Hizi mbio za usajili zinahitaji umakini kwa klabu na wachezaji

Muktasari:

  • Hii itasaidia kuwazuia wachezaji wanaohitajika na klabu hizo na pia kuwapata wale ambao wanapenda kuona wakiungana na wenzao ndani ya vikosi vyao kwa msimu ujao.

MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2018-2019 umesaliwa na mechi chache kabla ya kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu. Tayari vita ya ubingwa imesaliwa kwa klabu mbili za Yanga na Simba wanaopewa nafasi ya kulinyakua taji kwa mara ya pili.

Katika vita ya kushuka daraja, baada ya African Lyon kutangulia kwa sasa timu ya pili ya kuungana nayo imebaki kwa klabu kama sita ikiwamo Mwadui ya Shinyanga waliopo nafasi ya pili kutoka mwisho.

Nyingine zilizopo kwenye janga hilo ambalo hata kama watanusurika kushuka moja kwa moja bado watakuwa na kazi ya kujinasua katika Ligi Ndogo dhidi ya klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambazo zimeanza kuumana kwenye playoff.

Timu zilizopo kwenye mtego wa kuifuata Lyon ama kucheza playoff na timu za FDL ni Biashara United, JKT Tanzania, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Mbao ambazo zina wastani wa alama 37-43 katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20.

Wakati ligi ikiwa ukingoni tayari baadhi ya klabu zimeanza kuchangamkia usajili hata kabla halijafunguliwa kwa kuwasainisha mikataba mipya nyota wao ambao mikataba yao inaelekea mwishoni na pia kufanya mazungumzo na wachezaji wa timu nyingine.

Ni jambo zuri kwa klabu kuanza mazungumzo kwa wachezaji ambao ndani ya klabu zao na wale wa klabu nyingine wanaomaliza mikataba kwani kanuni ya usajili inaruhusu.

Hii itasaidia kuwazuia wachezaji wanaohitajika na klabu hizo na pia kuwapata wale ambao wanapenda kuona wakiungana na wenzao ndani ya vikosi vyao kwa msimu ujao.

Hata hivyo kitu cha muhimu ambacho Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo hasusani soka ni kuzikumbusha klabu kuepuka kufanya hila na ghiriba ya kuzungumza na wachezaji wa timu pinzani wasioruhusiwa kisheria ili kuepuka kujitibulia mapema.

Tunalisema hili kwa kurejea matukio ya siku za nyuma kwenye sajili kama hizo ambapo klabu na wachezaji wamejikuta wakijiingiza matatani kwa kufanya mazungumzo na hata kusainishwa mikataba wakati wakiwa na mikataba katika klabu zao inayowabana. Kadhalika wachezaji wanapaswa kuwa makini kwa kuzingatia muda wa mikataba yao ili kuepuka kujikuta wakijitia kitanzi na kuja kufungiwa kwa kufanya udanganyifu katika usajili wao kwa sababu ya tamaa ya fedha.

Ilishatokea misimu kadhaa nyuma kwa wachezaji kujikuta wakifungiwa kwa sababu ya kubainika wamesaini klabu nyingine ilihali wana mikataba na klabu zao walizokuwa wakizutumikia. Mfano mdogo ilimkuba Mohammed Mkopi ambaye alisaini Mbeya City, huku akijua kabisa ana mkataba na Prisons ama William Lucian ‘Gallas’ wa Ndanda aliyekaribia kufungiwa kwa kujisajili Mwadui. Kama sio huruma na busara za viongozi wa klabu hizo mbili na wale wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Gallas yangemkuta.

Lakini Hassan Kessy, Mrisho Ngassa ni baadhi ya wachezaji waliojikuta wakisimamishwa kwa muda kucheza misimu michache iliyopita kutokana na makosa ya usajili kutoka klabu moja kwenda nyingine wakiwa ndani ya mikataba.

Hivyo kwa kuwa kufanya kosa sio kosa bali kosa kurudia soka na vilevile mtu hujifunza kutokana na makosa, ni vyema klabu na wachezaji kwa ujumla kubwa makini kipindi hiki cha kuanza michakato ya usajili kabla dirisha halijafunguliwa ili kujiweka salama.

Katika dunia ya sasa kwanini klabu na wachezaji wawe wanaviziana badala ya kufuatilia na kufanya mazungumzo ya wazi na wachezaji sambamba na viongozi wa mchezaji kama kweli wanamhitaji ili kuepuka kujiingiza kwenye hasara isiyo ya lazima.

Tunaamini kama Yanga itakuwa inahitaji mchezai Simba, ama Simba wanamtaka nyota wa Yanga au Azam, waulizie kupata uhakika kama mkataba wake ukoje, iwe kwa wachezaji wenyewe na kujiridhisha kwa klabu husika ya mchezaji. Hatuoni sababu ya viongozi kuviziana na kukomoana katika kusajiliana wachezaji wakati kwa sasa biashara ya soka ni kama tu biashara nyingine na kila kitu lazima kiwe hadharani tena kwa maandishi.

Tunajua wachezaji wakati mwingine wanaingiwa na ibilisi na kujikuta wakijikataa kwa tamaa ya fedha wanazoahidiwa na klabu zinazowataka, lakini wakumbuke mikataba walioisaini katika klabu zao za sasa ndiyo inayowabana na wakizingua nayo itawazingua.

Tunaamini kila kitu kikifanyika kwa utaratibu na kuzingatia kanuni na sheria, hakuna litakaloharibika mbele ya safari na mwishowe mmoja akajuta.