa kawaida.

Ajenda ya Mkutano Mkuu wa kawaida itajumuisha mambo yafuatayo ya kikatiba;

(a). Kuhakiki idadi ya wanachama wanaohudhuria mkutano

(b). Kuthibitisha ajenda

(c). Kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliopita

(d) Yatokanayo na kumbukumbu za mkutano uliopita

(d). Hotuba ya Mwenyekiti

(f). Kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kutoka Bodi ya Wakurugenzi.

(g). Kupokea taarifa ya hesabu za fedha zilizokaguliwa za mwaka uliotangulia za Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(h). Kupokea bajeti ya mwaka ya shughuli na mipango ya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(i) Uchaguzi wa nafasi zozote zilizo wazi za Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(j). Kupokea na kujadili mapendekezo ya marekebisho ya kanuni na Katiba za Simba Sports Club.

(k) Kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na wanachama au Bodi ya Wakurugenzi.

IBARA YA 23:

Mkutano Mkuu wa dharura

1. Bodi ya Wakurugenzi inaweza kuitisha mkutano mkuu wa dharura kama itaona inafaa.

2. Endapo wanachama hai wasiopungua 1,000 watajiorodhesha na kuwasilisha kimaandishi ombi kwa Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki wa Simba Sports Club, Bodi ya Wakurugenzi itawajibika kuitisha mkutano mkuu wa dharura katika kipindi kisichozidi siku 30 baada ya kupokewa kwa ombi.

3. Wito wa mkutano mkuu wa dharura hauna budi kupelekwa kwa wanachama kupitia matawi yao angalau siku 15 kabla ya mkutano.

4. Ajenda na nyaraka nyingine muhimu zitapelekwa kwa wanachama kupitia kwenye matawi angalau siku saba kabla ya mkutano.

5. Endapo Mkutano Mkuu wa dharura utaitishwa kwa juhudi za Bodi ya Wakurugenzi, basi Bodi ya Wakurugenzi itaandaa ajenda. Endapo utaitishwa kwa

ombi la wanachama 1,000, ajenda itakuwa na masuala yaliyopendekezwa na wanachama hao.

IBARA YA 24. Akidi

1. Maamuzi ya Mkutano Mkuu yatakuwa halali wakati watakapopitishwa kwa wingi wa kura (50%+1) za wanachama waliohudhuria wenye haki ya kupiga kura, bila kuathiri aya ya 2 ya Ibara hii. Mkutano MKuu utakuwa ni halali endapo idadi hiyo ya wanachama wasiopungua 500. Endapo idadi hiyo ya wanachama haitafikiwa basi mkutano mkuu utaendelea siku inayofuata hata kama idadi ya wanachama haitofikia mia tano.

2. Iwapo akidi haikutimia, Mkutano mkuu utafanyika siku inayofuata kwa agenda zile zile. Katika mkutano huo hakutahitajika akidi, isipokuwa kama kuna ajenda ya marekebisho ya Katiba ya Simba Sports Club, uteuzi wa watendaji, kufukuzwa kwa mjumbe mmoja au wengi katika chombo cha Simba Sports Club.

IBARA YA 25:

Uendeshaji wa Mkutano Mkuu

1. Mkutano Mkuu utaendeshwa na Mwenyekiti aliyechaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 27 (1) (a) ya Katiba hii, Mwenyekiti asipokuwepo Bodi ya Wakurugenzi itachagua mjumbe mmoja kati ya wajumbe sita wa Bodi ya Wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 27 (1) (a) - (b) kuwa Mwenyekiti wa Mkutano.

2. Mkutano unaweza kuteua idadi ya kutosha ya waangalizi.

3. Wanachama watazungumza katika mkutano kwa kutumia lugha rasmi ya Simba Sports Club.

4. Mwenyekiti atakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mkutano unaendeshwa kama ulivyopangwa. Kwa hali hiyo, Mwenyekiti atakuwa anayo haki ya kukatiza hotuba za wanachama.

5. Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki atatayarisha kumbukumbu za mkutano na kuwapelekea wanachama kupitia matawi yao mwezi mmoja baada ya mkutano.

IBARA YA 26:

Maamuzi na uchaguzi

1. Mkutano MKuu hautatoa uamuzi kwa suala lolote lisilokuwamo katika ajenda.

2. Kila mwanachama rasmi atakuwa na kura moja na hatawakilisha zaidi ya mjumbe mmoja.

3. Uchaguzi utafanywa kwa kura ya siri

4. Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika Katiba, maamuzi ya Mkutano Mkuu yatafanywa kwa wingi wa kura zilizopigwa na wanachama rasmi.

5. Maamuzi ya marekebisho yoyote ya ajenda katika Katiba na Kanuni, Mabadiliko yoyote ya ajenda ya Mkutano Mkuu...

Je unawafahamu wanaostahili kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba. Sifa zao je zikoje na nani hastahili? Majibu yote utayapata kesho Ijumaa.

Advertisement