Hivi wamiliki wa Azam wanajisikiaje?

Muktasari:

Miaka sita hadi minane iliyopita ukisikia kuna mechi ya Simba au Yanga na Azam, ulikuwa unajua kabisa kwamba hiyo mechi ina vita ndani yake. Vijana wa Chamazi walikuwa na timu iliyotimia kila idara.

BAO la kwanza la mechi baina ya Simba na Azam FC iliyochezwa wiki hii jijini Dar es Salaam lilifungwa na John Bocco. Kwa wasiojua, Bocco ni mchezaji ambaye si tu ametengenezwa na Azam lakini ameichezea tangu ikiwa katika madaraja ya chini kabisa.

Kama kuna mchezaji wa Azam anayestahili heshima ya kuitwa gwiji wa klabu; yeye na mmojawapo katika kundi la wachezaji wasiozidi watano.

Hakuwa mchezaji wa kawaida wakati wake. Alikuwa mfungaji bora, nahodha na mtu ambaye ungeweza kumwita shabiki wa Azam. Alikuwa akizifunga timu kubwa kiasi kwamba washabiki wa Simba na Yanga walikuwa na tabia ya kumzomea wakati akichezea timu ya taifa.

Miaka mitatu iliyopita, Azam ilimruhusu ahamie Simba. Tangu Bocco aondoke Azam unajua klabu hiyo imechukua mara ngapi ubingwa wa Ligi Kuu?

Mara sifuri. Zero. Zilch. Nada.

Katika mechi hiyohiyo, unajua nani alitengeneza bao la pili? Shomari Kapombe. Kabla ya kuhamia Simba, unakumbuka alikuwa mchezaji wa klabu gani? Umepatia. Jibu ni Azam FC.

Kama mtu atataka kutafuta mchezaji nyota wa mechi ile, wapo watakaomtaja Kapombe ambaye anaamini kuwa ndiye mlinzi bora wa kulia hapa nchini kwa sasa.

Mlinda wa Simba ambaye hakuruhusu bao kwenye ile mechi anaitwa Aishi Manula. Kabla ya Simba, kijana huyu pia alikuzwa na kulelewa Azam.

Alipoumia mlinzi Kennedy Juma, makocha wa Simba hawakupata tabu ya kutafuta wa kubadilishana naye. Aliingia Erasto Nyoni kuchukua nafasi. Hata nisipoandika, unaweza kuhisi tu Erasto alitoka wapi. Labda nikusaidie. Azam FC.

Miaka sita hadi minane iliyopita ukisikia kuna mechi ya Simba au Yanga na Azam, ulikuwa unajua kabisa kwamba hiyo mechi ina vita ndani yake. Vijana wa Chamazi walikuwa na timu iliyotimia kila idara.

Wangekuwa na Manula langoni, wangekuwa na kina Said Morad, Joakins Atudo na huyu Aggrey Morris kwenye ngome. Wangekuwa na watu kama Abdulhalim Humoud, Kipre Bolou na Himidi Mao kwenye kiungo na Kipre Tchetche na Bocco wakishambulia.

Haikuwa timu inayokuvutia machoni kwa mchezo mzuri; ukiondoa kipindi kifupi walichokuwa chini ya kocha Boris Bunjak – lakini Azam ya Stewart Hall au Joseph Omog ilikuwa ni patashika nguo kuchanika.

Na jambo la muhimu kuliko yote; hakuna kiongozi wa Simba aliyetaka kupora mchezaji wa Azam FC kwa sababu wakijua klabu hiyo ina uwezo wa kulipiza kisasi na kuchukua mchezaji yeyote iliyemtaka wakati huo.

Kukawa na heshima mjini. Ndiyo sababu, hata alipoondoka Kipre Tchetche ilikuwa kwenda ughaibuni na si mojawapo ya timu mbili kubwa za jijini Dar es Salaam.

Najaribu kutafakari nini hasa yalikuwa maono ya wamiliki wa Azam FC kufikiri kwamba wanaweza wakawaacha wachezaji wao nyota na kusajili wengine.

Bocco, kwa sasa, pengine ndiye mshambuliaji pekee wa Kitanzania mwenye wastani wa kufunga mabao 15 kwa msimu. Tangu kustaafu kwa kina Emmanuel Gabriel, Bocco ndiye amebaki pekee wa daraja hilo miongoni mwa Watanzania.

Nani alidhani kwamba kuachana na mchezaji wa namna hii kunaweza kuwa na faida yoyote kwa Azam FC? Na afadhali ingekuwa Bocco peke yake; Na Erasto? Na Kapombe? Manula?

Kitendo hiki kilikuwa sawa na klabu kama Barcelona itake kusonga mbele na katika mapendekezo yake waseme wanataka Messi, Ter Stegen, Suarez na Busquets wapunguziwe mishahara au gharama zao za kusajiliwa zipunguzwe. Watu wa Barcelona wangeandamana siku hiyibiyo.

Kila nilipokuwa nikitazama mechi ile ya wiki hii kati ya Simba na Azam, nilifadhaika tu na kiwango cha ubora cha Azam. Hawakucheza vizuri na Wekundu wa Msimbazi wangeweza kuwafunga kwa idadi kubwa ya mabao kuliko hiyo 2-0 tuliyoishuhudia.

Mimi ni mmoja wa Watanzania wanaoamini kwamba wakati Azam FC inapokuwa bora, mfumo wetu wa kuendesha soka nao unakua.

Tanzania inahitaji Azam bora. Tunataka kuiona tena Azam iliyokuwa na ndoto ya kutwaa ubingwa wa Afrika. Sijajua nini wamiliki wake wanawaza vichwani kwao kwa sasa lakini najua kwamba Azam inaweza kabisa kutimiza ndoto zake kubwa.

 

Wasemaji wa Klabu

Nimewahi kuwa msemaji wa klabu huko nyuma na najua uchungu na utamu wake. Ninajua pia kwamba ni jambo la kawaida kwa ulimi au kalamu ya kuandikia kuteleza.

Nimemsikia Thabit Zakaria wa Azam na Haji Manara wa Simba wakilumbana katika vyombo vya habari na mitandao wiki hii.

Ningewaomba mahasimu hawa wawili warudishe visu kwenye ala zao badala ya kuendekeza malumbano ambayo yanawaweka pagumu sana.

Nawafahamu wote kuwa ni watu mahiri. Wanachokifanya sasa kinaweza kuathiri taaluma hii ya usemaji kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo. Washikane mikono, wanywe chain a tuendelee na mambo mengine.