Hizi ndizo mechi kali za FDL zilizobamba

Muktasari:

Katika michezo 18 iliyopigwa, kuna baadhi ya mechi ambazo ziliacha alama kutokana na timu hizo zilipokutana katika msako wa alama tatu, na Mwanaspoti linakuchambulia michezo 10 kati ya 21 iliyopigwa.

HATUA ya mzunguko wa 18 wa Ligi Daraja la Kwanza ilipofikia ni balaa tupu, kwa maana nyingine kila mtu acha ashinde za kwake tu.

Gwambina FC inahitaji alama tatu kujihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao, na kama sio ligi kusimama basi kwa sasa zingekuwa habari nyingine kwa upande wao.

Katika michezo 18 iliyopigwa, kuna baadhi ya mechi ambazo ziliacha alama kutokana na timu hizo zilipokutana katika msako wa alama tatu, na Mwanaspoti linakuchambulia michezo 10 kati ya 21 iliyopigwa.

GEITA GOLD 2-2 MASHUJAA FC

Kipute hicho kilipigwa katika Uwanja wa Nyamkumbu na wenyeji Geita kubanwa mbavu katika mchezo huo wa ufunguzi Septemba 14, mwaka uliopita.

Mabao ya wenyeji hao yaliwekwa kambani na Simba Boazi pamoja na Geofrey Jojo wakati Shedrack Ntabindi aliifungia Mashujaa FC na bao la pili lilitokana na Yusuph Mgeta kujifunga.

GWAMBINA FC 2-2 GIPCO FC

Gwambina FC iliingia katika mchezo huo ikiwa na matokeo chanya kwenye michezo yake miwili iliyopita ikiichapa 3-1 Arusha FC na kuilaza 1-0 Stand United.

Lakini katika mtanange huo mambo yaliwaendea kombo vijana hao wa Kocha Novatus Fulgence baada ya kubanwa kwa mabao 2-2 yaliyofungwa na Jacob Massawe na Kelvin Sabato huku ya Gipco yakifungwa na Nicodemas Justin na Nelson Richard.

COSMOPOLITAN 3-3 PAN AFRICAN

Moja ya mchezo uliokuwa wa kuvutia tangu ligi ianze ni huu wa vijana kutoka Jiji la Dar es Salaam walipoonyeshana umwamba katika mechi ya mzunguko wa tatu na kutoshana nguvu.

Mshambuliaji wa Cosmopolitan FC, Karim Salehe aliandika hat trick ya kwanza ya FDL, huku mabao ya Pan African yakikwamishwa kambani na Alex Peter, Ayoub Mohamed na Hamis Punje.

DODOMA 1-0 IHEFU FC

Vita yao bado haijaisha na kinachosubiriwa kuona nani ataendelea kubaki kwenye nafasi yake. Timu hizo zimepishana mabao manne ya kufunga pekee kwani wote wamefungwa mabao 10 na alama zao 39.

Katika mchezo huu Dodoma ikiwa nyumbani ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Rajabu Seif na katika mchezo wa marudiano Uwanja wa Highland Estates, Dodoma ikafa 1-0 kwa bao la Abdi Kassim ‘Mwape’.

SAHARE 2-0 GWAMBINA

Ulikuwa mchezo wa mzunguko wa tano baada ya kuanza vyema ligi Gwambina ikishinda michezo miwili ya kwanza, ilianza kuona machungu kwa vichapo.

Kwanza ililazimishwa sare na Gipco ya 2-2 nyumbani, ikachwapa 1-0 na Geita Gold na katika mchezo huu pale Mkwakwani mjini Tanga mbele ya Sahare All Stars ikalala 2-0 kwa mabao ya Kassim Shaban na Hussein Amir.

MAWENZI MARKET 4-0 PAMBA FC

Ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Kocha Fred Felix ‘Minziro’ akipokea mikoba ya Muhibu Kanu aliyetimkia Boma FC.

Pamba ilipigwa 4-0 kwa mabao ya Hashim Salum, Seleman Mwalim akipiga mbili na Offen Francis akipiga moja, ukiwa mchezo wa tatu Pamba kupoteza baada ya kulala 2-0 kwa Gipco na 1-0 kwa Geita.

MBEYA KWANZA 5-1 IRINGA UTD

Enock Jiah wa Mbeya Kwanza alipiga hat trick katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Kayala Mbuta na Elam Mwakabungu kila mmoja akifunga bao moja huku, Juma Mpeka akifunga kwa Iringa United.

Hata hivyo Iringa United licha ya kuburuza mkia kwa muda mrefu kwenye Kundi A iliifanyia kitu mbaya vijana hao kutoka Mbeya katika mchezo wa maruadiano kwa kuichapa mabao 2-1 mchezo ambao ulikuwa muhimu kwa Mbeya kuendelea kufufua matuamaini ya kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

DODOMA FC 1-1 MAJIMAJI FC

Lilikuwa bonge la bato, kwa timu hizo zinazopewa nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao na walipokutana hakukuwa na mbabe baada ya mabao ya Anuary Jabir (Dodoma) na Razack Omary wa Majimaji FC.

Timu hizo zinataraji kukutana tena kwenye mzunguko wa 20 mkoani Ruvuma wakati Dodoma ikihitaji alama tatu za kuzidi kukaa kileleni, Majimaji inakazi ya kuhakikisha inapunguza pengo kwa waliokaa juu yake.

MAJIMAJI 3-1 IHEFU FC

Moja ya mchezo uliochangia kufukuzwa aliyekuwa kocha mkuu wa Ihefu FC, Salhina Mjengwa ni pamoja na kichapo cha mchezo huu wa mzunguko wa lala salama na baadaye ikalala 1-0 kwa Njombe Mji.

Vichapo hivyo viliifanya Ihefu FC ianze kupoteza muelekeo wa kukaa kileleni kwa muda mrefu na kumpa nafasi Dodoma kuongoza usukani, kwa sasa inanolewa na Maka Malwisi.

AFRICAN LYON 6-0 PAN AFRICAN

Mchezo huu ndio umefanya timu iliyofunga mabao mengi katika mchezo mmoja huku nyavu zao kutoguswa na wapinzani.

Mabao ya Lyon yaliwekwa kambani na Mwaramy Mwaramy aliyefunga mabao mawili, Mussa Gadi, Samy Sultan Kasikasi na Jaruf Rajabu kila mmoja akitupia moja kambani.