Hizi ndio hat trick 14 za Aguero Manchester City

Muktasari:

  • Kwa kufanya hivyo anafikisha Hat trick 11 katika Ligi Kuu ya England na kumfikia mkongwe, Alan Shearer kuongoza kwa kufunga Hat trick katika Ligi Kuu ya England. Lakini kwa ujumla Aguero ana Hat trick 13 katika maisha yake Manchester City

MANCHESTER, ENGLAND.MTU anayeitwa Sergio Kun Aguero anatisha. Ndani ya wiki moja amezipiga Hat trick Arsenal na Chelsea.

Kwa kufanya hivyo anafikisha Hat trick 11 katika Ligi Kuu ya England na kumfikia mkongwe, Alan Shearer kuongoza kwa kufunga Hat trick katika Ligi Kuu ya England. Lakini kwa ujumla Aguero ana Hat trick 13 katika maisha yake Manchester City

Aguero vs Wigan Athletic (Septemba 2011)

Hii ilikuwa Hat trick yake ya kwanza katika jezi ya Manchester City msimu wa kwanza tu. kwa kutumia juhusi binafsi yeye mwenyewe aliiharibu Wigan katika uwanja wa nyumbani Etihad. kuna alifunga bao la kwanza katika dakika ya 13, akafunga mengine katika dakika za 63 na 69. Mabao haya alifunga ndani ya dakika 54 tu huku City wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Aguero vs Watford

(Januari 2014)

Aguero alilazimika ikusubiri kwa miaka miwili kufunga Hat trick yake ya pili. Ilikuja Januari 2014 katika pambano muhimu dhidi ya Watford huku City ikiwa imeshalala 2-0. Alitumia dakika 31 tu kuiharibu Watford. Mabao yote yalikuja kipindi cha pili katika dakika za 59, 78 na 90. City waliondoka uwanjani na ushindi wa mabao 4-2.

Aguero vs Tottenham (Oktoba 2014)

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Aguero kutupia mabao manne ndani ya mechi moja akiwa katika jezi ya Manchester City. Alitumia dakika 63 kupiga Hat trick lakini zaidi ni kwa msaada wa penalti mbili huku akikosa moja. Akafunga mengine mawili katika njia ya kawaida na hivyo kufikisha Hat trick ya tatu katika jezi ya City.

Aguero vs Bayern Munich (Novemba 2014)

Inashangaza sana. Aguero alilazimika kusubiri miaka miwili kupiga hat trick yake ya pili lakini hapa ndani ya Mwezi mmoja alikuwa amepiga Hat trick ya tatu na ya nne. Dhidi ya kikosi jeuri cha Bayern Munich kilichokuwa kinaongozwa na kocha wake wa sasa, Pep Guardiola, Aguero alionyesha moja kati ya viwango bora zaidi katika jezi ya City. Alifunga bao la kuongoza kwa penalti mapema lakini Bayern Munich wakapiga mabao mawili kabla ya kwenda mapumzikoni. Zikiwa zimesalia dakika tano mechi hiyo kumalizika Aguero alifunga mabao mawili na kuipatia City ushindi maarufu wa mabao 3-2 Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Katika mechi hii alitumia dakika 61 kufunga hat trick yake.

Aguero vs QPR (Mei 2015)

Kama Hat trick iliyopita, na hii Aguero alitumia dakika 61 tu kuiteketeza QPR. Tayari QPR walikuwa wameshashuka daraja lakini Aguero akaamua kuwasindikiza vizuri zaidi. Alifunga bao la kwanza katika dakika ya nne tu kabla ya kuongeza jingine katika dakika ya 10 na kisha dakika ya 65 akakamilisha hat trick yake kwa penalti. City waliondoka uwanjani na ushindi wa mabao 6-0.

Aguero vs Newcastle

(Oktoba 2015)

Hii ilikuwa Hat trick yake ya mapema zaidi lakini pia ilikuwa mechi yake ya kwanza kufunga mabao matano akiwa katika jezi ya Manchester City. Vibonde wa safari hii walikuwa Newcastle United na Aguero alitumia dakika 20 tu kufunga mabao hayo matano. Newcastle ndio walianza kwa mbwembwe kwa kufunga bao la kuongoza lakini Aguero akawashindilia mabao matano katika dakika za 42, 49, 50, 60 na 62. Hii ina maana dakika 20 alitumia kwa kufunga mabao yote matano, lakini tayari alishapiga hat trick kwa kutumia dakika nane tu.

Aguero vs Chelsea (April 2016)

Kama unadhani Hat trick ya Aguero juzi dhidi ya Chelsea ilikuwa ya kwanza basi unakosea. Tayari alishafanya hivyo mwaka 2016. Hii pia ilikuwa hat trick yake ya kwanza ugenini huku City wakiiharibu vibaya Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani. Alitumia dakika 47 tu kupiga Hat trick hii katika dakika za 33, 54 na 80.

Aguero vs Steaua (Agosti 2016)

Hii ilikuwa mechi ya mtoano kwa ajili ya kufuzu kwenda hatua za makundi baada ya City kushika nafasi ya nne katika Ligi. Aguero alihakikisha kwamba mechi ya pili ya marudiano inakuwa ya kutimiza muda tu baada ya kuiharibu Steaua ugenini. Alifunga mabao hayo katika dakika za 41,78 na 90. Kifupi alitumia dakika 49 tu kupiga hat trick hiyo katika ushindi wa 5-0.

Aguero vs Monchengladbach

(Septemba 2016)

Hat trick ya pili ndani ya mwezi mmoja katika ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Alitumia dakika 69 tu kukamilisha Hat trick akianzia kwa bao la kwanza dakika ya nane kabla ya kufunga bao la pili dakika ya 28 akitumia vema mkwaju wa penalti kabla ya kufunga kazi katika dakika ya 77.

Aguero vs Watford (Septemba 2017)

Hii ilikuwa Hat trick ya kwanza ambayo Aguero alitumia kichwa, mguu wa kushoto na mguu wa kulia kufunga. Lakini pia ilikuwa hat trick yake ya pili ugenini katika Ligi Kuu ya England huku ikiwa ya tatu kwa ujumla ugenini. Alifunga katika dakika ya 27, 31, na 81.

Aguero vs Newcastle

(Januari 2018)

Hat trick yake ya pili dhidi ya timu moja. Newcastle lazima wanaumwa wakimuona Aguero uwanjani. Hat trick hii pia alitumia kichwa, mguu wa kushoto na mguu wa kulia. Alifunga katika dakika ya 34, 63 na 83 kukamilisha mabao yake. Alitumia dakika 49 tu huku City wakiondoka uwanjani na ushindi wa mabao 3-1. Msimu huu Aguero ameifunga Newcastle bao moja na hilo linakuwa bao lake la 15 katika mechi 13 dhidi yao.

Aguero vs Huddersfield (Agosti 19, 2019)

Katika pambano hili ambalo City walishinda mabao 6-1 hii ilikuwa hat trick yake ya kwanza Aguero msimu huu. vibonde Huddersfield walijipendekeza kwake katika uwanja wa Etihad na Aguero aliosha nyota akitumia dakika 50 kupiga hat trick hii. Alifunga mabao katika dakika ya 25, 35 na 75.

Aguero vs Arsenal

(Februari 3, 2019)

Wiki moja kabla ya Chelsea haijateketea kwa City juzi, tayaroi Aguero alikuwa amepiga Hat trick yake ya kwanza msimu huu huku ikiwa ni hat trick yake ya 10 katika Ligi kuu ya England. katika mechi hii dhidi ya Arsenal alianza biashara mapema kwa kufunga katika dakika ya kwanza tu. akafunga bao la pili katika dakika ya 44 huku akifunga kazi kwa kupiga jingine dakika ya 61. Hata hivyo baadaye alikiri kwamba bao la tatu alifunga kwa mkono

Aguero vs Chelsea

(Februari 10, 2019)

Hii ni hat trick yake ambayo ilimfanya afikie rekodi ya mkongwe Alan Shearer ya kufunga hat trick nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya England. katika pambano la juzi ambalo City walishinda 6-0, Aguero alitumia dakika 43 tu kuiteketeza vibaya Chelsea. Alifunga mabao yake katika dakika za 13, 19 na 56.