Hivi sio mechi za kuzikosa kabisa!

Monday July 23 2018

 

By THOMAS NG’ITU

DIRISHA la usajili limebakisha siku chache kabla ya kufungwa rasmi, huku baadhi ya timu zikizidi kutanua vikosi vyao kwa kusaini vifaa vipya ili kuongeza ushindani na sio kushiriki tu Ligi Kuu.

Wakati dirisha hilo likielekea ukingoni, nayo Bodi ya Ligi (TPLB) imetoa ratiba mapema ili kila timu iweze kujua itakutana na nani na kujipanga mapema kwa lengo la kufanya vizuri msimu ujao.

Mwanaspoti kupitia ratiba iliyotolewa katikati ya wiki iliyopita imeangalia na kuona kuna michezo ambazo shabiki wa soka hapaswi kuzikosa kwa namna yoyote.

Hizi ni mechi zenye mvuto, msisimko na ushindani wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na mechi za ‘derby’ na hata ule upinzani tu baina ya timu na timu. We chungulia hapo chini uone mambo.

ALLIANCE vs MBAO FC

Kama kuna sapraizi iliyoifanya TPLB, ni kuliweka pambano hilo la ‘derby’ ya Jiji la Mwanza mapema.

Hii ndio ‘derby’ ya mapema katika Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 ikihusisha Alliance iliyopanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza dhidi ya Mbao FC wazoefu wa ligi hiyo kwa msimu wa tatu sasa.

Mechi hiyo imepangwa kupigwa Agosti 22, yaani siku ya ufunguzi wa msimu mpya kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Hii ni mechi ngumu kwa timu zote kwa vile Alliance imepanda ikichukua nafasi ya Toto Africans na mashabiki watakuwa na hamu ya kutaka kuona imekuja kuleta kitu gani kipya.

Kali zaidi ni kwamba timu zote zipo chini ya mdhamini mmoja, hivyo Alliance itataka kuwaonyesha wadhamini wao kwamba wana kitu cha ziada, lakini Mbao nayo itataka kuionyesha Alliance kwamba wao ndio wababe wa Mwanza kwenye Ligi Kuu.

Timu hizo zitarudiana tena Januari 5, 2019 kama hakutakuwa na mabadiliko na bila shaka, timu yoyote itakayozubaa mbele ya mwenzake ijue kabisa itaumia kweupeee!

SIMBA vs YANGA

Mpaka sasa Simba imefanya usajili wa maana kuliko Yanga na mashabiki wa soka wana hamu kubwa ya kuishuhudia ‘derby’ ya Kariakoo wakati miamba hiyo itakapokutana kwa mara ya kwanza.

Bodi ya Ligi imeipanga mechi hii kupigwa kwa mara ya kwanza Septemba 30, kabla ya kurudiana tena kama hakutakuwa na mabadiliko Februari 16, mwakani.

Bila ya shaka hii sio mechi ya kuikosa kutokana na upinzani wa timu hizo na hali ilizonazo kwa sasa zikitofautiana mno.

Mashabiki walikuwa na hamu ya kuiona ‘derby’ ya mapema katika SportPesa Super Cup 2018 kule Kenya, lakini Yanga ikatolewa mapema. Wakasubiri na kuamini zingekutana katika Kagame Cup 2018 baada ya Cecafa kuzipanga kundo moja, lakini Yanga ikachomoa. Ilijitoa michuanoni na kuongeza kiu kwa mashabiki wa kutaka kuona pambano hili la watani, bila shaka siku hiyo itakuwa kazi.

PRISONS vs MBEYA CITY

Hii ni ‘derby’ ya Jiji la Mbeya. Jiji hilo husimamisha shughuli zake kwa muda ili kupisha pambano hili la Banyambala ambalo wakati mwingine humalizika kwa mashabiki wao kuonyeshana utemi.

Pambano la kwanza limepangwa kupigwa Oktoba 6 kabla ya kurudiana tena Februari 20 mwakani palepale Uwanja wa Sokoine na kwa namna klabu hizo zilivyotofautiana kwa sasa kazi ipo.

Hakuna anayejua kama ni Kocha Abdallah Mohammed ‘Bares’ wa Prisons ama Mrundi Ramadhan Nswazurwimo wa City atakayecheka safari hii.

MTIBWA SUGAR vs KAGERA SUGAR

Pambano hili ni derby ya tamtamu, zote zinamilikiwa na viwanda vya sukari vyenye uhusiano na huwa na mvuto wake kwa mashabiki.

Msimu uliopita Mtibwa ilikuwa bora dhidi ya Kagera Sugar. Hakuna anayejua msimu ujao itakuwaje kwani zitaanza kunyooshana kazi Oktoba 28 kabla ya kurudiana Machi 16 mwakani.

Bila shaka ni bonge la gemu ikizingatiwa Mtibwa msimu ujao itapanda ndege kuiwakilisha nchi kimataifa baada ya kubeba taji la FA na makocha wote walicheza pamoja pale Manungu. Kocha Mecky Mexime wa Kagera na Zubeir Katwila wa Mtibwa.

STAND UNITED vs MWADUI

SHY Derby ndio mpango mzima ambapo mashabiki wa soka Mkoa wa Shinyanga linapokuja pambano hili ni kama vile Simba na Yanga.

Timu hizo zina upinzani tangu safari yao ya kupanda Ligi Kuu msimu kadhaa iliyopita wakipishana kwa msimu mmoja. Mechi yao ya kwanza msimu huu itapigwa Oktoba 29. Chama la Wana likiwa nyumbani Kambarage kabla ya kuwafuata wapinzani wao Mwadui katika mechi ya marudiano Machi 15 mwakani. Patamu!

JKT TANZANIA vs RUVU SHOOTING

Hili ni pambano la Maafande ni vita ya Mchawi Mweusi, Bakar Shime na Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ wa Ruvu. Pambano la timu hizi huwa na mvuto kutokana na ushindani mkubwa waliokuwa nao.

TPLB imepanga kuzikutanisha mechi ya kwanza Siku ya Ukimwi, Desemba Mosi kabla ya kurudiana na Mei 3 mwakani.

AZAM VS AFRICAN LYON

Derby hii ya TMK ni tamu kinoma. Timu hizi zimekuwa na ushindani kwa muda mrefu, japo Lyon imekuwa ikiingia na kutoka Ligi Kuu. Safari hii imerudi tena na kazi itakuwapo zitakapokutana, japo inategemea na Lyon ilivyojipanga.

Mechi ya kwanza itapigwa Oktoba 20 kabla ya kumalizana tena Machi Mosi mwakani na timu yoyote itakayozubaa lazima iumie.

MECHI NYINGINE

Mechi nyingine ambazo zinatarajiwa kuwa kali ni kati ya Singida dhidi ya Yanga na hasa kutokana na sakata linaloendelea na kumgombea kiungo Feisal Salum.

Yanga imekuwa ikitaabika kwa Singida enzi za Hans Pluijm na hata miaka ya nyuma, hivyo safari hii itakapokutana kwa mara ya kwanza msimu huu Septemba 23 na kurudiana tena Februari 6 mwakani ni wazi kazi itakuwa sio ya kitoto. Ngoja tuone itakavyokuwa.

Coastal Union dhidi ya Mbeya City nayo sio ya kuikosa kwa jinsi timu hizo zilivyojengeana upinzani usio wa kawaida kutokana na matukio mbalimbali ya mechi zao za nyuma kabla Wagosi hawajashuka daraja.

Vurugu walizofanyiwa Mbeya City Mkwakwani na utata wa mechi yao ya marudiano msimu wa 2015-2016 inaifanya mechi hii nayo kuwa sio ya kukosa kama ilivyo ile ya Mbao na Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Mbao imekuwa ikitesa Yanga tangu ipande VPL kwenye uwanja huo, je, safari hii itakuwaje. Hatujui!

Advertisement