Hiyo Simba ya kimataifa ijipange kuanzia sasa

Muktasari:

Simba huenda wakatangaza pia wale wanaowaacha ama kuwatoa kwa mkopo na kuanza rasmi maboresho yao ingawa mpaka sasa boresho moja pekee la beki wa kulia David Kameta 'Duchu' kutoka Lipuli ndilo linadaiwa kukamilika

SIMBA wamemaliza kazi ya msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara tatu mfululizo na kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC). Mbali na hilo msimu uliopita walitwaa pia ubingwa wa Ngao ya Jamii, hivyo kubeba mataji yote matatu yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Hiyo ni hatua kubwa kwa Simba, wameonyesha namna gani walidhamiria kutwaa makombe yote. Nia hiyo iliwekwa na Wanasimba kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki. Kwa ufupi walishirikiana kuleta mafanikio ndani ya Simba.

Kama kanuni zingekuwa zinaruhusu timu inayotwaa makombe mawili yanayoruhusu timu kushiriki michuano ya kimataifa inayoandaliwa na CAF, basi Simba ingeshiriki Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika. Lakini kwa sababu haziruhusu, basi Simba wanawapa nafasi Namungo ambao walicheza nao fainali ya kombe hilo wikiendi iliyopita Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga ambapo Simba ilishinda bao 2-1.

Hivyo basi kwa kuzingatia kanuni hiyo, Simba inabidi washiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo sasa wanatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha ili kuthibitisha thamani ya kiwango chao kimataifa.

Simba ni miongoni mwa timu ambazo zimefanya uwekezaji mkubwa ukiachana na Azam FC ambayo ndio inaongoza, lakini katika kufanya usajili Simba wapo juu zaidi kusajili wachezaji kwa gharama kubwa.

Yote hayo ni kutaka mafanikio ya kiwango cha juu ambayo yataendana na mfumo wa uendeshaji wa klabu ambao ni wa kisasa.

Pamoja na kutwaa makombe hayo, bado Simba inahitaji kuboresha kikosi ili wakiingia kwenye michuano hiyo mikubwa wasiishie hatua za awali kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo waliishia hatua ya awali ukiachana na mwaka juzi waliofika hatua ya makundi.

Kwa namna ambavyo usajili unaendelea baada ya TFF kufungua dirisha la usajili, Simba wameonekana kutokuwa na haraka na usajili wao na walisema watafanya maboresho madogo tu.

Timu kama Yanga na Azam ndizo zimeonyesha kuwa na uhitaji wa wachezaji wengi ambao wengine tayari wamemwaga wino na kutangazwa, huku Yanga ikiweka wazi wachezaji 14 walioachana nao.

Simba huenda wakatangaza pia wale wanaowaacha ama kuwatoa kwa mkopo na kuanza rasmi maboresho yao ingawa mpaka sasa boresho moja pekee la beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ kutoka Lipuli ndilo linadaiwa kukamilika.

Simba wana kazi kubwa, tena kubwa kweli kweli kuhakikisha wanafikia malengo yao msimu ujao kwenye michuano hiyo, huu sio muda wa wao kukosea katika maboresho ya kikosi chao.

Bosi wao Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amesema timu nzuri hazihitaji kusajili sana, ni kweli inawezekana kauli yake ina ukweli mtupu, lakini bado katika huo usajili wao mdogo unahitaji umakini mkubwa.

Wanapaswa kusajili nafasi zile ambazo zina mapungufu tu, tena wachezaji watakaowasajili ni wale wenye viwango vya hali ya juu kuliko waliopo na wasiboreshe kikosi kwa kusajili wachezaji ambao wataishia jukwaani ama kusugua benchi.

Endapo watafanya hivyo kwa kusajili wachezaji ambao viwango vyao vitakuwa vya kawaida na hawakuwa na ushindani basi watakuwa wameikosea sana Simba inayotarajiwa kuonwa kwenye levo nyingine zaidi ya hapo ilipo.

Simba sasa inapaswa kuonyesha kwamba makombe matatu waliyoyapa ndani ya msimu mmoja hawajabahatisha bali wana uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya hapo.

Wanatajwa wengi sana kutua Simba lakini kati ya hao huenda ni wachache sana watakaobahatika kuvaa uzi mwekundu msimu ujao.

Michuano hiyo ya kimataifa nayo inaendelea mwaka huu huu ambao ligi ya hapa nchini inaanza hivyo muda wa maandalizi utakuwa mdogo, hivyo kama watafanya mabadiliko makubwa ya kikosi basi itawagharimu kwani kikosi kitakuwa hakijapata muunganiko wa kutosha.

Viongozi wa Simba wasimamie kwenye malengo yao ya kuboresha safu ambazo wanaona zina mapungufu kupitia ligi iliyopita tu.