Hivi huyu Kagere mnamjua lakini...!

Friday January 11 2019

 

By MWANDISHI WETU

HAKUNA ubishi, straika Meddie Kagere hajafunga bao la Ligi Kuu Bara tangu alipofunga bao lake la mwisho katika ligi hiyo Novemba 3, 2018. Hata hivyo huwezi kumbeza straika huyo, kwani huko kwenye michuano mingine nyota huyo wa Simba ameendelea kutupia akizidi kuboresha rekodi yake Msimbazi.

Kagere aliyesajiliwa Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya alifunga mabao yake ya mwisho katika Ligi Kuu wakati timu yake ikiizamisha JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda mabao 2-0, yote yakiwekwa kimiani na straika huyo Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda na baada ya hapo mabao yakakauka mguuni mwake katika ligi hiyo ilipo duru la pili kwa sasa.

Hata hivyo ni kwamba Kagere ameendelea kufunga kwenye michuano mingine na hivi unavyosoma, tayari ana mabao 17 katika michuano yote ambayo ameichezea timu hiyo, yakiwamo mawili aliyofunga wiki iliyopita kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019 iliyopo hatua ya nusu fainali kwa sasa.

Straika huyo alifunga mabao hayo mawili wakati Simba ikiichapa Chipukizi mabao 4-1, ikiwa ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi ndani ya kikosi cha Msimbazi kwa msimu huu akiwafunika hadi Emmanuel Okwi na John Bocco waliotamba msimu uliopita.

Rekodi zinaonyesha mabao 17 ya Kagere yamefungwa ndani ya miezi mitano na ushei katika mashindano matano tofauti, yakiwamo saba ya Ligi Kuu aliyoyafunga dhidi ya timu tano kati ya 17 ambazo zimevaana na timu yake.

Kagere amezifunga, Prisons (1), Mbeya City (2), Mwadui (1), Ruvu Shooting(1) na JKT Tanzania (2).

Pia Kagere amefunga mabao manne katika michuano ya Kombe la Kagame 2018 dhidi ya timu nne tofauti na kufunga mengine matatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, mawili dhidi ya Mbabane Swallows na moja akiwatungua Nkana FC.

Kagere amefunga pia bao moja katika mechi ya Ngao ya Jamii na kusaidia kuwapa taji dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi iliyopigwa CCM Kirumba na hivi karibuni alifunga mawili kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019 dhidi ya Chipukizi ya Pemba.

Kagere hakucheza mechi mbili zilizofuata za Simba kwenye Mapinduzi na kuzua hofu kwamba huenda akawa majeruhi, lakini mabosi wake wamesisitiza yupo fiti na ametulizwa ili kuwavutia kasi Waalgeria watakaovaana nao kesho kwenye mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

MSIKIE MWENYEWE

Kagere amesisitiza amekuja Tanzania kufunga mabao, hivyo haijalishi anashiriki mechi za aina gani, kwani hata kwenye michezo ya kirafiki tangu akiwa Uturuki alifunga pia mabao, hivyo sio kitu cha ajabu kwa mchezaji wa kariba yake.

“Kazi yangu ni kufunga. Simba ilinisajili ili nifunge na ndio maana kila mechi nikipata nafasi nafunga ili kuhakikisha timu yangu inapata mafanikio. Siwezi kusifiwa kama sifungi,” alisema straika anayeichezea pia timu ya taifa ya Rwanda, ‘Amavubi’.

Straika huyo kesho atakuwa na kibarua kingine cha kuisaidia timu yake katika mechi yao ya kwanza ya makundi watakapovaana na JS Saoura ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika michuano hiyo ya CAF, Kagere analingana mabao na John Bocco, huku kiungo Clatous Chama akiongoza orodha ya nyota wa klabu hiyo akiwa na mabao manne.

Advertisement