Hizi ndio mechi zilizobakia za ubingwa Simba, Yanga

Muktasari:

  • Aussems alisema ratiba ngumu waliyokutana nayo ya kucheza mechi kila baada ya siku mbili, huku wakiwa wanasafiri wanakosa muda wa kufanya mazoezi ni mambo yaliyosababisha kutofanya vizuri mechi zao mbili mfululizo.

MATOKEO ya mechi mbili zilizopita za Simba baada ya kufungwa dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0, na kutoka suluhu dhidi ya matajiri wa Ligi Kuu Bara ni kama yamewashtua mashabiki wa timu hiyo kuelekea mwisho wa msimu huku wakiwa na malengo ya kutwaa ubingwa kwa mara ya pili.

Simba baada ya matokeo hayo wamefikisha pointi 82, huku wakiwa wamebakiwa na michezo mitano huku mitatu wakiwa wanacheza nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar, Ndanda na Biashara United, lakini watacheza miwili ugenini dhidi ya Singida United na Mtibwa Sugar ambao ndio utakuwa mchezo wa mwisho wa kufunga ligi.

Ili Simba waweze kuwa mabingwa msimu huu wanatakiwa kuvuna pointi nane katika mechi zake tano zilizobaki ambazo atafikisha pointi 90, na kuziacha Yanga waliokuwa katika nafasi ya pili na Azam nafasi ya tatu hakuna timu ambayo itaweza kumfikia.

Simba kama watashindwa kupata pointi nane katika mechi zao zilizobaki wataongeza vita ya ushindani katika mbio za kuwania ubingwa kati yake na Yanga waliokuwa nafasi ya pili wakiwa na pointi zao 80, kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Ruvu Shooting ambao ulichezwa Uwanja wa Uhuru.

Yanga kama watamaliza kwa kushinda mechi zao zote tatu zilizobaki ambazo zote atacheza Uwanja wa Uhuru dhidi ya Ruvu Shooting ambao walicheza nao jana, Azam na Mbeya City watamaliza msimu wakiwa na pointi 89, huku wakiomba matokeo mabaya katika mechi tano za watani wa Simba.

Kocha wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems alisema mashabiki wa wapenzi wote wa timu hiyo waondoe wasiwasi wowote waliokuwa nao kulingana na matokeo waliyoyapata katika mechi mbili zilizopita na watapata matokeo mazuri katika mechi tano zilizobaki na kutwaa ubingwa msimu huu kama malengo yao yalivyo.

Aussems alisema ratiba ngumu waliyokutana nayo ya kucheza mechi kila baada ya siku mbili huku wakiwa wanasafiri wanakosa muda wa kufanya mazoezi ila ambacho anafanya ni kuwaacha wachezaji ili kupata muda mwingi wa kupumzika, kwani hawana muda wa kufanya mazoezi na marekebisho kulingana na mchezo uliopita.

Alisema mbali ya hilo wamekutana na changamoto nyingine ya wachezaji wake wake ambao anawatumia kuwa katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani, lakini kama mazingira ya Uwanja ambayo wanatumia huwa vinaathirika na mvua ambazo zinaendelea kunyesha na muda mwingine kushindwa kucheza vizuri.

"Sioni nafasi ya kushindwa kupata pointi nane katika mechi tano ambazo zimebaki tuna kila sababu na uwezo wa kufanya hivyo jambo ambalo niwatoa hufu kuwa Simba msimu huu ndio mabingwa watarajiwa licha ya changamoto zote hizo ambalo tunakabiliana nazo," alisema Aussems.

Kocha wa Yanga Mkongomani Mwinyi Zahera alisema kuhusu mbio za ubingwa hilo halipo ndani ya uwezo wao kwani kuna mechi mbazo walifungwa na wakashindwa kupata pointi tatu si makosa ya timu bali ni kwa mapungufu ya waamuzi ambao walishindwa kuwa sahihi.

"Tumepoteza mechi ambazo tulinyimwa penati za wazi, tulinyimwa magoli ya wazi na kufungwa magoli ambayo mengine hayakuwa sahihi jambo ambalo lilifanya kukosa pointi ambazo muda huu tungekuwa tupo katika mbio za kuwania ubingwa," alisema Zahera na kusisitiza wanataka kushinda mechi zao zilizobaki ili kumalizika katika timu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba na Mtibwa Sugar

Simba na Ndanda

Singida na Simba

Simba na Biashara

Mtibwa na Simba

 

Yanga na Ruvu Shooting

Azam na Yanga

Yanga na Mbeya City