Hizi ndio haki za wanachama Simba

Tuesday September 11 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

JANA Jumatatu tuliona jinsi ambavyo mwanachama wa Simba anavyoweza kuchukuliwa hatua endapo atapeleka masuala ya michezo hususan soka mahakamani. Pia, Katiba hiyo inaeleza namna ambavyo mwanachama anaweza kuwajibishwa kwa kwenda kinyume na kanuni ikiwa ni pamoja na kuvuliwa uanachama ndani ya Simba Sports Cllub Company Limited. Leo Jumanne tunaendelea na uchambuzi wa Katiba Mpya ya Simba ambayo inaelezea, jinsi muundo mzima wa klabu utakavyokuwa na taratibu zake.

Klabu ya Simba katika mfumo mpya wa uendeshaji utakuwa na muundo mpya, ambapo kila mjumbe ama mwanachama anapaswa kufahamu majukumu yake na mipaka katika utendaji kazi, ambao ndio mwongozo wao.

Katika mwendelezo wa uchambuzi wa katiba hiyo, Mwanaspoti linazidi kukuletea kwa karibu muundo mzima wa klabu ya Simba utakavyokuwa, pitia katiba hii.

SEHEMU YA III: MUUNDO

Hapa ndio roho ya katiba ilipo, ambapo inaelezea muundo mzima wa klabu kwa kufuata katiba yao, ina Ibara 24 kuanzia Ibara ya 17 hadi 40.

IBARA YA 17: ORODHA YA VYOMBO VYA UTENDAJI

1. Simba Sports Club itakuwa na vyombo vya utendaji vifuatavyo

(a). Mkutano Mkuu

(b). Bodi ya Wakurugenzi

(c). Sekretarieti

(d). Vyombo vya Haki

(f). Baraza la Wadhamini

(g). Matawi, Uongozi wa Wilaya na Mikoa ya Simba Sports Club nchi nzima

A. MKUTANO MKUU

Ibara ya 18: Ufafanuzi na Muundo

1. Mkutano Mkuu ni mkutano ambao wanachama wote wa Simba Sports Club wanakutana. Mkutano Mkuu ulioitishwa kwa kufuata utaratibu ndio wenywe mamlaka ya kufanya maamuzi.

2. Hali kadhalika, watakaoitwa katika Mkutano Mkuu kama washauri ni wajumbe waalikwa walioteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi.

3. Bodi ya Wakurugenzi itaamua kuhusu ushiriki wa wasiokuwa wanachama watakaohesabiwa kuwa ni washiriki waalikwa (third parties) katika Mkutano Mkuu. Hata hivyo, hawatakuwa na haki ya kupiga kura, ingawa wataombwa ushauri kwa idhini ya Mweyekiti wa Mkutano.

Ibara ya 19. Idadi na mgawanyo wa wajumbe Mkutano Mkuu utakuwa na Mamlaka yafuatayo:

1. Kupitisha au kurekebisha katiba na kanuni na kusimamia matumizi yake.

2. Kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliopita.

3. Kupokea bajeti ya mwaka ya shughuli na mipango ya Simba Sports Cluba na Simba Sports Club Company Limited.

4. Kupokea taarifa ya chombo cha ukaguzi wa fedha cha Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

5. Kupokea taarifa ya shughuli za Bodi ya Wakurugenzi.

6. Kila miaka minne(4), kuchagua viongozi.

Ibara ya 20: Mamlaka ya Mkutano Mkuu Mkutano Mkuu utakuwa na Mamlaka yafuatayo:

1. Kupitisha au kurekebisha katiba na kanuni na kusimamia matumizi yake.

2. Kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliopita.

3. kupokea bajeti ya shughuli na mipango ya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

4. Kupokea taarifa ya chombo cha ukaguzi wa fedha cha Simba Sports Club Company Limited.

5. Kila miaka miaka minne (4), kuchagua viongozi.

Ibara ya 21: Mkutano Mkuu wa Kawaida

1. Mkutano Mkuu wa kawaida utaitishwa na Bodi ya Wakuregenzi mara moja kwa mwaka, yaani ndani ya siku 120 baada ya mwaka wa fedha. Mwaliko wa mkutano huo lazima upelekwe kwa wanachama angalau siku 30 kabla ya mkutano huo.

Mwaliko huu utatolewa kupitia vyombo vya habari, ofisi za matawi na kwenye ubao wa ofisi za makao makuu ya klabu. Hesabu za mwaka wa fedha uliotangulia zitawasilishwa katika mkutano wa mwaka wa wanachama wote.

2. Agenda ya mkutano itataja mahali, tarehe na muda utakaopangwa na Bodi ya Wakurugenzi. Agenda, taarifa za kazi, bajeti, taarifa za hesabu na nyaraka nyingine zinazohusika zitapelekwa kwa wanachama angalau siku saba (7) kabla ya mkutano kupitia anuani za matawi yao. Kila mwanachama atakuwa na haki ya kuomba dondoo liingizwe katika ajenda ilimradi sekretarieti ya Simba Sports Club inapokea ombi hili angalau siku 21 kabla ya mkutano.

Ibara ya 22: Ajenda ya Mkutano Mkuu wa kawaida.

Ajenda ya Mkutano Mkuu wa kawaida itajumuisha mambo yafuatayo ya kikatiba;

Itaendelea Alhamisi.

(a). Kuhakiki idadi ya wanachama wanaohudhuria mkutano

(b). Kuthibitisha ajenda

(c). Kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliopita

(d) Yatokanayo na kumbukumbu za mkutano uliopita

(d). Hotuba ya Mwenyekiti

(f). Kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kutoka Bodi ya Wakurugenzi.

(g). Kupokea taarifa ya hesabu za fedha zilizokaguliwa za mwaka uliotangulia za Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(h). Kupokea bajeti ya mwaka ya shughuli na mipango ya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(i) Uchaguzi wa nafasi zozote zilizo wazi za Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

(j). Kupokea na kujadili mapendekezo ya marekebisho ya kanuni na katiba za Simba Sports Club.

(k) Kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na wanachama au Bodi ya Wakurugenzi.

Ibara ya 23: Mkutano Mkuu wa Dharura

1. Bodi ya Wakurugenzi inaweza kuitisha mkutano mkuu wa dharura kama itaona inafaa.

2. Endapo wanachama hai wasiopungua 1,000 watajiorodhesha na kuwasilisha kimaandishi ombi kwa Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki wa Simba Sports Club, Bodi ya Wakurugenzi itawajibika kuitisha mkutano mkuu wa dharura katika kipindi kisichozidi siku 30 baada ya kupokelewa kwa ombi.

3. Wito wa mkutano mkuu wa dharura hauna budi kupelekwa kwa wanachama kupitia matawi yao angalau siku 15 kabla ya mkutano.

4. Ajenda na nyaraka nyingine muhimu zitapelekwa kwa wanachama kupitia kwenye matawi angalau siku saba kabla ya mkutano.

5. Endapo Mkutano Mkuu wa dharura utaitishwa kwa juhudi za Bodi ya Wakurugenzi, basi Bodi ya Wakurugenzi itaandaa ajenda. Endapo utaitishwa kwa ombi la wanachama 1,000, ajenda itakuwa na masuala yaliyopendekezwa na wanachama hao.

Ibara ya 24. Akidi

1. Maamuzi ya Mkutano Mkuu yatakuwa halali wakati watakapopitishwa kwa wingi wa kura (50%+1) za wanachama waliohudhuria wenye haki ya kupiga kura, bila kuathiri aya ya 2 ya Ibara hii. Mkutano MKuu utakuwa ni halali endapo idadi hiyo ya wanachama wasiopungua 500. Endapo idadi hiyo ya wanachama haitafikiwa basi mkutano mkuu utaendelea siku inayofuata hata kama idadi ya wanachama haitofikia mia tano.

2. Iwapo akidi haikutimia, Mkutano mkuu utafanyika siku inayofuata kwa agenda zile zile. Katika mkutano huo hakutahitajika akidi, isipokuwa kama kuna ajenda ya marekebisho ya Katiba ya Simba Sports Club, uteuzi wa watendaji, kufukuzwa kwa mjumbe mmoja au wengi katika chombo cha Simba Sports Club.

Ibara ya 25: Uendeshaji wa Mkutano Mkuu

1. Mkutano Mkuu utaendeshwa na Mwenyekiti aliyechaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 27 (1) (a) ya Katiba hii, Mwenyekiti asipokuwepo Bodi ya Wakurugenzi itachagua mjumbe mmoja kati ya wajumbe sita wa Bodi ya Wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 27 (1) (a) - (b) kuwa Mwenyekiti wa Mkutano.

2. Mkutano unaweza kuteua idadi ya kutosha ya waangalizi.

3. Wanachama watazungumza katika mkutano kwa kutumia lugha rasmi ya Simba Sports Club.

4. Mwenyekiti atakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mkutano unaendeshwa kama ulivyopangwa. Kwa hali hiyo, Mwenyekiti atakuwa anayo haki ya kukatiza hotuba za wanachama.

5. Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki atatayarisha kumbukumbu za mkutano na kuwapelekea wanachama kupitia matawi yao katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya mkutano.

Ibara ya 26: Maamuzi na uchaguzi

1. Mkutano MKuu hautatoa uamuzi kwa suala lolote lisilokuwamo katika ajenda.

2. Kila mwanachama rasmi atakuwa na kura moja na hatawakilisha zaidi ya mjumbe mmoja.

3. Uchaguzi utafanywa kwa kura ya siri

4. Isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika Katiba, maamuzi ya Mkutano Mkuu yatafanywa kwa wingi wa kura zilizopigwa na wanachama rasmi.

5. Maamuzi ya marekebisho yoyote ya ajenda katika Katiba na Kanuni, Mabadiliko yoyote ya ajenda ya Mkutano Mkuu wa kawaida yatahitaji theluthi mbili ya kura halali zilizopigwa na wanachama waliohudhuria na kutimiza akidi ya mkutano husika.

6. Karatasi za kura zilizoharibika, karatasi za kura zisizotumika, au aina nyingine zozote za kutokupigia kura hazitoingizwa katika hesabu ya kura halali zilizopigwa.

7. Uchaguzi wa wajumbe watakaoiwakilisha Simba Sports Club kwenye bodi ya wakurugenzi utafanywa na kuamriwa kwa wingi wa kura wa wanachama waliohudhuria wenye haki ya kupiga kura.

8. Mkutano Mkuu wa uchaguzi utachagua wajumbe sita watakaoiwakilisha Simba Sports Club katika Bodi ya Wakurugenzi, nafasi moja wapo angalau awe ni mjumbe mwanamke.

9. Maamuzi mengine yote ya wanachama yatafanywa kwa kunyoosha mikono. Uchaguzi utaendeshwa kwa utaratibu wa kura ya siri kwa kutumia karatasi zilizotayarishwa kwa maelekezo ya Kamati ya Uchaguzi.

10. Kupiga kura kwa uwakilishi au barua hauruhusiwi.

11. Uamuzi unaofanywa na Mkutano Mkuu utaanza kutumika mara moja isipokuwa kama mkutano unapanga tarehe nyingine au kuiachia uamuzi huo Kamati ya Uchaguzi.

12. Uchaguzi MKuu utafanyika kila baada ya miaka minne kufuata na vipindi vya uongozi kwa kugombea kwa vipindi vya miaka minne minne.

Ibara ya 27: Sifa za Wagombea

1. Kutakuwa na wajumbe nane watakaoiwakilisha Simba Sports Club katika Bodi ya wakurugenzi; sita (6) wa kuchaguliwa na wawili (2) wa kuteuliwa ambao kati yao;

(a). Mjumbe mmoja atachaguliwa kama Mwenyekiti na ni lazima awe na taaluma kiwnago cha chini elimu ya angalau Shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

(b). Mjumbe mmoja (1) lazima awe na taaluma kiwango cha chini cha elimu ya angalau shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania.

(c). Wajumbe wengine wanne wa kuchaguliwa waliobaki wanatakiwa kuwa na elimu isiyopungua kidato cha nne na angalau mjumbe mmoja wapo kati yao awe mwanamke.

(d). Wajumbe wawili watateuliwa na Mwenyekiti kutoka miongoni mwa wanachama ambao ni lazima wawe na taaluma ya angalau kidato cha nne.

2. Mtu yeyote anayegombea nafasi yeyote ya Simba Sports Club hana budi kutimiza masharti yafuatayo;

i. Awe na sifa zinzotakiwa kwa nafasi husika na amelipa ada ya uanachama kikamilifu tangu alipoanza uanachama.

ii. Awe na kiwango cha chini cha elimu kama ilivyoanishwa katika ibara ya 27 (1) (a) (b) na (c.

iii. KIongozi wa kuchaguliwa atakaa madarakani kwa vipindi viwili tu vya kupiga kura kwa nafasi ya uongozi. Endapo atataka kurejea madarakani baada ya kutumikia vipindi viiwli mfululizo, itabidi asubiri kwanza kupita kwa walau uchagiz mkuu mmoja wa kikatiba.

iv. Asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kwa kuhukumiwa kifungo.

v. Awe na umri angalau miaka 25

vi. Awe ametimiza angalau miaka mitatu ya uanachama

vii. Asiwe mwamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu anayefanya shughuli za uamuzi kwa kipindi hicho.

viii. Mwanachama mwenye umri wa miaka 65 na kuendelea hataruhusiwa kugombea.

Ibara ya 28: Marekebisho ya Katiba na Kanuni

1. Mkutano Mkuu una jukumu la kurebisha Katiba na kanuni kuu za mkutano mkuu.

2. Pendekezo lolote la marekebisho ya Katiba halina budi kuwasilishwa na mwanachama/wanachama ni halali, alimradi limeungwa mkono kwa maandishi na angalau wanachama wengine mia moja na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki siku 21 kabla ya mkutano mkuu.

3. Kwa kura inayohusu marekebisho ya katiba kuwa halali, lazima wanachama halali wanaostaili kupiga kura wawe zaidi ya nusu (50%+1).

4. Pendekezo la maerekebisho ya katiba litapitishwa endapo 2/3 ya wanachama wenye haki ya kupiga kura watakaopiga kura na watakubaliana nalo.

5. Pendekezo la marekebisho ya kanuni zinzohusu matumizi ya katiba na kanuni kuu za mkutano, lazima ziwasilishwe kwa manadishi kwa sekretarieti siku 21 kabla ya mkutano.

6. Pendekezo la marekebisho ya matumizi ya katiba na kanuni kuu za mkutano mkuu litapitishwa tu iwapo zaidi ya nusu (50%+1) ya wanachama waliohudhuria na wanaostahili kupiga kura watakubaliana nalo.

B. BODI YA WAKURUGENZI

Ibara ya 29: Muundo

1. Klabu ya Simba itafanya kazi chini ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Sports Club Company Limited.

2. Wajumbe saba waliochaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 watakuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi na watafanya kazi kwa mujibu wa kanuni zinzoongoza bodi ya wakurugenzi zilizoidhinishwa na Simba Sprts Cluba Company Limited.

3. Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi hawezi kuwa wakati huo huo mjumbe wa chombo cha haki cha klabu ya Simba au Kamati ya Uchaguzi.

4. Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi aliyechaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 ya katiba hii atakoma kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi iwapo atatenda au kufanya mojawapo ya mambo yafuatayo;

(a). Kujiuzulu kwa maandishi na kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa bodi ya wkaurugenzi

(b). Hatahudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya Bodi ya Wakurugenzi bila sababu za msingi.

(c). Anashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo.

(d). Kufariki.

Ibara ya 30. Muda wa madaraka wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi

1. Muda wa madaraka na mamlaka wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 ya katiba hii utakuwa miaka minene. Kamati ya muda (Interim Committes) hazitaruhusiwa.

2. Mamlaka ya wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi yanaweza kuongezwa muda na mkutano mkuu kwa sababu maalumu za msingi.

3. Endapo itatokea kuwa nafasi, yoyote ya bodi ya wakurugenzi kuwa wazi, katika mkutano mkuu wa kawaida unaofuata nafasi hizo zitajazwa kwa kuchaguliwa wajumbe wengine kwa kipindi kilichobaki cha mamlaka.

C. SEKRETARIETI

Ibara ya 31: Uanzishaji, Miundombinu na Kazi

1. Kutakuwa na sekretarieti yenye muundo wa ajira wa Simba Sports Club.

2. Wafanyakzi wote wa Sekretarieti watakuwa wa kuajiriwa na wataajiriwa na Bodi ya Wakurugenzi.

3. Sekretarieti itaundwa na

(a). Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki

(b). Nafasi nyingine kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Wakurugenzi

4. Sekretarieti itaongozwa na Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki na kazi zake mahususi ni;

(a) Utekezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu, bodi ya wakurugenzi na vyombo vingine vya Simba Sports Club Company Limited.

(b). Kufanya matayarisho ya mkutano mkuu.

(c). Kutayarisha kumbukumbu za mkutano mkuu

(d). Kuhakikisha usimamizi mzuri na utunzaji wa rasimali za Simba Sports Club.

(e). Kushughulikia mawasiliano ya Simba Sports Club na kusimamia ofisi za Simba Sports Club.

(f). Kutunza vitabu vya hesabu za Fedha za Simba Sports Club.

(g). Kushughulia mahusiano ya Simba Sports Club, wanachama wake na wadau wengine.

Ibara ya 32: Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki

Kutakuwa na Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki Simba Sports Club atakayesimamia sekretarieti ya Simba Sports Club.

1. Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki atafanya kazi chini ya usimamizi na muongozo wa Mtendaji mkuu wa Simba Sports Club Company Limited.

2. Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki atakuwa mwandishi wa mkutano mkuu na kuzihifadhi kumbukumbu hizo.

3. Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki atawasimamia wafanyakazi wa Simba Sports Club na Utendaji wa sekretarieti.

4. Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki atakuwa Ofisa Masuhuli wa klabu.

5. Mkurugenzi wa wanachama na mashabiki atapokea mipango na bajeti za kila mwaka kutoka Simba Sports Club Company Limited na kusimamia utekelezaji wake.

D. VYOMBO VYA HAKI

Ibara ya 33: Dhana

1. Simba Sports Club itatumia vyombo vya haki vya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited.

2. Vyombo vya haki vitakuwa ni Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Maadili. Vyombo hivi vitakuwa huru na maamuzi yake hayatangiliwa na chombo chochote cha Simba Sports Club.

3. Bila kuathiri maeneo ya mamlaka yaliyoandaliwa na mkutano mkuu, vyombo vilivyotajwa hapo juu vinaidhinishwa kuchukuwa hatua mbalimbali za nidhamu na maadili zilziotajwa katika katiba hii na kanuni zinazohusika.

4. Muundo, maeneo ya mamlaka, na kazi za vyombo vya haki, vitakuwa kwa mujibu wa kanuni mahususi ambazo lazima ziidhinishwe na Bodi ya Wakurugenzi.

5. Wajumbe wa vyombo vya haki watateuliwa na Bodi ya Wakurugenzi.

Ibara ya 34: Hatua za Kinidhamu

1. Onyo

2. Karipio

3. Kurudisha tuzo

4. Kusimamishwa

5. Kufukuzwa

6. Bodi ya Wakurugenzi itaandaa kanuni za nidhamu na za maadili pasipokuwa na kanuni za nidhamu na za maadili za Simba Sports Club Company Limited, Kanuni za nidhamu na za maadili za TFF au FIFA zitatumika.

Ibara ya 35: Kamati ya Nidhamu

1. Simba Sports Club inatambua Kamati ya Nidhamu ya Simba Sports Club Company Limited, itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe watatu watakaoteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti lazima wawe na Taaluma ya Sheria.

2. Chombo hiki kitasimamia Katiba ya Simba Sports Club kwa kutumia kanuni zake za Nidhamu au kanuni za TFF pale ambapo kanuni za Nidhamu za Simba Sports Club Company Limited hazipo.

3. Kamati itapitisha uamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmojawapo akiwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti.

4. Kamati inaweza kutangaza hatua za kinidhamu zilivyoelezwa katika katiba hii au kanuni zilizotayarishwa kutokana na Katiba hii dhidi ya wanachama, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 26(8) au wafanyakazi wa Simba Sports Club.

5. Rufaa yoyote dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya Simba Sports Club Company Limited, itapelekwa kwa kamati ya rufaa ya nidhamu ya TFF. Rufaa dhidi ya maamuzi ya TFF yanaweza pia kukatiwa rufaa CAS ambayo itakuwa na maamuzi ya mwisho.

Ibara ya 36: Kamati ya Maadili

1. Simba Sports Club inatambua Kamati ya Maadili ya Simba Sports Club Company Limited, itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe watatu watakaoteuliwa na Bodi ya Maadili lazima wawe na taalumu ya sheria.

2. Chombo hiki kitasimamia Katiba ya Simba Sports Club kwa kutumia Kanuni zake za Maadili au Kanuni za TFF pale ambapo kanuni za Maadili za Simba Sports Club Company Limited hazipo.

3. Kamati itapitisha uamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmojawapo akiwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti.

4. Kamati inaweza kutangaza hatua za kimaadili zilivyoelezwa katika Katiba hii au kanuni zilizotayarishwa kutokana na katiba hii dhidi ya wanachama, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa kwa mujibu wa ibara ya 26 (8) au wafanyakazi wa Simba Sports Cluba.

5. Rufaa yoyote dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Simba Sports Cluba Company Limited itapelekwa kwa Kamati ya rufaa uya Maadili ya TFF. Rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Rufaa ya Maadoli ya TFF yanaweza pia kukatiwa rufaa CAS ambayo itakuwa na maamuzi ya mwisho.

E. KAMATI YA UCHAGUZI

Ibara ya 37: Uanzishaji, Kazi na Majukumu

1. Kutakuwa na Kamati ya Uchaguzi wa Simba Sports Club itakayoteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ambayo itahusika na kuandaa na kusimamia uchaguzi wa Simba Sports Club, itashauri bodi ya wakurugenzi kuhusiana na kanuni za uchaguzi. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club itafanya kazi chini ya usimamizi na maelekezo ya Kamati ya uchaguzi ya TFF.

2. Kamati ya cuhaguzi itaundwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe watatu. Mwenyekiti na Makamu wa Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi lazima wawe na taaluma ya sheria.

3. Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club itatekeleza majukumu yake kwa kutumia kanuni za uchaguzi za Simba Sports Club na kama hazipo kanuni za uchaguzi za TFF zitatumika.

4. Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club itapitisha maamuzi iwapo angalau wajumbe watatu wamehudhuria mmoja wao akiwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti.

5. Maamuzi ya Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club yanaweza kukatiwa rufaa kwa kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF ambayo maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.

F. BARAZA LA WADHAMINI

Ibara ya 38: Muundo wa mamlaka

1. Simba Sports Club itakuwa na Baraza la Wadhamini litakalokuwa na wajumbe wanne na ndiyo watakuwa wasimamizi na wadhibiti wa mali zote za klabu zinzohamishika na zisizohamishika na watunzaji wa ‘lakiri’ (seal) ya klabu.

2. Wajumbe wa Baraza la Wadhamini watateuliwa na Bodi ya Wakurugenzi na kuthibitishwa na Mkutano mkuu na kuanza kazi mara watakaposajiliwa na Kabidhi Wasihi mkuu wa Serikali. Mkutano mkuu ndio utakuwa na mamlaka ya kumuondoa mjumbe/wajumbe wa Baraza la Wadhamini toka kwenye wadhifa huo baada ya kupata taarifa toka Bodi ya Wakurugenzi.

3. Wajumbe wa Baraza la Wadhamini ndio watakuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba Sports Club Holding Company Limited.

4. Baraza la Wadhamini litamiliki 99% ya hisa za Simba Sports Club Holding Company Limited kwa niaba ya Simba Sports Club na Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini atamiliki 1% ya hisa za Simba Sports Club Holding Company Limited kwa niaba ya Simba Sports Club.

Ibara ya 39: Ukomo wa Wadhamini

(a). Kufa, Kujiuzulu, kupata maradhi ya akili, kufungwa jela/magereza.

(b). Kuvuliwa nyadhifa na mkutano mkuu

(c). Bodi ya Wakurugenzi itawasilisha katika mkutano mkuu pendekezo la kumuondoa/kuwaondoa wadhamini watakaobainika ni chanzo cha migogoro ndani ya klabu au kama bodi ya wakurugenzi itakavyoona inafaa vinginevyo kwa maslahi ya klabu.

G. MATAWI YA SIMBA SPORT CLUB NCHI NZIMA

Ibara ya 40: (1) Matawi ya Simba Sprts Club na kazi zake

(a). Kutakuwa na uongozi wa matawi, wilaya na mikoa nchi nzima

(b). Matawi yote ya Simba Sports Club watalipa ada ya uanachama kila mwaka kwa kiwango kitakachopitishwa na MKutano mkuu baada ya mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi.

(c). Kila tawi litaruhusiwa kuwa na wanachama hai wasiozidi 250 na wasiopungua 50.

(d) Kila tawi litafanya uchaguzi wa uongozi wake utakaohusisha Mwenyekiti wa Tawi, Makamu Mwenyekiti wa tawi, Katibu mkuu wa tawi, Mweka Hazina na wajumbe watatu, mmoja kati yao awe mjumbe mwanamke ambao kwa ujumla wao ndio wataunda Kamati ya Utendaji ya tawi.

Itendelea.....................

Advertisement